by Admin | 13 February 2020 08:46 pm02
Kusudi la Mungu ni lipi?
Jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze maneno ya uzima,
Baadhi yetu tunadhani mpaka Mungu atakapotuambia tufanye hivi au tufanye vile ndipo hapo tutakuwa na uhakika kuwa tunalolifanya ni kusudi la Mungu,… Lakini Jambo lingine ambalo pengine hatufahamu ni kuwa kila wazo au kusudi tunalolifanya liwe ni jema au ni baya..ndani yake limebeba kusudi la Mungu..Hata shetani alipoingiwa na wazo la tamaa la kuwa kama Mungu, mpaka akaleta migogoro kule mbinguni, na baadaye akatupwa huku chini duniani na kuendelea na uharibifu wake, alikuwa analitimiza kusudi la Mungu.. na ndio maana Mungu hakumuua tangu ule wakati hadi sasa..Ni kwasababu anayohuduma yake hapo, Siku atakapomaliza kusudi lote la Mungu ndipo atakapoharibiwa katika lile ziwa la Moto.
Yuda alipoingiwa na wazo la kumsaliti Bwana Yesu, Ni kweli lilikuwa ni wazo bovu lakini ndani yake, kulikuwa na kusudi la Mungu timilifu kabisa, ilikuwa ni lazima iwe vile ili Kristo asulibiwe tupate wokovu..Ipo mifano mingi ya namna hiyo katika biblia mfano Farao kuwa na moyo mgumu, Samsoni kwenda kuwapenda wanawake wa kifilisti, n.k.
Leo tutatazama tena katika maandiko, Taifa lingine ambalo Mungu alilichagua kufanya mapenzi yake ya kuyapiga mataifa, japo lilikuwa halijui kuwa linaifanya kazi ya Mungu…Na kupitia hilo ndio tutajifunza somo letu la leo.
Isaya 10:5 “Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu!
6 Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani.
7 Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache.
8 Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme?”.
Kwa ufupi taifa hili la Ashuru enzi za wafalme lilikuwa ni moja katika ya mataifa matatu yenye nguvu duniani..mengineyo yakiwemo Misri, na Babeli..Ni sawa na leo Marekani, Urusi na China jinsi yalivyo na nguvu za kijenzi duniani.. Ndivyo ilivyokuwa wakati huo..
Sasa kama wewe ni msomaji wa biblia utagundua kuwa Hili taifa la Ashuru lilikuwa ni kubwa, na lenye nguvu sana kijeshi, hili ndio Mungu alilolitumia kulichukua taifa la Israeli utamwani(yale makabila yote 10), na lile moja lililosalia ndio lilikuja kuchukuliwa utumwani na babeli baadaye..
Na sio tu Israeli peke yake, hapana, bali ukisoma biblia utaona liliyapiga na mataifa mengine mengi sana..kama biblia inavyotuambia hapo sio machache. Na ni Mungu mwenyewe alilinyanyua liwe na nguvu kiasi hicho ili alitumie hilo kuyapiga hayo mataifa yote ambayo yalikuwa yanaabudu sanamu.
Lakini sasa..ukisoma kwa makini mstari wa 7 unasema.. Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu…
Unaona?..moyoni mwake alikuwa hafikirii kuwa ndiye Mungu anayemtumia kulipiza kisasi, bali yeye alikuwa anafiriki kuwa anayakomesha yale mataifa yaliyokuwa hayamtii, au alikuwa anawaza kujiongezea tu himaya yake,..apate mali nyingi na mateka mengi..Hivyo akawa anafanya kwa bidii sana na kwa jinsi alivyokuwa anafanya bidii Zaidi kutaka awe ngome thabiti kwa kuyapiga mataifa ndivyo alivyokuwa analitimiza kusudi la Mungu kirahisi Zaidi pasipo yeye kujijua…
Na ndio maana Bwana Yesu alimwambia Yuda…uyatendayo uyatende upesi..(Yohana 13:27)..Yaani yale maazimio mabovu yaliyokuwa ndani yake ya kutaka apate pesa kwa kumsaliti Bwana ayafanikishe upesi kwasababu kwa kupitia hayo ataharikisha pia kusudi la Mungu lifanyike haraka..
Lakini hawa wote tunaona mwisho wao ulivyokuja kuwa mbaya..Mataifa hayo yalikuja kuangamziwa vibaya..vilevile na Yuda..
Sasa nachotaka uone ni kuwa kanuni hiyo hiyo, wakati mwingine ndiyo Mungu huwa anayoitumia hata kutimiza mapenzi yake makamilifu ndani ya watu wake.
