NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

by Admin | 30 April 2020 08:46 pm04

Shalom, karibu tujifunze maandiko katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo.

Leo tutajifunza jambo lingine ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujua ni kwa nini tunapaswa tuihubiri injili wakati wote bila kujali ni nani tunayempelekea ujumbe huo.

Ukisoma Habari za wafalme katika biblia, utakutana na mfalme mmoja ambaye alimuudhi Mungu kwa viwango vya juu sana, naye si mwingine Zaidi ya mfalme Ahabu ambaye pia alichochewa na mke wake Yezebeli,

1Wafalme 11:25 “Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea”.

Wote hawa wawili waliigeuza Israeli kuwa nchi ya waabudu sanamu, wakawafukuza na manabii wote wa Mungu, na kama hiyo haikutosha walikuwa wanamwaga damu nyingi za watu wasiokuwa na hatia..

Hivyo Mungu akakusudia kumuua Ahabu, kwa kumtolea kabisa unabii, kwa kinywa cha Nabii Eliya kuwa atakufa kifo cha aibu na damu yake italambwa na mbwa (1Wafalme 21:17-19)..Lakini miaka ilikwenda, miaka ikarudi, hakuna aliyejua mfalme huyu mwovu ni nani atamuua, wala atakufaje.

Lakini siku ya siku, akakusudia kwenda vitani, kupigana na maadui zake washamu, lakini safari hii hakwenda peke yake, bali alimtafuta Rafiki yake Yehoshafati ambaye yeye alikuwa ni mfalme wa Yuda wakati huo, isipokuwa Yehoshafati alikuwa anamcha Mungu kuliko yeye.. Hivyo akapanga njama, akamwambia Yehoshafati, kwamba yeye ndio ajifanye kuwa mfalme wa Israeli, avae nguo za kifalme, Na yeye atavaa nguo za kawaida, atajichanganya mule mule vitani..kwasababu alijua washami walikuwa hawana shida na watu, bali walikuwa na shida na mfalme wao..Maana ndivyo walivyopatana kuwa watakapokwenda vitani, wasihangaike na mtu yeyote bali wapeleke nguvu zao kwa mfalme wa Israeli tu, kwasababu walijua wakishamuua tu mfalme wao basi vita vitakuwa vimekwisha..

Lakini Ahabu yeye alikwenda kinyume chao, akamfanya mwenzake Yehoshafati awe shabaha ya maadui zao..Hivyo wakaingia wote vitani mapambano yakaanza, Na Yehoshafati alipoona maadui zao, wote wanamkimbilia kumfuata yeye, saa hiyo hiyo akamlilia Mungu amwepushe na ile mauti, Na Mungu akamsikia Hivyo wale washami walipoona kuwa yule wanayemfukuzia siye mfalme halisi wa Israeli waliachana naye, wakaendelea na mapambano..

Lakini sasa, wakiwa katika mapambano, hawajua mfalme ni yupi katikati ya umati, biblia inatuambia mtu mmoja akavuta upinde wake kwa kubahatisha tu, pengine yeye alikuwa na lengo la kumpinga, mwanajeshi mmoja wa kawaida tu aliyemwona mbali, akitimiza kusudi lake la kutupa silaha yake, kwa adui yake aliyemwona mbele yake..Lakini hakujua kuwe kumbe yule ndio Kichwa cha Adui wao, tusome…

1Wafalme 22:33 “Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.

34 Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.

35 Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari.

36 Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake.

37 Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria”

Unaona?..Ule upinde ulikwenda kupenya kwenye ile sehemu dhaifu kabisa ya mavazi yake ya chuma, yaani pale ambapo yanakutana, pale kwenye mkunjo hapo hapo ndipo mshale ukaingia..Na baadaye akafa kwa kuchurukiza damu, na mwisho wake ukawa umefikia hapo..

