TAHADHARI YA NEEMA YA MUNGU.

by Admin | 13 April 2020 08:46 pm04

Chukua tahadhari juu ya neema ya Mungu.


Hakuna ulinzi mkubwa ambao mwanadamu anaweza kuupata kama ulinzi wa kuwa ndani ya Yesu..Kama wengi wetu tunavyojua au tulivyosikia kwamba watu wote waliompokea Yesu Kristo uhai wao unakuwa umefichwa pamoja na Kristo.(Wakolosai 3:3). Kiasi kwamba tunalindwa dhidi ya nguvu za giza na mipango yote ya Ibilisi.

Wengi wetu tunaifurahia neema hii na kutamani kuingia ndani yake lakini hatujui kuwa ikichukiliwa isivyopaswa ina madhara makubwa kuliko kitu kingine chochote tunachoweza kukijua.

Neema ya Mungu inafananishwa na nyumba ya karamu, yenye mlango…Mathayo 7:13. Sasa kama tujuavyo nyumba yoyote ile ya muhimu kama Ikulu au ukumbi wa sherehe ya muhimu sana ina mlango na vile vile ina uzio…na mara nyingi kuta zake zinakuwa zimezungushiwa uzio mwingine ambao ni wa umeme..Na kama ni nyumba yenye umuhimu mkubwa zaidi ya hayo inakuwa na walinzi wanaotembea tembea wenye silaha kuizunguka, lengo ni kuzuia watu wa wasiruke ukuta na kuingia ndani…Na ikitokea mtu akijaribu kukiuka na kuusogelea ukuta kutaka kuruka aingie ndani ndipo anaweza akajikuta kapigwa risasi au kapigwa shoti ya umeme, na hivyo hata kuweza kujisababishia kifo…Lakini ulinzi huo haujawekwa kwaajili ya kuangamiza watu, bali kulinda usalama.

Na Neema ya Mungu ni hivyo hivyo…Ipo nguvu ya ziada iwalindao wale watu walioingia ndani ya Neema ya Kristo..Nguvu hiyo ndiyo inayotulinda dhidi ya nguvu zote za giza, dhidi ya shetani na majeshi yake (mapepo na wachawi) na kila mpango mwovu wa Ibilisi..Hivyo yoyote anayejaribu kuingia kutaka kuwaharibu watu wa Mungu walio chini ya neema ya Mungu basi atakuwa anajitafutia matatizo yeye mwenyewe..

Lakini jambo lingine la kuogopesha ni kwamba ikitokea mtu aliyeko ndani ambaye tayari kashaingia ndani ya jengo hilo, akatoka na kwenda kupanda ukuta na kurukia zile nyaya za umeme zilizouzunguka ukuta, yeye naye atajeruhiwa vile vile kama sio kufa kabisa. Maumivu yale yale atakayoyasikia Yule anayetaka kuruka ukuta na kuingia ndani ndio hayo hayo atayapata Yule anayetaka kuruka na kutoka nje.

Madhara atakayoyapata mchawi anayetaka kuwadhuru watu wa Mungu, ndio hayo hayo atakayoyapata mkristo anayeuacha wokovu na kuurudia ulimwengu. Mkristo ambaye ameshaonja kipawa cha Mungu na kuburudika na neema ya Mungu, na ghafla anarudia uasherati wake, anarudia wizi wake, anarudia matusi yake, anarudia mauaji yake, usagaji wake, utoaji mimba wake, mambo ambayo alikuwa ameshayaacha machafu anayarudia tena…akidhani kwamba mkono wa Mungu ni kinyume cha wale waliopo nje pasipo kujua hata waliopo ndani ambao wanataka kutoka vile vile mkono wa Mungu upo kinyume chao.

Wengi wetu hatupendi kusikia mambo kama haya kwasababu hatupendi kuumizwa mioyo, hatupendi kusikia habari mbaya, lakini fahamu kuwa tahadhari siku zote sio habari njema, lakini zina umuhimu sana katika maisha hususani katika siku za baadaye…hata vidonge tupewacho na wataalamu wa afya ambavyo vinatumika kwa tiba, bado vina tahadhari zake…lengo la tahadhari zile sio kuwatisha watumiaji wala kuwakatisha tamaa bali kuwanufaisha zaidi.

Vivyo hivyo Neema ya Kristo inayo tahadhari…Na ni lazima kila mtu aijue tahadhari hiyo, wahubiri wengi hawaifundishi kwasababu watakosa waumini, na wao bado wanatafuta waumini…Lakini sikia leo hii mtu wa Mungu tahadhari, ili baadaye tusije kujuta, na tahadhari hii haikuhusu wewe unayesoma tu, hapana hata mimi ninayeandika inanihusu. Biblia inasema..

Waebrania 10:26 “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;

27 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.

28 Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”

Kama umeamua kumfuata Yesu basi umfuate kweli kweli..usiusogelee kabisa ukuta wa Neema..uwe ndani au nje ni upanga ukatao kuwili..Neno la Mungu linasema usizini…hizo ni kuta!..neno linasema usiibe, usiue hizo ni kuta..ukipanda na kuzivuka nguvu ya Mungu utakumaliza..ambayo hiyo Mungu hakuiweka kwaajili ya kuua watu, bali kwaajili ya kuwalinda watu wake.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JE KUPONYWA NI UTHIBITISHO WA MUNGU KUWA NA WEWE?

USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

Je kupiga miayo ni ishara ya mapepo?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/13/tahadhari-ya-neema-ya-mungu/