Je! Shetani alitolea wapi uovu?

by Admin | 8 February 2020 08:46 pm02

SWALI: Ikiwa Mungu aliviumba viumbe vyake vikiwa vikamilifu Je! Shetani alitolea wapi uovu?. Na Je! ni nani aliyeiumba  dhambi?.

JIBU: Kitu chochote kizuri tunachokiona,  mpaka tumejuwa kuwa ni kizuri basi tujue kuwa ni lazima kilikuwepo  kingine kibaya  ambacho kimeuthibitisha uzuri wake..kwamfano unapolamba sukari mpaka umejuwa kuwa sukari ni tamu ni kwasababu ulishakutana na kitu kama chumvi huko nyuma chenye ladha tofauti n hiyo , au unapouona mwanga, mpaka umejua kuwa  hii ni nuru, ni kwasababu ulishawahi kuliona giza huko nyuma ndipo ukaweza kuielewa vizuri nuru ni nini, kamwe usingekaa ujue kuwa huu ni mchana kama usingekaa uuone usiku ulivyo, usingekaa ujijue kama wewe una afya kama usingewahi kuugua..Na vitu vingine vyote tunavyoviona ni vizuri vivyo hivyo..Utagundua kuwa kibaya kipo kwa lengo la kukithibitha kizuri,  mpaka kujua huyu mtu anayo hekima, ni kwasababu mpumbavu yupo, mpole-kwasababu mkali yupo, mpaka kujua kuwa kuna mrefu ni kwasababu mfupi yupo, mweupe-kwa-mweusi, mwanamke-kwa -mwanaume..n.k.

Sasa Mungu alipoanza kuviumba viumbe vyake, aliviumba vyote vikiwa vikamilifu, ndipo hapo akawauumbia WEMA ndani yao, lakini hakuishia hapo tu, alitaka pia wajitambue kuwa wao ni wema, na hivyo wazidi kuupenda wema ndipo hapo akauumba na UBAYA pia, ili uuweze kuuthibitisha wema..

Hivyo tangu mwanzo malaika zake walipewa Ujuzi huo wa kuweza kujua mema na mabaya..Ili kusudi kwamba wazidi kuupenda wema  waliokusudiwa kuwa nao, na kuuzidi kuuchukia ubaya usiowafaa.

Ndipo hapo sasa, Malaika wakawa wanajua sasa ili sisi tuwe watakatifu kama Mungu ni lazima tuchukie matendo  yasiyoendana na utakatifu, ili tuwe wema ni lazima tuukatae ubaya wa kumchukia malaika mwenzetu na Mungu wetu, ili tuwe wakweli ni lazima tusisemezane uongo sisi kwa sisi….

Isaya 45:7 “Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote”.

Maombolezo 3:38 “Je! Katika kinywa chake Aliye juu Hayatoki maovu na mema”?

Lakini sasa mambo yakaja kubadilika baadaye..Baadhi ya malaika, wakiongozwa na baba yao shetani, wakaanza kukengeuka, wakawa wanataka kuijitawala wenyewe, hivyo wakaona ni bora wachague yale mabaya ili  kutimiza adhma yao, sasa badala ya kupenda wakaanza kuchukia, wakawachukia malaika wenzao waliomtii Mungu vilevile wakamchukia na muumba wao aliyewaumba wao,  wakaanza kusema uongo, wakaanza kuharibu n.k.

Hapo ndipo dhambi ilipopata nguvu ndani yao, wakapungukiwa na utukufu wa Mungu, wakaonekana ni waovu, wakafukuzwa watoke mbinguni katika makao ya Mungu matakatifu.

Hivyo ukiuliza  uovu ulitoka wapi, fahamu kuwa ouvu na wema viliumbwa vyote pamoja viliumbwa na Mungu kila kimoja kikae katika sehemu yake kutimiza kusudi lake..Lakini wale waliokengeuka walipoupenda ubaya zaidi ya wema ndipo wakaonekana wakosaji…Hivyo shetani alitolea wapi uovu?..jibu> aliumbiwa nao.

Hata sasa, iwe wewe ni mkristo au sio mkristo, ujuzi huo wa mema na mabaya upo ndani yako tangu Edeni. Ulikuwa ni Mpango wa Mungu kabisa ubaya uwepo ndani ya mtu kwa makusudi maalumu mema.. Sasa ni jambo la wewe kuchagua moja kati ya hilo, ukipenda wema basi utajitahidi ukae mbali na ubaya, vivyo hivyo ukiupenda ubaya basi utafanya juu chini uwe mbali na wema.

Yohana 3:19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.

20 Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.

21 Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu”.

Lakini sisi tuliokoka tumeipenda Nuru, a ndio maana hukumu ya Mungu haipo juu yetu…kama maandiko yanavyosema katika Warumi 8:1

 Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

NI KWASABABU YA YESU KRISTO.

JE WAJUA?

TOFAUTI KATI YA HEKALU, SINAGOGI NA KANISA NI IPI?

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

TUMAINI NI NINI?

MAMBO 5 AMBAYO KILA MKRISTO ANAPASWA KUFAHAMU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/02/08/je-shetani-alitolea-wapi-uovu/