by Devis Julius | 10 August 2020 08:46 am08
Je! Unazijua faida za kufunga na kuomba?
Embu isome Habari ifuatayo kwa makini;
Mathayo 17:18 “Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.
19 Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa?
20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.
21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga”.
Mstari wa 21 unasema.. “Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga”
Hii ikiwa na maana kuwa yapo mambo ambayo mtu atashindwa kuyafanya, haijalishi yeye ni mkristo au la, haijalishi yeye ni mtakatifu au la! kama hafungi na kuomba, basi atashindwa kufanya mambo mengi sana.
Embu tuzitazame faida za kufunga na kuomba..
1) Pale mtu unapofunga, ina maana kuwa hali chakula, au hanywi maji, kwa wakati Fulani, Na hiyo inampelekea mtu kuwa katika uhitaji mkubwa, Sasa uhitaji huo ndio unaoutesa mwili na kufanya mates ohayo yapenye mpaka kwenye nafsi ya mtu. Nafsi ya mtu ikishapokea mabadiliko hayo inaifanya roho ya mtu kuwa na mwitikio wa tofauti sana katika mambo ya rohoni. Tofauti na mtu ambaye hajafunga kabisa.
Kufungu kunakwenda sambamba na magonjwa, kwamfano mtu aliye katika hali nzito ya kuumwa au kuugua mwilini, mateso yale huwa yanashuka mpaka kwenye nafsi ya mtu, na ndio hapo utaona wagonjwa wengi wapo karibu na Mungu kuliko watu walio na afya zao,
Sasa turudi katika kufunga, pale unapofunga hata maombi yako yanakuwa na uzito wa tofauti ukilinganisha na siku nyingine ambazo ulikuwa hufungi, (jaribu hilo utalithibitisha) kama ulikuwa katika kuyatafakari maandiko, uelewa wako unakuwa wa ndani Zaidi tofauti na siku nyingine ambazo ulikuwa hufanyi hivyo .
Na kwa jinsi atakavyozidi kuenendelea kufunga kwa siku nyingi, ndivyo utakavyozidi kuwa mwepesi katika mambo ya rohoni.
Musa alifanikiwa kufunga siku 40 asiku na mchana bila kula, na sote tunajua ni nini alipata kule mlimani..Mungu alizungumza naye uso kwa uso, na kumpa zile Amri 10, Vivyo hivyo hata kwa Eliya naye alipofunga siku 40, Mungu alisema naye kwenye ule ule mlima wa Musa..
Halikadhalika na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, yeye pia alifunga siku 40 usiku na mchana bila kula chochote, mpaka ibilisi akatokea kumjaribu na kushindwa na aliposhuka kule mlimani alishuka na nguvu nyingi za Roho Mtakatifu ndipo akaanza kuhubiri injili na kuponya wangojwa katika Israeli yote.
Hivyo mifungo ya muda mrefu inafaa sana.
2) Faida nyingine ya kufunga inakusaidia kushusha chini matamanio ya mwili. Kwa kuwa chakula kinakuwa hakina sehemu kubwa katika mwili kwa wakati huo, hivyo hata kazi za uzalishaji wa homoni, zinapungua na hivyo inamfanya yule mfungaji awe katika hali ya utulivu Zaidi katika kumtafuta Mungu.
Biblia inatuambia pia, ukifunga, Mungu anakupa thawabu, Hiyo ni kuonyesha kuwa Mungu anathamini kujitesa kwetu kwa ajili yake.
Mathayo 6:16 “Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao.
17 Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso;
18 ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.
Lakini pia unapaswa kujua kuwa kufunga kokote ni lazima kuambatane na kuomba..hivi ni vitu viwili vinavyokwenda sambamba, ni sawa na chai na sukari, unapobandika chai jikoni, inamaanisha kuwa sukari ni lazima iwepo chini pale inaongojea chai iepuliwe, vinginevyo haitaitwa chai.
Vivyo hivyo na Katika kufunga, hupaswi kufunga tu, unaamka asubuhi, unarudi jioni, halafu hufanyi lolote, unarudia tena hivyo kesho, na kesho kutwa,..hapo ni sawa na kufanya “diet” tu , Lakini unapofunga ni lazima uwe na malengo ya rohoni kwanini unafanya hivyo.
Hapo ndipo hapo sasa suala la kuomba lazima lijitokeze; Danieli alipofunga alikuwa mwombaji, vivyo hivyo na watu wote katika biblia..
Danieli 9:3 “Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.
4 Nikamwomba Bwana, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake;
5 tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako”;
Ukizingatia vigezo hivyo basi faida za kuomba ni kama zifuatazo;
Mathayo 26:40 “ Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?
41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu”
Mathayo 6:5 “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao
6 Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi”.
Kama tulivyoona katika mistari ya mwanzoni juu, Bwana aliwaambia wanafunzi wake, pale waliposhindwa kutoa mapepo, kuwa namna ile haitoki isipokuwa kwa kufunga na kusali. Hata wewe unapojijengea ustaarabu wa kuwa mwombaji mzuri, basi unapokea mamlaka kubwa Zaidi ya kuamrisha nguvu za giza ziwatoke watu.
Siri nyingine ya maombi ni kuwa, kwa jinsi unavyodumu kwenye kuomba ndivyo unavyoukaribisha uwepo wa Mungu ndani yako..Na matokeo yake ni kuwa ile furaha ya wokovu inajengeka ndani yako.
Usipokuwa mwombaji, ni ngumu sana kuufurahia wokovu wako, utaona kama Mungu yupo mbali na wewe kila siku, utakosa ujasiri wa Imani yako, lakini ukiwa mwombaji amani Fulani utaipata na ujasiri.
Hivyo kama wewe, ulikuwa unalega lega, au ulikuwa hujua faida za kufunga, basi anza leo kufanya hivyo, pia hakikisha unajijengea utaratibu wa kuomba, saa moja kila siku, hicho ndio kiwango cha chini tulichopewa na Bwana Yesu.Kama ukifanya hivyo hakika utaona matokeo makubwa katika Maisha yako..
Utaona tofauti yako ya leo na jana.
Bwana akubariki.
Ikiwa utatamani kujua Zaidi juu ya faida za kufunga, basi tazama masomo mengine yaliyoorodheshwa chini hapa.
Lakini Kama hujaokoka, na unatamani kuokoka leo, Basi uamuzi huo ni mzuri sana, hivyo fungua hapa kwa ajili ya kuongozwa sala ya Toba >>>>>
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.
Namna ya kuomba
KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.
KIAMA KINATISHA.
NA NENO LA BWANA LILIKUWA ADIMU SIKU ZILE.
SABATO TATU NI NINI?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/08/10/faida-za-kufunga-na-kuomba/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.