NJIA MOJAWAPO YA KUPATA MSAADA KUTOKA KWA MUNGU.

by Admin | 8 September 2020 08:46 pm09

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe. Ni neema za Mungu tumeiona siku nyingine, hivyo nakukaribisha katika kuyatafakari maandiko, ambayo ndio chakula cha roho zetu.

Watu wengi tumekuwa tukitafuta msaada kutoka kwa Mungu wetu, jambo ambalo ni zuri sana, kwasababu hakuna pengine popote ambapo tunaweza kupata msaada, shetani kazi yake ni kutuharibu na si kutupa msaada.

Hivyo basi zipo njia nyingi za kupata msaada kutoka kwa Mungu katika jambo lolote lile unalopitia au unalohitaji.

Njia ya kwanza na ya Muhimu kuliko zote, ni wewe binafsi kupiga magoti na kumwomba Mungu. Kama Maovu na dhambi zote zinazoendelea leo ulimwenguni zinamfikia Mungu, si Zaidi maombi yetu!. Mungu wetu anasikia hata sauti ya mapigo ya mioyo yetu, kila sekunde yanapodunda, hata ile sauti ya jogoo anayewika alfajiri inamfikia, Si zaidi sana maneno yanayotoka katika vinywa vyetu.

Kwahiyo njia ya kwanza na bora ni ile ya kupiga magoti binafsi na kumwomba Mungu hitaji la moyo wako huku ukiamini kwamba anakusikia na atakifanya hicho ulichomwomba kikiwa ni sawasawa na mapenzi yake.

Njia ya Pili, ambayo ndio kiini cha Somo letu, ni ile ya KUWATUMIA WATUMISHI WA MUNGU.

Njia hii sio bora kuliko hiyo ya kwanza lakini ni Njia halali, ambayo imehalalishwa na Mungu mwenyewe. Upatapo shida, au upitiapo jambo lolote..watafute watumishi wa Mungu wa ukweli. Hao Bwana amewapa neema ambayo huwezi kuipata mahali pengine. Watakapokuombea au kukushauri ni rahisi kupata majibu au matokeo yaliyo sahihi kabisa.

Ipo mistari mingi kujifunza juu ya neema waliyopewa watumishi wa Mungu, lakini leo napenda tujifunze mistari ifuatayo ili tupate kuelewa Zaidi.

Marko 6:34  “Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. 

35  Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa; 

36  uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula. 

37  Akajibu, akawaambia, WAPENI NINYI CHAKULA. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula? 

38  Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili. 

39  Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi. 

40  Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini. 

41  Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, AKAWAPA WANAFUNZI WAKE WAWAANDIKIE; na wale samaki wawili akawagawia wote. 

42  Wakala wote wakashiba. 

43  Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia. 

44  Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume”.

Katika mistari hiyo kuna mambo kadhaa nataka tujifunze.

Jambo la kwanza Bwana aliwahurumia makutano lakini hakuwapa yeye ile mikate. Badala yake aliwaambia wanafunzi Ndio wawape wao chakula (soma mstari wa 37). 

Jambo la Pili, ni kwamba muujiza ule haukufanyika mkononi mwa Bwana, bali mikononi mwa Wanafunzi wake. Utaona kuwa Bwana alishukuru kisha akaimega ile mikate mitano na samaki wawili na kuwapa wanafunzi… Na wala hakuimega mikate elfu tano na kuwapa wanafunzi. Hapana! Maana yake ni kwamba miujiza ilitendeka mikononi mwa wanafunzi na si mkononi mwa Bwana Yesu. Hivyo likatimia neno Bwana alilowaambia “wapeni nyinyi chakula”, na wanafunzi wakawapa chakula.

Kwahiyo kwa ufupi ni kwamba muujiza ule ulifanywa na Bwana Yesu, kwa kupitia mikono ya mitume wake (watumishi wake). Bwana hakushindwa kufanya yeye, lakini ndivyo ilivyompendeza yeye kuwatumia watumishi wake kutimiza kusudi lake la kuwahudumia watu wake wenye kuhitaji msaada.

