Ni kwa namna gani Yesu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka?

by Admin | 8 April 2020 08:46 pm04

SWALI: mstari huu una maana gani? Luka 2:34 “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa”?


JIBU: Kwa faida yetu wote, ni vizuri tukaanzia mistari ya juu ili tupate ufahamu wa habari yote hiyo inamuhusu nani..

Luka 2:25 “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.

26 Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana.

27 Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,

28 yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,

29 Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema;

30 Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,

31 Uliouweka tayari machoni pa watu wote;

32 Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.

33 Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake.

34 Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, TAZAMA, HUYU AMEWEKWA KWA KUANGUKA NA KUINUKA WENGI WALIO KATIKA ISRAELI, NA KUWA ISHARA ITAKAYONENEWA.”

Ukitazama hapo, kuna vipengele vitatu, 1) kuanguka, 2)Kuinuka kwa wengi 3) na kuwa ishara itakayonenewa.

Huyo ni Bwana wetu Yesu Kristo anayezungumziwa hapo na Simeoni akitolewa unabii juu ya mambo atakayokuja kuyatekeleza huko mbeleni kwamba atawekwa kwa ajili ya kutumiza makusudi hayo matatu, yaani kuanguka na kuinuka kwa watu wengi walio katika Israeli na kuwa ishara itakayonenewa.

Tuanze kwa kutazama kwa ufupi kipengele kimoja kimoja..

  1. Kuanguka: Hii ni kazi mojawapo ambayo Kristo alikuja kuitimiza hapa duniani licha ya kuwa alikuwa ni mwokozi wa Ulimwengu aliyekuja kuokoa, lakini pia wale waliompinga na kuyakataa maneno yake, mambo yalikuwa ni tofauti badala ya kubakia kama walivyokuwa baada ya kumpinga kinyume chake ndio walianguka chini kabisa..

na unabii huo ulishatolewa tangu zamani..

Isaya 8:14 “Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu.

15 Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa”.

Jambo hilo tuliliona kwa mafarisayo, waandishi na masadukayo, na Taifa la Israeli kwa ujumla wale wote waliompinga Kristo na kumkataa, walitiwa upofu..

Yohana 9:39 “Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.

40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?”

Neema hiyo ya wokovu iliondolewa kwao, na kuletwa kwetu sisi watu wa mataifa, na kilichobakia kwao hakikuwa kingine Zaidi ya , taifa la Israeli kuja kuangamizwa na Warumi mwaka 70 WK, Ili kutimiza ule unabii Kristo aliozungumza juu yao kuhusu uharibifu wa Yerusalemu na Watoto wao (Soma Luka 19:41-44)

  1. KUINUKA KWA WENGI: Lakini kinyume chake wale waliompokea, walipewa uzima wa milele, Ikiwemo waisraeli wachache na watu wengi wa mataifa, (Ambao ni mimi na wewe). Ukisoma matendo ya Mitume utaona jinsi Mungu alivyokuwa akilizidisha kanisa kwa kasi, na watu wengi walikuwa wanamjua Mungu, na kupata uzima wa milele.
  2. KUWA ISHARA ITAKAYONENEWA: Hilo Neno “itayakayonenewa” maana yake ni itakayozungumziwa kinyume..

Ukisoma tafsiri nyingine hususani zile za kiingereza utaelewa vizuri, mstari huo unasema..” and for a sign which shall be spoken against;”(kjv).. Ishara ambayo haitapokelewa/haitakubaliwa na wengi..

Licha ya kuwa Kristo alijidhihirisha kwao kwa ishara nyingi, na miujiza mingi, akitimiza maandiko mengi yamuhusuyo masihi, lakini wayahudi wengi walimpinga, walitazamia pengine masihi wao angetokea kwenye majumba ya kifalme, lakini walipomuona amezaliwa katika familia ya kimaskini wakajikwaa kabisa.

Hata sasa, Kristo anatimiza, unabii huo, yaliyotokea wakati ule, ndio yanayotokea wakati huu, wakati wengine wanaokolewa, na kunyanyuka, na kupokea uzima wa milele, wapo wengine saa hii wanajikwaa kwa Kristo na kuanguka na kupoteza neema ya wokovu moja kwa moja…Na wanaanguka kwa jinsi gani?.. Ni Pale mtu anapoona Kristo anaokoa na kwamba yeye ndio mwokozi wa ulimwengu halafu hataki kumwamini apokee uzima wa milele, kama ilivyokuwa kwa wale mafarisayo na waandishi, kinyume chake haonyeshi kuthamini jambo hilo, au anadhihaki, basi mtu huyo Kristo anabadilika hawi tena mwokozi kwake bali anakuwa jiwe la kukwaza.. Inamaana kuwa akiendelea hivyo kuna wakati utafika Yule Roho wa Kristo wa neema anayemlilia kila siku atubu, ataondoka ndani yake, kitakachobakia kwake ni kuendelea tu kuupinga wokovu na kudhihaki watu wa Mungu mpaka siku anaondoka duniani.

Watu kama hao wapo kila mahali, utajiuliza hawamwogopi hata Mungu, kulitamka jina la YESU ovyo ovyo tu mitaani, hawaogopi kuufanyia mzaha wokovu na msalaba.

Hivyo na sisi Bwana atusaidie, tuitii injili ili iwe na manufaa kwetu ya rohoni, tusije tukaanguka kwa injili hiyo hiyo. Neno la Mungu ni upanga ukatao kuwili.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Biblia inakataza kuapa kabisa, lakini kwanini watu wanaapa mahakamani na katika vifungo vya ndoa?

Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yeftha ya kumtoa binti yake kafara?

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

Je! Shetani alitolea wapi uovu?

Ikiwa sisi tuliumbwa na Mungu,Je! Mungu aliumbwa na nani?

JE MOYO WAKO NI MNYOFU MBELE ZA MUNGU

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/08/ni-kwa-namna-gani-yesu-amewekwa-kwa-kuanguka-na-kuinuka/