WALA SIJIHUKUMU HATA NAFSI YANGU.

by Admin | 5 July 2020 08:46 pm07

Kuna hatua unafika Mungu anahitaji umuangilie sana yeye kuliko kujiangalia nafsi yako ili uweze kusonga mbele katika kumtumikia. Lipo tatizo kubwa ambalo lilishawahi kunikumba mimi, siku za mwanzoni nilipookoka, na naamini linawakumbuka watu wengi hata sasa waliookoka, Jambo hilo mtume Paulo alishaliona na kulitolea ufumbuzi wake kwa ufunuo wa Roho..

Kuna wakati unafika, unaona kila jambo unaloweza kujaribu kulifanya unaona pengine linaweza likawa linamkosea Mungu, au kama umefanya dhambi fulani ukatubu, unaona kama vile Mungu hajakusamehe vizuri, au amekukakasirikia, na hiyo inakufanya ujilaumu muda mwingi, Unajihukumu na kuhitimisha kuwa Mungu hawezi kuwa na mimi tena, Mungu hawezi kunitumia, Mungu ananiona mimi ni mchafu sana, Nimeuhuzunisha moyo wake sana hivyo ameshakata tamaa na mimi..

Paulo alisema hivi..

1 Wakorintho 4:1 “ Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu.

2 Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.

3 LAKINI, KWANGU MIMI, SI KITU KABISA NIHUKUMIWE NA NINYI, WALA KWA HUKUMU YA KIBINADAMU, WALA SIJIHUKUMU HATA NAFSI YANGU.

4 MAANA SIJUI SABABU YA KUJISHITAKI NAFSI YANGU, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana.

5 Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu”.

Kama tunavyojua Paulo ni mtu ambaye mawazo yake yote yalielekea kwa Mungu sana, alikuwa anajitahidi kwa kadiri awezavyo kumpendeza Mungu lakini pengine katika Nyanja fulani za Maisha yake ya huduma alishawahi kufanya makosa kadha wa kadha, au alishawahi kushindwa kufanikisha hiki au kile kwa ajili ya Mungu, kiasi kwamba hata yeye mwenyewe au watu wengine wangemwona kama ameshindwa kabisa, lakini hapa anasema..

“Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu.

4 Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu”

Unaona madhaifu yake hayakuwa sababu ya yeye kujihukumu kuwa anafaa au hafai mbele za Mungu, japokuwa hilo halimthibitishii kuwa anafaa, lakini hakuruhusu ajihukumu kwasababu haoni sababu kwanini afanya vile, Pengine aliwaza Mungu hakuwahi kumwambia kuwa hampendi, Au Mungu hakuwahi kumuonyesha katika maono kuwa hamtaki tena? Kama sivyo, ni kwanini ajihukumu mwenyewe?

Hivyo Paulo aliamua kuendelea kuishi Maisha ya kumtegemea Kristo kuliko kuutegemea ukamilifu wake wote umsaidie katika huduma yake, na hiyo ilimfanya afike mbali, japokuwa alikutana na milima na mabonde,

Lakini kumbuka jambo kama hili halimuhusu mtu anayefanya dhambi za makusudi. Wewe kama mzinzi, Maisha yako yapo mbali na wokovu unafanya dhambi kwa makusudi, ndani yako hakuna hofu yoyote ya Mungu, ujue kuwa hata kama hutajihukumu, basi dhamira yako itakushuhudia ndani yako kuwa kuwa wewe ni mnafki na mwovu. Na utahukumiwa siku za mwisho…Na kumbuka mojawapo ya dhambi za makusudi kabisa, zisizo za madhaifu, ni dhambi ya uzinzi na uasherati. Mtu anayefanya uasherati baada ya kuokoka anafanya dhambi ya makusudi inayostahili hukumu. Hivyo kama unaifanya ndugu iache mara moja.

Lakini ikiwa upo ndani ya Kristo, na una kiu kweli ya kuzidi kumpendeza Mungu na unajitahidi kujizuia kwa kila kitu kiovu, basi kataa hukumu yoyote inayokuja ndani ya moyo wako inayokuambia wewe hufai, kataa mawazo yote yanayokuambia unachofanya kwa Mungu hakimpendezi hata kidogo, kataa hayo mawazo yanayokuambia Mungu hana mpango wa wewe, yakija yaulize mbona Mungu hajawahi kuniambia hilo jambo?. Endelea kumtumikia Mungu kwa karama aliyoiweka ndani yako..

Ikiwa ulifanya makosa Fulani madogo, basi rekekebisha makosa yako, kisha endelea kusonga mbele, mtazame Kristo, na yeye atakuwa na wewe siku baada ya siku, Vilevile usikubali hukumu kutoka kwa mtu yeyote ikutaabishe moyo,..yupo mtu anaweza kukuambia wewe bado hujaitwa na Mungu kwa kutazama maisha uliyokuwa unaishi huko nyuma?…na akakwambia Mungu hawezi kukutumia mtu kama wewe, muulize mbona Mungu hajawahi kunisemesha mambo kama hayo? Wengine wanaweza kukutamkia maneno ya laana hata kama yataonekana yana ukweli ndani yake lakini wewe yakatae matazame Kristo, endelea na safari…

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

JE KUNA UISLAMU KATIKA BIBLIA?

Ni uthibitisho upi unaoonyesha kuwa kuna MBINGUNI na KUZIMU?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/05/wala-sijihukumu-hata-nafsi-yangu/