Mungu akitaka kufanya jambo lolote jema, labda tuseme la kumwokoa mtu fulani mlevi aliyeshindakana.. kwanza ataanza atamnyanyua mtu fulani..Na mtu huyo hajui kuwa ametumwa kwa mlevi, yeye akilini mwake anaweza kufikiri labda ni mtu tu fulani pale stendi……Lakini kumbe ndani yake anakwenda kulitimiza kusudi la Mungu alilolipanga juu ya mlevi Fulani aliyeko mahali pale.
Kwamfano anaweza ukasema ngoja nitoke nikasambaze kipeperushi vya injili stendi ya mabasi..Akatoka na vitano, akawapa watu 5 kisha akaondoka zake, mmoja wa wale 5 akawa sio mkristo, akakichukua akakisoma kisha akakiacha pale pale stendi kwenye daladala..Na baada ya muda mfupi akaja mtu mwingine akakiona kwenye siti kikamvutia akakichukua akaenda nacho nyumbani..akakiweka kwenye kabati ikapitia hata miaka 2,siku moja mume wake ambaye ni mlevi ametoka bar, akiwa katika kuyatafakari Maisha yake ya dhambi, akajisema moyoni Eee Mungu, Kama wewe unanipenda mimi basi naomba unionyeshe ni nini cha kufanya..Na saa hiyo hiyo wakati anayafikiria hayo anafungua kabati lake atafute biblia anakutana na kile kipeperushi ulichokisambaza wewe miaka 2 iliyopita, na ndani yake anakutana na ujumbe ambao ulikuwa unaendana na jambo lile lile alilokuwa anamwomba Mungu…Na mlevi huyo usiku huo huo anampa Bwana Maisha yake.. Na mbingu inaandika wewe umelitimiza kikamilifu kusudi la Mungu alilokupa la kwenda kumuokoa mlevi..ingawa wewe hujui chochote kinachoendelea.
Lakini ilikuwa ni sharti kwanza wazo fulani jema liingie ndani yako, kisha kwa kupitia hilo ulitimize kusudi la Mungu ambalo ulikuwa hujui ni lipi..Huo ni mfano tu..
Kwahiyo hivyo ndivyo Mungu anavyotimiza mapenzi yake kwa kupitia watu..Hatuwezi kuijua kazi yote ya Mungu..na ndio maana biblia inatuambia..
Mhubiri 11:4 “Mwenye kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna.
5 Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika HUIJUI KAZI YA MUNGU, AFANYAYE MAMBO YOTE.
6 Asubuhi panda mbegu zako, Wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa,kama ni hii au hii,au kama zote zitafaa sawasawa”.
Hivyo sisi tukijitoa kufanya kila kitu chema kinachohusiana na kazi yake, basi huko huko ndipo atakapotimiza kusudi lake alilolipanga kwa watu wake..
Na tena tukifanya kwa bidii Zaidi ndivyo Mungu atakavyotutumia Zaidi kutimiza makusudi yake..Kwahiyo kama wewe unahubiri basi ongeza bidii Zaidi katika kuhubiri kwako, usiangalie ni matunda mangapi leo hii nimeyapata kwa Kristo au la, maadamu unachokifanya kinaleta manufaa katika ufalme wa mbinguni, endelea usianze kujiuliza uliza, je ni kweli ninafanya mapenzi ya Mungu au la..Wewe fanya tena kwa bidii sana..na huko huko Mungu atakafanya kazi zake mwenyewe..Hivyo anza sasa kutumika..kwa kile Mungu alichokukirimia.
Lakini kama wewe ni mwovu kama lilivyokuwa taifa la Babeli, na Misri na Ashuru, ambayo baadaye baada ya kumaliza kusudi la Mungu la kuyapiga mataifa mengine, nayo pia yaliharibiwa..pamoja na Yuda na ibilisi mwenyewe siku ya mwisho, ndivyo itakavyokuwa na kwako, wewe ambaye unawapiga wengine, unawadhulumu wengine, unawaibia, unawasambazia ukimwi kwa makusudi mwisho wako utafika, pengine Mungu anaweza kukutumia kuwaadhibu hao lakini na wewe hutasalimika.. Mungu atakupiga na utakwenda Jehanaumu, na kule kitengo chako kitakuwa ni kikubwa Zaidi…Ni heri ukatubu dhambi zako sasa, Ili uokolewe.
Anza kuwaza vema kuyatenda yale yampendezayo Mungu.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/02/13/nifanye-nini-ili-nilitimize-kusudi-la-mungu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.