Hivyo upatapo tatizo, na hujui pa kuanzia msaada wa kwanza piga magoti mwombe Mungu binafsi, na kama bado unaona una mashaka mashaka, au bado kuna mambo unaona bado hayajakaa sawa..basi watafute watumishi wa Mungu wa kweli…watakusaidia, kwasababu Bwana anafanya kazi kupitia wao. Na Mungu anao watumishi wake karibia kila mahali, kwasababu anajua watu wake wengi wanahitaji msaada. 

Kama unahitaji ushauri wa kimaisha, wa kiroho, au una ugonjwa, au jambo lolote lile, mtafute mchungaji wako, au askofu, mweleze usimfiche kwasababu tatizo unalodhani wewe peke yako ndio wa kwanza unalipitia, kumbe hujui kuna wengi waliotangulia kuwa nalo na likatatulika..hivyo usikubali shetani akutengenezee hofu, na kusema haiwezekani..Chukua hatua kawatafute, na jaribu kueleza kwa kina, kama unavyomweleza daktari unapokwenda hospitali..Ukifanya hivyo ni rahisi kupata msaada kwa haraka sawasawa tu na kama Kristo mwenyewe angekuwepo hapo kukuhudumia…

Na pia nakushauri!..Usiende mikono mitupu!..na wala usiende na saikolojia kwamba anahitaji fedha yako..nenda kama vile unaenda kukutana na Kristo, na kwamba huwezi kuondoka bila kuacha chochote cha kumshukuru Mungu. Ukifanya hivyo utaona matokeo makubwa sana.

Na pia kama wewe ni mtumishi wa Mungu wa kweli,  utawahurumia wenye matatizo kama hawa wanafunzi walivyofanya, hata kufikia kupeleka hoja zao mbele ya Kristo. Wanafunzi wa Yesu, hawakuona fursa ya fedha bali waliona matatizo ya watu.. Ingawa walijua wale watu walikuwa na fedha zao mifukono mwao, ndio maana walimwambia Bwana awape ruhusua wakajinunulie chakula, hilo neno kujinunulia linaonyesha kabisa kwamba wale watu ingawa walikuwa na matatizo lakini walikuwa na fedha mifukoni mwao!..

Lakini mitume walihurumia matatizo yao na hawakutamani fedha zao. Na nani ajuaye pengine baada ya kupokea ile miujiza ya kula mikate na kushiba, zile fedha walizokuwa nazo walizitoa pale kama sadaka!!!..pengine walitoa kwasababu katika hali ya kawaida hakuna mtu ambaye anaweza kuponywa na kufanyiwa kitu cha kimiujiza na asiguswe kabisa kutoa chochote.  

Na pia tunajifunza kitu kingine kuwa wanafunzi waliwaketisha watu kwa SAFU, watu hamsini na sehemu nyingine watu mia. Pengine yalitengwa makundi ya wanawake na wanaume kivyao, hali kadhalika ya wazee kivyao na Watoto kivyao..hawakuchanganywa wote kwa Pamoja.

 Hiyo ni kutufundisha watumishi kuwa ni lazima katika kuwahudumia watu Utaratibu uwepo.. Mungu wetu ni Mungu wa utaratibu, mahali pasipo na utaratibu basi Mungu hafanyi kazi. Na utaratibu ni Pamoja na kuwaheshimu watu, kujua jinsi gani ya kushughulika na marika..Huwezi kumhudumia mzee kama unavyomhudumia mtoto, huwezi kuzungumza na mzee kama unavyozungumza na kijana. Hekima na heshima lazima viwepo, ndipo Bwana ataachilia miujiza yake.

1Wakorintho 14: 40 “ Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu”

Hivyo ni kwa njia gani utapata msaada kutoka kwa Mungu? Ni kwa kuwatumia pia watumishi wa Mungu, na sio tu msaada wa kimwili, bali pia msaada wa kiroho ambao ni Neno la Mungu.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

UNAZO KILA SABABU ZA KUMSHUKURU MUNGU

Atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? Maana yake nini?

Mafuta yanayozungumziwa kwenye Yakobo 5:14, ni mafuta gani?

Nyamafu ni nini?

HUDUMA YA WALE MASHAHIDI WAWILI.

BWANA SI MWEPESI WA HASIRA, LAKINI BWANA NI MWINGI WA HASIRA.

Nyamafu ni nini?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/08/njia-mojawapo-ya-kupata-msaada-kutoka-kwa-mungu/