NI NANI ALIYEWALOGA?

by Admin | 26 February 2020 08:46 pm02

Ni nani aliyewaloga?..Je! nini maana ya kulogwa? na je! wewe nawe umelogwa?

Unaweza kujiuliza swali je! watu wa Mungu wanalogwa?..Jibu ni Ndio! Biblia inasema hivyo wanalogwa..Sasa ni kwa namna gani wanalogwa? Leo tutajifunza ni kwa namna gani wanalogwa.

Kulogwa kwa watu wa Mungu ni tofauti na kule kunakotafsiriwa na watu wa kidunia…Leo ukizungumzia neno kulogwa au kuloga moja kwa moja tafsiri yake ya kwanza inayodhaniwa ni “uchawi ” unahusika….Mtu ambaye hana fedha ni rahisi kudhaniwa kuwa kalogwa kwa nyakati zetu hizi, mtu ambaye ana ugonjwa unaodumu muda mrefu kulingana na kizazi cha sasa ni amelogwa, mtu ambaye ana tatizo la akili huyo kalogwa moja kwa moja, mtu ambaye ana udhaifu fulani ni lazima atakuwa amelogwa n.k

Lakini leo tututazama maana kuu ya neno “kulogwa” kibiblia..yaani kulogwa hasaa ni kupi?

Tusome..

Wagalatia 3:1 “Enyi Wagalatia msio na akili, NI NANI ALIYEWALOGA, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?

2 Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

3 Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?”

Ukisoma kitabu hicho cha Wagalatia karibia chote utaona Mtume Paulo kwa uweza wa Roho alikuwa akiwakemea sana wakristo hawa waliokuwepo huko Galatia..KUHUSU MWENENDO WAO WA KUIACHA IMANI, NA KUCHUKULIWA NA MAFUNDISHO MENGINE MAGENI…Wagalatia hawa walianza vizuri na Mungu, walianza kwa kumwabudu Mungu na kushika mafundisho ya kweli ya kumhusu Yesu Kristo, kama walivyofundishwa na Mitume..Lakini baadaye kidogo ghafla wakaanza kuingiliwa na mafundisho mageni na kuyaamini, na kuacha Imani ya kwanza ya kweli ya neno la Kristo.

Hivyo hiyo tabia ya kuiacha Imani ya kwanza na kugeukia mafundisho yadanganyayo ndiyo inayofananishwa na “kulogwa” kibiblia….Na hakuna kulogwa bila mlogaji…Hivyo waliokuwa wanawaloga wakristo hawa waliokuwa Galatia ni waalimu wao wa uongo waliokuwa wanazuka, waliokuwa wanalipindua Neno la Mungu, na kuwafanya watu waenende kidini Zaidi badala ya kuenenda katika kweli ya Neno la Mungu, wanawafundisha watu waishike torati kidini, mambo ambayo ni kinyuma na misingi ya imani iliyo katika Kristo Yesu…hawa ndio wale Mtume Paulo aliwazungumzia katika..

Wafilipi 3:18 “Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo;

19 mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani.

20 Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;

21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake”

Watu hawa Mtume Paulo alisema kwa uweza wa Roho kwamba wamelaaniwa ukisoma mwanzoni kabisa mwa kitabu hichi cha Wagalatia..

Wagalatia 1:6 “NASTAAJABU KWA KUWA MNAMWACHA UPESI HIVI YEYE ALIYEWAITA KATIKA NEEMA YA KRISTO, NA KUGEUKIA INJILI YA NAMNA NYINGINE.

7 Wala si nyingine; lakini WAPO WATU WAWATAABISHAO NA KUTAKA KUIGEUZA INJILI YA KRISTO.

8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, NA ALAANIWE.

9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe”

Umeona maana ya kulogwa?..Je na wewe umeiacha Imani na kuigeukia injili ya namna nyingine inayokuambia hakuna kuokoka duniani?..Je umeiacha Imani na kuigeukia injili inayokuambia Mungu haangalii jinsi mtu anavyovaa bali anaangalia moyo wake? Je umeiacha injili inayokuambia pasipo huo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu (Waebr.12:14), na kuigeukia injili inayokuambia bila kuwa mshirika wa dhehebu fulani huwezi kuingia mbinguni?, Je! Umeiacha injili inayokuambia Waasherati, walevi, waabudu sanamu, walawiti, wezi sehemu yao ni katika lile ziwa la moto na kuigeukia injili inayokuambia Mungu hawezi kuwateketeza watu aliowaumba katika ziwa la moto?..

