JE BWANA WETU YESU ALIKUWA NI MZUNGU?

by Admin | 10 July 2020 08:46 pm07

Shalom, karibu tujifunze Biblia…

Nimewahi kukutana na watu kadha wa kadha ambao ukijaribu kuwaeleza tu habari za msalaba na wokovu ulioletwa na mwokozi wetu Yesu Kristo, wanasema Bwana Yesu alikuwa ni mzungu, hivyo hawawezi kumfuata mzungu, wala dini iliyoletwa na wazungu…Huko ni kutawaliwa na wazungu na wanahitimisha kwa kusema kwanini sisi waafrika tusidumishe Imani zetu, kwanini mpaka tuige vitu tulivyoletewa na wazungu? Kwanini tusifuate vya kwetu, huo ni ukoloni mamboleo?..kwanini hatujikubali?.

Hii ni hoja kubwa sana ambayo inawasumbua watu wengi….. na inatokana na kutojiamini na uchungu moyoni…Sasa kabla ya kwenda kwenye swali letu la msingi hapo juu linalouliza “Je Bwana Yesu alikuwa ni mzungu au la!” hebu tutafakari kwanza vipengele vifuatavyo.

Mtu unayehoji kwamba “hatupaswi kufuata kitu chochote cha mzungu” bali tudumishe vya kwetu…basi anapaswa akatae vyote vilivyoletwa na watu hao pia wa magharibi bila kuacha hata kimoja…ikiwemo simu anayoitumia, asiitumie tena, nguo anazovaa asizivae tena (kwasababu hata nguo anazovaa zimetengenezwa na viwanda vya hao hao anaowaita wazungu)..hivyo anapaswa aendelee kuvaa mavazi yake ya asili waliokuwa wanavaa waafrika wa zamani kama ni Kamba au makuti au nyuzinyuzi.

Hali kadhalika hapaswi kuishi kwenye nyumba za kisasa zenye umeme, kwasababu hata huo mfumo wa ujenzi ni kutoka kwa hao hao anaowaita wazungu na umeme pia, hapaswi kutumia dawa ya meno, pasi, hatakiwi kutumia hata trekta kulimia, hapaswi pia kuangalia wala kutumia TV, hapaswi pia kutumia jiko la gesi, wala sufuria,wala hapaswi kumiliki gari wala chombo chochote cha usafiri wa moto kwasababu vyote vimeletwa na hao hao anaowaita wazungu, akitaka kusafiri kutoka mji mmoja kwenda mwingine hana budi kutumia punda…na pia hapaswi kwenda hospitali yoyote wala kutumia aina yoyote ya matibabu ya kisasa na mwisho hapaswi kupeleka Watoto wake shule….Kama hivyo vyote atakuwa amefanikiwa kuacha kuvitumia basi atakuwa sio mnafiki kuikataa pia na Imani iliyoletwa na wazungu…lakini kama hawezi kuacha hivyo vyote na anavipenda basi atakuwa ni MNAFIKI kuchukia Imani ambayo imeletwa na hao anaowaita Wazungu, kwa kisingizio kwamba imeletwa na watu weupe!.

Sasa baada ya kutafakari hayo twende mbele Zaidi….

Ni ukweli usiopingika kwamba Imani ya Kikristo iliingia barani Afrika kupitia Wamisionari waliotoka nchi za Ulaya…Hao wamisionari hawakuwa waafrika bali walikuwa watu weupe (wazungu)….kwa njia yeyote ile waliyokuja nayo huku, lakini mwisho tunajua kuwa ilikuwa ni mpango wa Mungu wao kufika huku kuleta Habari za Mwokozi.

Sasa swali la msingi la kujiuliza ni kwamba hawa Wazungu/wamisionari je waliitolea wapi Imani ya Kikristo?…Kama unasoma biblia utakuwa unalo jibu tayari kwamba Imani ya kikristo chanzo chake ni Taifa la Israeli. Taifa la Israeli ndio taifa pekee ambalo Mungu alilichagua liwe mwanzo wa kupitisha kusudi lake hapa duniani… Hivyo hilo pekee ndio lilikuwa taifa teule la Mungu…na mataifa mengine yaliyosalia duniani yaliitwa “MATAIFA”….sasa hili neno “mataifa” ni neno la ki-ujumla ambalo lilikuwa linawakilisha makundi ya nchi zote ulimwenguni mbali na Israeli ambazo hazikuwa zinamwabudu Mungu mmoja wa mbingu na nchi (Yehova)…Ni Taifa moja tu pekee ambalo ndilo lililokuwa linamwabudu Mungu wa mbingu na nchi kulingana na jinsi yeye anataka!…na hilo si lingine Zaidi ya Taifa la Israeli.

