KILA KIUNGO LAZIMA KISHUGHULIKE.

by Admin | 26 May 2020 08:46 pm05

Kanisa la Kristo limefananishwa na mwili wa binadamu. Kama vile mwili ulivyo na viungo mbalimbali, mfano mikono, miguu, macho, masikio, mdomo n.k. vikiongozwa na kitu kimoja cha muhimu kiitwacho kichwa. Vivyo hivyo na kanisa la Kristo. Biblia inasema sisi tu viungo mbalimbali na kichwa chetu ni Kristo.

Sasa kama vile katika mwili tunajua hakuna kiungo hata kimoja kisichokuwa na shughuli yoyote vivyo hivyo sisi kama viungo hakuna hata mmoja anayesema ameokoka akawa hana shughuli yoyote ya  kufanya katika mwili wa Kristo. Tena sifa nyingine ya viungo ni  kwamba vyote huwa vina vinashirikiana kwa umoja usiokuwa wa kawaida.

Waefeso 4:16 “Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo”.

Umeona huwezi kusema umeokoka, miezi inapita, miaka inapita, hakionekani chochote unachokichangia katika mwili wa Kristo,..Ukiona hivyo basi ujue ulishakufa kutoka katika mwili wa Kristo, na hivyo ulishakatwa na kutupwa nje siku nyingi. Hutambuliki, ukijiona ni wa kuhubiriwa tu daima, lakini wewe hakionekani chochote unachomfanyia Kristo,ni lazima ujitathimini tena mara mbili wokovu wako.

Tabia ya viungo vilivyo hai vya Kristo ni hizi.

1.Kwanza kiungo kinakuwa kinalihudumia kanisa la Kristo kwa mali zake: Ni jukumu la kila mkristo kumtolea Mungu ili kazi ya injili izidi kuenda mbele, na hii sio tu kwamba inawahusu wanaopelekewa injili tu, bali pia kwa Yule anayeipeleka injili, yeye pia anao wajibu wa kumtolea Mungu, sehemu ya alivyo navyo kwa kadiri alivyokirimiwa neema.. Kwasababu jukumu hilo ni la kila kiungo.

2. Pili ni wajibu wa kila kiungo kuliombea kanisa: Maombi ni sehemu ya maisha ya mkristo yoyote, ni lazima aliombe kanisa lote la Mungu kwa ujumla duniani kote, Si rahisi kukutana viungo vyote kwa wakati mmoja, lakini maombi yanawakutanisha katika roho..Hata viungo katika mwili si vyote vinavyokutana, lakini vinajuana, na kusaidiana kwa kuchukuliana udhaifu, vivyo hivyo na sisi, kuliombea kanisa la Kristo ni wajibu wetu kila siku kama wakristo. Macho hayawezi kujiosha yenyewe ni lazima mikono iisaidie, na kadhalika hata mkono mmoja unauhitaji mkono mwingine..

3. Tatu; Kiungo ni lazima kifanye kazi ya kupeleka habari njema kwa wengine: Jukumu ambalo tulipewa wote na Bwana wetu ambaye ni Kichwa, ni kwamba tuenende ulimwenguni mwote, tukawafanye mataifa kuwa wanafunzi (Mathayo 28:19).. Hivyo kila mmoja wetu kwa jinsi alivyopewa karama, anayowajibu wa kuifanya kazi ya kuwahubiria wengine kwa jinsi awezavyo. Ikiwa ni muhubiri, unawajibu wa kuhubiri kwa bidii, ikiwa ni mwinjilisti, mwalimu, mtume, nabii, mwimbaji, mwandishi, n.k. Unafanya vyote kwa bidii, na katika Roho na kweli..Na hiyo inathibitisha kuwa wewe ni kiungo kilicho hai.

Hizo ni ndizo dalili zinazothibitisha uhai wa viungo vya Kristo.  Lakini ni kwanini watu wengi wanaosema ni wakristo wamekosa vigezo hivyo  vitatu kwa pamoja?

Ni kwasababu hawataki kukaa ndani ya Kristo kumtii yeye, ambaye ndiye anayewajalia watu uhai huo. Ndugu usipokitii kichwa, kamwe huwezi kufanya lolote mwilini. Bwana Yesu mwenyewe alisema.

Yohana 15:4 “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.

15 Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.

6 Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea”.

Umeona,..Ukiwa hutakubali kumaanisha kuyasalimisha maisha yako moja kwa moja kwa Kristo, yaani kukataa maisha ya mguu mmoja ndani mwingine nje, kamwe hutaweza kuwa kiungo hai, hata iweje. Wewe utakuwa ni sawa na tawi lililokatwa linangojea tu kutupwa motoni. Na pia kumbuka huwezi kuwa na karama zote, hata viungo vya mwili vinatufundisha, lakini utakuwa na karama yako ya kipekee ambayo itakuwa ya muhimu katika kanisa la Kristo.

Huu ni wakati wa wewe, kufanyika kiungo hai Kristo..Ikiwa upo tayari kufanya hivyo, basi tubu makosa yako, mrudie Kristo, nenda kabatizwe kama ulikuwa hujabatizwa ipasavyo hapo kabla, kwa ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji tele sawasawa na (Yohana 3:23 na Matendo 2;38). Kisha kuanzia huo wakati anza kuishi maisha yanayouhakisi wokovu.

Na kuanzia huo wakati  wewe mwenyewe utaona tu, Kristo anavyoanza kukutumia kwa ile karama atakayoishusha ndani yako..Na wewe pia utakuwa kiungo chenye kazi yake maalimu ndani ya mwili wa Kristo. Siku ile ya mwisho kikisubiriwa kupewa heshima yake ya kipekee.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

KIFO CHA MTAKATIFU POLIKAPI (Policarp).

JE KUHUDUMU KWA NYIMBO ZA INJILI KUKOJE?

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

Maana ya ‘Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake’

NIMEOKOKA, ILA MUNGU NDIYE ANAYEJUA NITAKWENDA WAPI.

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/05/26/kila-kiungo-lazima-kishughulike/