Je kupiga miayo ni ishara ya mapepo?

by Admin | 5 April 2020 08:46 pm04

Shalom, Naomba kufahamu kitendo cha kupiga miayo mara kwa mara hususani wakati wa maombi, Je! Ishara ya kuwa na mapepo au nguvu za giza?.

JIBU: Kwa namna ya kawaida kupiga miayo ni ishara ya mambo mawili makuu katika mwili, 1) Ya kwanza ni njaa, 2) Ya pili ni usingizi.

Hivyo tukirudi katika masuala ya maombi mkristo hapaswi kufikiria kuwa kupiga miayo ni kitendo cha mapepo au nguvu za giza, hapana bali ni mwitikio wa mwili wake mwenyewe, ukimwambia kuwa huu sasa ni wakati wa kwenda kupumzika umechoka, sio wakati wa kusali..Na ndio maana utagundua ni wakati tu wa kusali, au wa kusikiliza Neno watu ndio wanasikia uchovu wa hali ya juu, lakini wakitoka hapo hiyo hali inapotea yenyewe, utajiuliza ni kwa nini?

Ni kwasababu Biblia inatufundisha kuwa mwili ni adui wa mambo ya rohoni sikuzote, wakati roho yako ipo tayari hata kuzama muda mrefu kwenye maombi mwili wako utaanza kutoa sababu nyingi, mara umechoka, unapaswa ukapumzike, utakuletea mpaka hivyo viashiria vya miayo mingi, ili tu kukuthibitishia, na tena kama utakuwa unafikiria chakula muda wa maombi ndio kabisa utakuletea mpaka miayo ya njaa, mpaka utatetemeka wakati ni muda mfupi tu nyuma hapo ulitoka kula.

Wagalatia 5:17 “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka’’.

Hivyo, hali kama hiyo ikikujia, hupaswi kukemea mapepo, bali ni wakati kushindana na mwili wako mpaka ukutii wenyewe, na habari njema ni kuwa kwa jinsi utakavyozidi kuzama katika maombi, ndivyo hiyo hali itakavyokuwa inatoweka yenyewe ndani yako kidogo kidogo, mpaka mwishoni utajikuta unaweza kwenda muda mrefu mpaka utajiuliza ule usingizi mwanzoni ulitokea wapi.

Kwahiyo njia rahisi ni kuhakikisha wakati unaposali, peleka mawazo yako yote na fikra zako zote kwenye maombi na sio katika mambo mengine, ndivyo utakavyoweza kuushinda mwili kirahisi, na kama ni usiku unasali toka katika mazingira ya kitanda.

Mwisho, fahamu kuwa kama mkristo huwezi kuishi bila maombi.

Kwahiyo shindana na mwili wako mpaka uushinde, vinginevyo hutadumu muda mrefu katika imani au kama utaendelea kuwepo basi ujue maisha yako yatakuwa ni ya majaribu kila kukicha ambayo yangeweza kuepukika tu kwa maombi..

Mathayo 26:41 “ Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu”.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.

JE MOYO WAKO NI MNYOFU MBELE ZA MUNGU

JE WAKRISTO TUNARUHUSIWA KUSHEHEREKEA VALENTINE’S DAY?

PASAKA NI NINI? NA JE TUNARUHUSIWA KUSHEHEREKEA PASAKA?

Je! Ni dhambi kwa kijana aliyeokoka kuvaa suruali za kubana (model), kunyoa mitindo (mfano kiduku), ?

Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?

ROHO ZILIZO CHINI YA MADHABAHU:

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/05/je-kupiga-miayo-ni-ishara-ya-mapepo/