Na waisraeli hawakuwa wazungu!…walikuwa ni watu wanaokaribia kufanana sana na “waarabu”.. Hivyo kama wewe unajua vyema jamii za watu unaweza kujua tofauti ya mzungu na mwarabu kimwonekano, hawafanani, na hata waarabu si weupe kama wazungu! Na hawana macho ya blue kama wazungu!, na nywele zao ni nyuesi na si za gold kama za wazungu!….

Sasa mwokozi wetu Yesu Kristo ndiko alikozaliwa (yaani huko Israeli) hivyo kwa mwonekano alikuwa anafanana na hawa wa Israeli…Na waisraeli hawakuwa watu hodari wa kimaendeleo wakati wa mwokozi kuishi ulimwenguni..ndio maana utaona wakati Kristo akiwa duniani, Warumi(ambao sasa ndio walikuwa wazungu) walikuwa waitawala Israeli. Na Mungu aliwafanya Israeli kuwa wadogo mpaka kufikia hatua ya kutawaliwa, kutoka na makosa yao waliomuasi. Hivyo hawakuwa na maendeleo yoyote ya kushangaza ukilinganisha na mataifa mengine ya kizungu kama Rumi na Ugiriki(Uyunani).

Sasa tukirudi kwenye swali letu.. “je Bwana Yesu alikuwa ni mzungu?”..Jibu utakuwa umelipata kulingana na maelezo hayo hapo juu….hakuwa mzungu bali mtu wa Taifa la Israeli..Waliokuwa wazungu ni wakina Pilato, Herode ambao ndio walikuwa Warumi.

Kwahiyo kimwonekano Kristo hakuonekana kama Mzungu bali kama Mwisraeli…..

Sasa hawa wazungu ilitokeaje wakamwamini Bwana Yesu ambaye hakuwa mzungu?…Habari hizo unaweza kuzipata katika historia, lakini kwaufupi ni kwamba nao pia walipelekewa habari za Yesu kama sisi tu tulivyoletewa . Wale waliozipokea ipasavyo walijua kabisa kwamba na wao ni watu wa Mataifa ambao hawakustahili kuitwa watu wa Mungu lakini kwa kupitia mkombozi mmoja Yesu Kristo waliingizwa katika neema hiyo..ambayo iliwastahili Waisraeli tu peke yao!.

Hivyo wao nao wakatuletea sisi Injili, kwasababu huku Afrika kulikuwa ni giza nene, watu walikuwa wanaabudu miungu na imani potofu….na katika zama hizi za siku za mwisho, mambo yamebadilika ni wakati wa Afrika sasa nao kuipeleka Injili kwa wazungu kwasababu huko kwao sasa kumeoza, kile kizazi kilichomtumaini Mungu kimeshaondoka kimezuka kizazi cha watu wasiomwogopa Mungu huko kwao ndio kitovu cha watu mashoga, watu wanaokufuru, watu wanaotembea uchi mabarabarani n.k. Hivyo injili inahitajika sana sasa kwa wazungu Zaidi ya kwa waafrika, kama wao walivyotuletea ni wakati sasa wa sisi kuwapelekea wao watubu, wamwamini mwokozi.

Kwahiyo ndugu, kamwe usikae uliingize suala la wokovu wa mwokozi wetu Yesu Kristo na “Rangi” Mungu wa Israeli hana ubaguzi wa rangi na anaabudiwa na watu wa rangi zote…ili awe Mungu wa mbingu na nchi ni lazima apatikane kwa watu wote…Ukiona unamwabudu Mungu anayepatikana Afrika tu, au anayepatikana Ulaya tu!…basi huo ni uthibitisho tosha kwamba huyo sio Mungu wa kweli wa mbingu na nchi..Kwasababu Mungu wa kweli wa dunia yote ni lazima aabudiwe na kutangazwa ulimwenguni kote na watu wa rangi zote!.

Na usisahau jambo hili mwokozi Yesu Kristo, alikufa, akafufuka na akapaa mbinguni na atarudi tena mara ya pili, hivyo kama umeisikia injili na bado hujamwamini, au ulikuwa unafikiri labda ukimwamini utakuwa umetimiza matakwa ya watu weupe, au ni ukoloni!..basi hilo wazo lifute kuanzia leo… hukumu inakuja, hivyo tubu leo kama hujatubu,vilevile ukabatizwe ili dhambi zako ziondolewe na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusadia kushinda dhambi na kukusaidia kuelewa mambo ambayo ulikuwa huyaelewi kuhusu yeye.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

JE! PAKA KULIA USIKU NI ISHARA YA UCHAWI?

Je! Ni kweli kuna samaki mtu (Nguva) Baharini.

Tofuati kati ya Myahudi, Mwisraeli na Muebrania ni ipi?

KWA VILE ALIVYOKUWA MTU WA HAKI.

KRISIMASI (CHRISTMAS) NI NINI? JE IPO KATIKA BIBLIA?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/10/je-bwana-wetu-yesu-alikuwa-ni-mzungu/