Sasa ni vizuri kufahamu kuwa habari zote tunazozisoma katika agano la kale, sio kutuburudisha sisi, hapana bali kila tukio lina ujumbe wa siri wa kanisa la Kristo katika agano jipya..

Hivyo katika Habari hiyo Bwana anatuonyesha, mojawapo ya njia ya kumshinda adui yetu ibilisi kiurahisi.. Tunajua ibilisi huwa anatumia mbinu nyingi katika kushindana na kanisa la Kristo, Na wakati mwingine haji kwa njia ya moja kwa moja ili kushindana na sisi, kwani anajua akija hivyo ni rahisi kumgundua na kumshinda..

Hivyo anatumika njia ya kujigeuza kama alivyofanya Ahabu..

Kwahiyo inahitajika njia nyingine ya kupambana naye, vinginevyo tutamkosa, nayo si nyingine Zaidi ya kurusha mishale mingi kwa kadiri tuwezavyo,.. Yaani maana yake tuihubiri injili kama watu wasio na malengo kwa sababu kwa njia hiyo Hujui Mungu atammalizia shetani katika engo ipi..

Unaweza ukakutana na mtu lakini hujui kuwa huyo ni ajenti mkubwa wa shetani, ambapo pengine angesikia injili yako kidogo tu, angegeuka, kutokwenda kusababisha maajali barabarani siku hiyo..

Au tunakutana na mtu ambaye anaonekana ni wa kidunia tu, tunaishia kusema huyu ni jambazi, au mlevi, au mshirikina na hawezi kubadilika, lakini hutujui shetani ndiye aliyempelekea mapepo mengi ya ushawishi ili aendeleee kuwa vile, kwasababu alishaona tangu zamani katika ulimwengu wa roho kuwa ikitokea akiiamini injili basi siku moja atakuwa mhubiri wa kimataifa wa kuwaleta wengi kwa Kristo, hivyo kaamua kumfanya vile awe muuaji, au mpingamizi mkubwa wa injili kama alivyofanya kwa mtume Paulo..Lakini kwasababu tunaogopa kurusha mishale, tukikisia kuwa haina faida yoyote hatujui kuwa ndivyo tunavyomkosa ibilisi hivyo vitani.

Kuna mhubiri mmoja wa kimataifa anaitwa Rick Jonyer, yeye alichukuliwa katika maono mbinguni akaonyeshwa, baadhi watu walio katika viti vya enzi, na alipotazama vizuri alimwona mtu mmoja aliyemjua,.akamuuliza Bwana Je! Imekuwaje mtu huyu mtu amefika hapa, Bwana akamfunulia historia ya Maisha yake, na jinsi yeye alivyokutana naye wakati fulani akamdharau, wala hakumhubiria kwasababu ya udhaifu wake wa kusikia..Lakini Yule mtu alipokuja kutubu dhambi zake, na kumtumikia Mungu kwa uaminifu wote katika madhaifu yake, ndio ikampelekea awe mtu mkubwa sana kule mbinguni.. Na mwisho kabisa Bwana akamwambia, kama usingekuwa na tabia hiyo ya kudharau watu, leo hii ungetambuliwa na mbingu kuwa wewe ndiwe mwalimu wa mfalme mkuu kama huyu.

Hivyo na sisi, tuhubiri kwa watu wote, bila kutazama ni nani aliye mbele yetu..Kwasababu hatujui kuwa ushindi mkubwa dhidi ya shetani tutaupata kupitia njia hiyo..

Mhubiri 11: 6 “Asubuhi panda mbegu zako, Wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa,kama ni hii au hii, au kama zote zitafaa sawasawa”.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

IKIMBIE DHAMBI KWA GHARAMA ZOZOTE ZILE!

MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.

Shetani ni nani?

KWANINI UBATIZO NI WA MUHIMU.

Kwanini Mungu alisema hakuna mtu awazaye kuuona uso wake akaishi?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 3

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/30/na-mtu-mmoja-akavuta-upinde-kwa-kubahatisha-akampiga-mfalme/