Je umeiacha injili inayokuambia baada ya kifo ni hukumu (Waebr.9:27) na kuigeukia injili inayokuambia kuna nafasi ya pili baada ya kufa na kwamba kunauwezekano wa marehemu kuombewa baada ya kufa ili utoke kwenye mateso ya kuzimu?.

Je! Umeiacha injili inayokuambia mpatanishi katika ya Mungu na wanadamu ni mmoja tu, Yesu Kristo na umegeukia injili nyingine inayokuambia wapo wapatanishi wengine, pembezoni mwa Yesu kama vile bikira Mariamu n.k., au yupo nabii mwingine ambaye ameteuliwa na Mungu kuwa ndiye atakayewapeleka wanadamu mbinguni..

Ndugu mpendwa kama umeacha hayo yote na mengine Zaidi ya hayo yaliyokweli ya Neno la Mungu na umegeukia mambo ambayo hayapo kwenye biblia basi UMELOGWA na Mhubiri huyo!, umelogwa na kanisa hilo!, umelogwa na kikundi hicho cha imani!. Toka upesi, anza kuisoma biblia.

Mahubiri yoyote ambayo baada ya kumaliza kuyasikiliza yanakufanya ujisikie hamu ya kufanya mambo ya kidunia Zaidi ya kulipenda Neno na kulitafuta kulisoma…Muhubiri huyo ni Mchawi, na analoga watu, hata kama hana tunguli nyumbani kwake, anafanya kazi ya kichawi madhabahuni….Mahubiri yoyote yasiyokupa Morali yoyote ya kumfuata Yesu na kuzidi kuyasafisha Maisha yako badala yake unapata morali zaidi ya kumchukia mwingine, kumlaani mwingine, kutafuta kisasi kwa mwingine, kumwacha mke/mume wako, kufanya uasherati, n.k…basi fahamu kuwa umelogwa na hayo mahubiri.

Uchawi mkubwa shetani anaoweza kumfanyia mtu sio kumfunga asipate kazi, au kumfunga asifanikiwe, au kumfunga asipate mtoto..hiyo ni ngazi ndogo sana ya uchawi wa shetani…Uchawi mkubwa anaoufanya ni KUWAFANYA WATU WASIMJUE KRISTO KWA MAARIFA YOTE!, kuwafanya watu wawe vuguvu katika Imani, kuwafanya watu waabudu sanamu na kumkosea Mungu. Huo ndio uchawi shetani kila siku anaoufanya kuuloga ulimwengu.

Na watumishi wake wa ngazi za juu, anaowahitaji na kuwaheshimu sana..si wachawi, wala waganga wa kienyeji…hao wanaloga vitu vidogo vidogo tu…Yeye jeshi lake kubwa linalofanya kazi yake kubwa ni MANABII WA UONGO! Wapinga-Kristo..Wanaoligeuza Neno la Mungu kuwa uongo..Hao ndio watumishi wake wa ngazi za juu kuliko wote. Ndio maana biblia haikusema nyakati za mwisho kutatokea waganga wa kienyeji wengi, au washirikina wa uongo wengi, au wachawi wengi…bali ilisema kutatokea “manabii wa uongo wengi”..Maana yake hao ndio shetani anawatumia kufanya maangamizi makubwa sana ya roho za watu .

Hawa ni watumishi Dhahiri kabisa wa shetani, wanaojigueza kuwa kama manabii wa kweli..Manabii hao wa uongo kazi yao ni kutoa unabii tu siku zote, lakini hawamshuhudii Yesu hata kidogo…Yohana Mbatizaji ambaye alikuwa ni nabii aliyetokea kuwa mkuu kuliko wote “YEYE ALIMSHUHUDIA YESU KWA NGUVU SANA” kwasababu alijua hakuna uzima nje ya Yesu. Na manabii wengine wote walikuwa wanaushuhuda wa Yesu…

Kama biblia inavyosema katika Ufunuo 19:10b “…….KWA MAANA USHUHUDA WA YESU NDIO ROHO YA UNABII”.

Hivyo tunapaswa tujihadhari sana. Hizi ni nyakati za mwisho.

Bwana akubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

KUOTA MTU AMEKUFA/NDUGU AMEKUFA.

JUMATANO YA MAJIVU NI TENDO LA KIMAANDIKO?

Kwanini kila nikitaka kusali naingiwa na uvivu?

6# SWALI : Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?

SAA YA KUHARIBIWA IIJIAYO ULIMWENGU WOTE.

KUOTA UMETUMBUKIA SHIMONI.

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/02/26/ni-nani-aliyewaloga/