THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.

by Admin | 15 July 2020 08:46 pm07

Tutakapofikia kule ng’ambo zipo thawabu za aina mbili Mungu alizotuandalia, zipo thawabu ambazo zitajulikana na kila mmoja wetu, na zipo thawabu ambazo hatutazijua kila mtu isipokuwa hao watakaozipokea.

Kwa mfano hata ukienda leo kwenye harusi, utagundua wale wanandoa huwa wanapokea aina mbili za zawadi, zipo zile ambazo zinatangazwa hadharani au zinaonekana pale, kwamfano mtu ataleta kabati, mwingine vyombo, au mwingine ataahidi shamba n.k. vitajulikana pale na waalikwa wote. Lakini pia zipo ambazo zinakuja katika maboksi au bahasha, au mifuko maalum, ambazo huwa hazijulikani na kila mtu aliyepo pale, isipokuwa tu kwa bibi-arusi na Bwana arusi siku watakapokuja kuzifungua.

Ndio hapo pengine utakuta ameandikiwa labda hundi ya fedha nyingine kwenye bahasha, mwingine ndani kaweka simu, mwingine saa, mwingine hata ufunguo wa gari n.k…

Sasa zawadi za namna hiyo huwa hazijulikani na wale waalikwa hata kidogo, sasa yule mtu mfano akienda kuchukua lile gari alilopewa kwa siri, akawa analitumia, itakuwa ni rahisi sana wale watu kudhani kuwa lile gari ni la kwake, alilihangaikia na kulinunua kwa gharama zake, kumbe anayejua siri hiyo ni yeye mwenyewe, na yule aliyemletea zawadi.

Na itakuwa hivyo hivyo kwetu sisi tukifika mbinguni siku ile, Mungu atatupa thawabu nyingi zitakazojulikana na kila mtu, kulingana na uaminifu wako hapa duniani, lakini pia ameahidi kutoa thawabu ambazo hizo zitamuhusu muhusika mwenyewe atakayezipokea na si mtu mwingine.

Na thawabu yenyewe kasema itakuwa ni JINA JIPYA .. Embu tusome kidogo.

Ufunuo 2:15 “Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.

16 Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.

17 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na JUU YA JIWE HILO LIMEANDIKWA JINA JIPYA ASILOLIJUA MTU ILA YEYE ANAYELIPOKEA”.

Soma tena mtari wa 17, unasema.. .nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea”.

Sasa jina hilo jipya hapewi kila mtu, bali ni yule tu atayeshinda vitav ya dunia hii..Na ndio maana utaona hata, Bwana wetu naye aliposhinda, naye pia alipewa na Mungu jina hilo jipya ambalo halijui mtu isipokuwa yeye mwenyewe,.soma hapa.

Ufunuo 19:11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.”

Sasa, jiulize ni kwanini atoe jina na si kitu kingine chochote.?

Ndugu jina ndio kila kitu, kwasababu jina linabeba hatma yote ya Maisha ya mtu, linaelezea heshima yake, linaeleza utajiri wa mtu,na linabeba uweza na nguvu na mafanikio yote ya mtu.

Kwamfano utaona Ibrahimu alipobadilishwa jina kutoka Abramu, na kuitwa Ibrahimu, ndipo hapo Mungu alimfungulia uzao, tena uzao mwingi kama nyota za mbinguni, kiasi kwamba hata mimi na wewe tuliookoka tumefanyika kuwa Watoto wa Ibrahimu kupitia Yesu Kristo, na Sara naye vivyo hivyo.

Mwangalie tena ni Yakobo utaona jinsi alivyobadilishwa jina na kuwa Israeli, ndipo jambo lingine rohoni likatokea, siri ambayo wengi wetu hatuijui ni kuwa, lile jina la Israeli lilikuwa na nguvu ya kuushikilia uzao wa Yakobo, kuanzia ule wakati na kuendelea bila kugawanyika, tofauti na ilivyokuwa kwa uzao wa Isaka, Utaona Isaka alizaa mapacha, ndugu kabisa wa damu, yaani Esau na Yakobo, lakini Mungu ilimpasa achague mmoja tu, Lakini Yakobo alizaa Watoto wengi, tena kwa wamama tofauti tofauti ambao undugu wao upo mbali mbali kidogo, kuliko ilivyokuwa hata kwa ndugu yake Esau, lakini kwasababu aliitwa Israeli, Watoto wake wote hadi leo, nao pia wanaitwa Israeli.

Halikadhalika, kwa Petro, na Paulo, majina yao yalipobadilishwa ndipo walifanya maajabu makubwa na kuwa Mahodari wa Imani.

Vivyo hivyo na wale watakaoshinda vita vya dunia hii kikamilifu, Mungu amewaahidia kuwapa majina mapya, ambayo hayo hayatajulikana na watu wengine, au mtakatifu yeyote isipokuwa mashujaa hao tu wa Imani peke yako… Hao wengine watakachokuja kushuhudia ni matokeo tu ya majina hayo jinsi yatakavyokuwa na uwezo wa kipekee na mamlaka katika huo ufalme unaokuja wa Yesu Kristo Bwana wetu. Hupendi kupewa jina jipya dada?, hupendi kupewa jina jipya kaka?

Hivyo mimi na wewe, tunapaswa tufanyaje ili tushinde?

Ni kwa kutubu dhambi zetu kikamilifu kama tulivyoambiwa pale juu katika mstari wa 16, na kisha kumkabidhisha njia zetu na Maisha yetu yeye peke yake ayatawale, tukiishi tu kama wapitaji hapa duniani, na pia kuifanya kazi yake kwa uaminifu kwa jinsi kila mmoja wetu alivyokirimiwa neema na Bwana wetu.

Swali ni Je umempa Kristo Maisha yako?, . Kama bado fahamu kuwa leo tumepiga tena hatua nyingine ya kuukaribia ule mwisho, na kesho kama itakuwepo tutaipiga nyingine, na kesho kutwa kama itakuwepo ndio tutakuwa tumezidi kabisa kuukaribia ule mwisho, lakini ghafla moja ya hizi siku Unyakuo utapita, na mlango wa neema utakuwa umeshafungwa. Waliopo nje hawataweza kuingia tena, na waliopo ndani hawataweza kutoka tena…Kama maandiko yanavyosema katika Mhubiri 11: 3 “Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala”.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA TATU WA YOHANA.

UFUNUO: Mlango wa 2 part 3

KUOTA UNAKULA CHAKULA.

BIBLIA TAKATIFU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/15/thawabu-za-siri-za-watakatifu-mbinguni/