YATAMBUE MAJIRA YA KUJILIWA KWAKO.

by Admin | 26 July 2020 08:46 pm07

Hivi unajua kuwa Wayahudi walikuwa wanamtazamia Kristo?..

Kila siku walikuwa wanamwomba Mungu wa mbingu na nchi… amtume Kristo wake duniani, aje awakomboe kutoka katika utumwa wa kirumi na wa dhambi. Na walidhamiria kabisa pindi atakapokuja wamheshimu na wamfurahie. Na hiyo ilimfanya kila mtu alitengeneza picha yake kichwani jinsi atakavyokuwa.

Lakini kama tunavyosoma biblia kipindi alipokuja hawakumjua kama ndio yeye…Na kosa kubwa walilolifanya ni KUTOKUJUA MAJIRA, hilo tu!. Siku zote ukishapoteza kujua majira, basi vitu vitakuja kwa kushtukiza mbele yako.

Umewahi kumwona mtu aliyepata tatizo Fulani na akapoteza kumbukumbu kabisa!..anakuwa katika hali ngumu sana, kwasababu anaweza kuja hata ndugu yake aliyeishi naye miaka yote na asimkumbuke hata kidogo!..kwake kila kitu ni kipya, lakini kumbukumbu zinapomrejea ndipo anashtuka huyu si ni Fulani?.

Umewahi kukaa na saa iliyopoteza majira?..Unaweza kujikuta kunapambazuka ukiwa bado kitandani ukidhani bado ni usiku, kwa kuitazama saa iliyopoteza majira! Hivyo na wewe ukapoteza majira.

Ndicho kilichowatokea wayahudi. Hawakujua wakati wa BWANA KUWAJILIA, walidhani Masihi hawezi kuja wakati kama huo, walijua ni kweli anakaribia kuja, lakini si katika kile kipindi walichopo..walizipeleka tarehe mbele kidogo..na wakajua Masihi atakapokuja atakuwa katika jumbe la kifalme, na atatawala kwa fimbo ya chuma, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake.

Luka 19:43 “Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

44  watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua MAJIRA YA KUJILIWA KWAKO”.

Ndugu upo WAKATI WA KUJILIWA KWA KILA MTU!. Sizungumzii wakati wa kujiliwa kupata Maisha mazuri au nyumba nzuri au fedha nyingi, au mali bali wakati wa kujiliwa na NEEMA YA MUNGU. Kama Wayahudi walivyojiliwa na Bwana lakini hawakuyatambua majira hayo, wakaikataa na mpaka sasa wameachwa katika hali ya ukiwa. Na siku sio nyingi watajua makosa yao na kutubu na kugeuka kumwamini Mwokozi wao waliyemkataa miaka Zaidi ya eflu 2 iliyopita.

Luka 12:54 “ Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.

56 Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya?”

Nguvu unayoisikia inakuvuta kwake jua ni majira ya kujiliwa kwako hayo…usiipuuzie hata kidogo! Na wala usikawie kawie…Na sasa tunaishi katika majira ya kurudi kwa Yesu mara ya pili. Wakati dunia inasema hawezi kuja leo..bado sana aje!…lakini alisema atakuja kama Mwivi…hawatajua chochote!…

Ukimwambia mtu kwamba Yesu amekaribia kurudi…kitu cha kwanza atatengeneza picha ya kipindi kirefu sana mbele, siku ambayo atatokea mpinga-kristo mwenye mapembe..pasipo kujua kuwa tayari Ofisi ya Mpinga-kristo ipo sasa duniani. na cheo chake kinajulikana…na tayari maandalizi ya ile chapa yapo tayari..Ni parapanda tu inasubiriwa mambo yote yaanze.

Huu ni wakati wa kuyasoma  na kuyatambua haya Majira tuliyopo!..tupoteze kujua kila kitu lakini tusipoteze kujua majira yetu ili mambo yasije yakatutokea ghafla..

1Wathesalonike 5:1  “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

2  Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3  Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

Kile kinara cha Taa ndani ya Hekalu la Sulemani kilikuwa kinawakilisha nini?

JE! PAKA KULIA USIKU NI ISHARA YA UCHAWI?

MAJONZI YA MTUME PAULO KWA NDUGU ZAKE.

UFUFUO TUNAOUSUBIRIA UTAHITIMISHA YOTE.

Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/26/yatambue-majira-ya-kujiliwa-kwako/