KWA HIYO NDUGU, VUMILIENI, HATA KUJA KWAKE BWANA.

by Admin | 7 March 2020 08:46 pm03

Yakobo 5:7 “Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho.

8 Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia”.

Kwanini mtume huyu alifananisha kumngojea Bwana na uvumilivu na wa mkulima anayengojea mazao ya nchi, mpaka atakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho.?

Hii Mvua ya kwanza na mvua ya mwisho ni ipi?

Mvua ya kwanza kwa jina lingine ni mvua ya masika, na mvua ya mwisho ni mvua ya vuli..Israeli tangu zamani hadi sasa ni nchi ya jangwa, sio kama huku kwetu kwenye ukanda wa kitropiki, ardhi ina unyevunyevu wakati wowote, kiasi kwamba hata ukitaka kuchimba kisima popote unakutana maji chini..Jambo hilo huwezi kulikuta katika nchi za jangwa kama vile Israeli..

Hivyo wakulima walikuwa wanategemea sana misimu ya mvua ili kulima na kupanda, wakati mwingine wowote ilikuwa haiwezakani kutokana na kwamba ardhi kuwa kame na ngumu.

Hivyo wakulima ilikuwa inawapasa wangojee wakati wa mvua tu, ndipo wafanye kazi za ukulima, Kwasababu hata mito haikuwepo, na hata kama ipo basi haijitoshelezi yote kwa kilimo cha umwagiliaji..Na hiyo ilikuwa inawafanya wasubirie tu wakati wa mvua, na utakapofika huwa basi wanafanya kazi kama vichaa kwa uvumilivu wote na kwa subira yote kwasababu wanajua upo wakati ambao hawataweza kufanya kazi tena.. Sasa kulingana na Jeografia ya Israeli, mvua ya masika kwao ilikuwa inaanza mwezi wa 10-11, na vuli mwezi 3-4, tofauti na huku kwetu ambapo ni kinyume chake.

Sasa masika ilikuwa ikishaanza tu wakulima wote wanatoka wanaingia mashambani na kuanza kuandaa mashamba na kupanda mbegu zao, na kuzipalilia…Mpaka itakapoisha, Lakini baadaye tena mvua nyingine ndogo ndogo zilikuwa zinaendelea si kali kama zile za Masika ndio hizo za Vuli, ili kustawisha tu mazao, na kuifanya ardhi isipoteze unyevu wake, mpaka misimu yote ya mvua itakapoisha moja kwa moja

Sasa ndio hapa Mtume Yakobo anafanisha kumngojea kwetu Bwana kama mkulima aliye katika msimu wa kilimo chake anavyovumilia mpaka mazao yake yatakapopata mvua zote mbili yaani ya kwanza na ya mwisho… Na akishamaliza basi huvuna na kuyaweka ghalani, jasho lake, na taabu yake sasa inakuwa imekwisha..

HIVYO,MVUA YA KWANZA, NA YA MWISHO ROHONI INAFUNUA NINI?

Vivyo hivyo na sisi tunaomgonjea Bwana, Tulishanyeshewa mvua ya kwanza, siku ile ya Pentekoste takribani miaka 2000 iliyopita, Kazi ikaanza..sasa kuanzia huo wakati tumekuwa tukilima, na kupanda, na kupalilia shamba la Bwana..Lakini pia iliahidiwa mvua nyingine itakayokuja huko mbeleni ambayo itakayokamilisha taabu yetu ya ulimaji..

Ndugu kama hujui ni kuwa tayari tumeshaingia katika kipindi cha msimu wa mwisho wa mvua ambayo ndio ile mvua ya mwisho ya vuli (rohoni), Na mvua hii ilianza mwaka wa 1906, Huu ni wakati ambapo kwa mara nyingine tena Mungu aliijilia dunia kwa vipawa na karama za roho, na kazi zile zile zilikuwa zinatendeka wakati ule wa Pentekoste ya mitume miaka 2000 iliyopita, mambo ambayo hapo katikati yalikuwa hayafanyiki, wala hayaonekani.. Hivyo kuanzia wakati huo ndio, Karama zile zote za rohoni zilianza kurejeshwa katika kanisa tena upya, vilevile Mungu akanyanyua watumishi wake wengi waaminifu kulithibitisha hilo kuwa wakati huo umeanza watu hao ikiwemo (William Seymor, baadaye William marrion Branham, Billy Granham, Oral Roberts, TL Osborn na wengineo wengi)

Tangu huu wakati injili ilianza kuhubiriwa kwa nguvu na ujumbe ulikuwa ni huu…WAKATI WA MAVUNO UMEKARIBIA!! BWANA ANAKARIBIA KULICHUKUA KANISA LAKE..

Wote hawa walikuwa na ujumbe huo, wote walijua tupo katika wakati ule wa MVUA YA MWISHO, wa mvua ya vuli..Na mpaka sasa ndipo mvua hiyo inakaribia kufika ukingoni kabisa… kwenda kugota..Na ikishagota, basi hakutakuwa ni mvua nyingine tena milele..

Ndugu hii neema unayoiona, unapoona unahubiriwa injili kirahisi hivi, Neno la Mungu limezagaa kila mahali, lakini unalipuuzia usidhani ilikuwa hivyo kipindi cha karne ya 19 kushuka huko chini..Hii miujiza unayoina na karama za rohoni unazoziona usidhani zilikuwepo muda wowote wa kanisa… Wewe Mungu amekupa neema ya kuishi katika msimu huu wa mvua ya Vuli rohoni, ambayo ipo karibuni kuisha..Lakini unaichezea hii nafasi..Upo wakati utaitamani lakini mlango wa neema utakuwa umeshafungwa..

Kipindi si kirefu, kanisa litanyakuliwa, wala hakuna mtu atakayesema mimi sikuambiwa wala sikujua, wakati huo Bwana atakusanya mavuno yake na kuyaweka ghalani na magugu kuyatupa motoni..Wote tunafahamu, hali ilivyo sasa, magonjwa ya kutisha yanavyozidi kuzuka, tetesi za vita, matetemeko,manabii wa uongo, watu kupenda fedha, watu kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu, ushoga kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, n.k. yote hayo yaliandikwa na tukaambiwa hizo ndio zitakuwa dalili kuu zitakazotutambulisha kuwa Kristo yupo mlangoni kurudi..

Lakini sisi tuliompokea tumeambiwa, tuyaonapo hayo..Basi ndio tunyanyue vichwa vyetu juu, kwasababu ukombozi wetu umekaribia..

Mvua hii ya neema ipo ukingoni, mkaribishe Bwana moyoni mwako kabla haijakoma kabisa moyoni mwako..Sisi sio wa kuambiwa tena tuvumilie kwasababu sisi tupo tayari wakati wa mavuno, waliokuwa wanapaswa wavulie ni wale wa makanisa mengine lakini sio sisi wa kanisa la mwisho la LAODIKIA.

Shalom.

Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine. Pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email, au Whatsapp au inbox yako ya faceboook, basi utujuze inbox nasi tutafanya hivyo. Vilevile usiache kutembelea website yetu hii (www wingulamashahidi org) kwa mafunzo zaidi.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?

SADAKA YA MALIMBUKO.

KUOTA NYOKA.

USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

Kwanini wakristo wengi ni maskini?.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/03/07/kwa-hiyo-ndugu-vumilieni-hata-kuja-kwake-bwana/