JE! NINYI NANYI MWATAKA KUONDOKA?

by Admin | 23 September 2020 08:46 pm09

Shalom, Jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima.

Kama wewe umeokoka, na kwa kitambo sasa upo katika wokovu, nataka nikuambie katika wakati unapaswa uwe nao makini sana basi ni huu, kwasababu neema uliyokuwa nayo kipindi cha mwanzoni ulichookoka, sio sawa na uliyonayo sasa..

Kulikuwa na wakati Bwana Yesu aliwaambia watu wote ikiwemo wanafunzi  wake maneno haya….

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Maneno ya kukaribisha, maneno ya kufariji, maneno ya kutia moyo. Huu ni wakati ambao chochote walichokitaka kwa Bwana walikipita..

Lakini mambo hayakuendelea hivyo hivyo milele..Kuna wakati alianza kuwafundisha wanafunzi wake na makutano kwa namna nyingine,   na baadhi yao kukwazika kwa maneno yake, utaona hakuwaambia tena, njoni, nifuateni, nitawafanya kuwa wavuvi wa watu, hakuwaita tena Boarnege, hakuwaambia tena nyie ni waisraeli kweli kweli msio na waa, kana kwamba anataka kuwavuta..bali aliwaambia  “Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka”?..

Unajua mpaka mtu anakuuliza hivyo ni kiashirio kuwa yupo tayari kwa uamuzi wowote utakaoutoa, ..Kama unataka kwenda ni sawa nenda tu,kama unataka kubaki baki, hakuna kupembelezwa, wala kupewa maneno ya faraja tena..kama unakwenda nenda wala sitakuulizia wala kukutafuta..Lakini Petro kuona hilo alijibu haraka sana..

Yohana 6:67 “Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka?

68 Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele”.

Huo wakati hata wewe na mimi tutaupitia tu..Si muda wote katika ukristo wako Yesu atakuambia Tubu, au njoo kwangu, si kila wakati atakuonya juu ya madhara ya dhambi.. Kuna wakati ile neema uliyokuwa nayo  mwanzo hutaisikia tena ndani yako..Kwasababu Kristo anakuhesabia kuwa umeshafahamu yakupasayo kutenda..

Hivyo, atakapokuona upo nusu nusu, mguu mmoja nje, mwingine ndani, upo ndani ya wokovu lakini mambo ya kidunia bado unayatamani, miezi inaenda, miezi inarudi upo vilevile.. Nataka nikuambie sauti ya Kristo utakayoisikia ndani yako ni hii NA WEWE UNATAKA KUONDOKA? Unataka kurudi nyuma?

Hatakwambia kwa mdomo, lakini atakuambia kwa vitendo. Kipindi hicho, Roho mtakatifu hatakuwepo pembeni yako tena kukushuhudia chochote, au kuugua ndani yako kukuvuta upande wake, kama ilivyokuwa kule mwanzo, ambapo ulipokuwa unaona dhambi unaogopa, hapo utakuwa ni wewe na maamuzi wako binafsi, kuchagua Mungu au dunia..Kristo atakuwa amesimama pembeni anasubiria uamue moja.

Ukichagua dunia, wala hutaona badiliko lolote ndani, unaweza ukafikiri kama vile Mungu hakuoni, utaendelea na hali hiyo hiyo, mpaka siku ile utakapojikuta kuzimu.

Hivyo mimi na wewe tusifikie hicho kipindi ndugu yangu, hata kama Mungu hakupi kile unachokitaka leo hii, hata kama unaona maneno yake ni magumu, hupaswi kufikiria kurudi nyuma au kufikiria mambo ya ulimwenguni, kumbuka walioitwa ni wengi, lakini wateule ni wachache, wanafunzi wa Yesu walikuwa ni wengi sana, lakini waliovumilia mpaka mwisho walikuwa ni 11 tu, na wengine wachache sana mfano wa Mathiya.

Jiulize ni nini kilichokuvuta kwa Yesu zamani, mpaka ukaamua kuokoka, na leo hii ni nini kinachokufanya utake kurudi nyuma? Neema ya kukuvuta haipo tena..Kwako Neno linalobakia kutoka kwa Yesu ni hili; Je! Na wewe unataka kuondoka?

Waebrania 6:4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5 na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri”.

Hivyo tusonge mbele katika Imani, mitume walivumilia mpaka mwisho, lakini sasa sote tunatamani kuwa kama hao,  Lakini wale wengine hata mmoja husikii habari yake baada ya pale.. Hivyo na sisi tukivumilia mpaka mwisho kwa Kristo, tutazirithi Baraka tulizoahidiwa na Mungu tangu zamani.

Taji la uzima limewekwa mbele yetu. Na siku ile tutaketi naye katika kiti chake cha enzi kama alivyotuahidia sisi wakristo wa kanisa hili la Laodikia(Ufunuo 3:21).

Bwana atusaidie, Bwana atutie nguvu sote.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Kwanini Kristo hakuitwa Imanueli badala yake akaitwa Yesu?

JE! KUNA UCHAWI KATIKA KUTENDA WEMA?

YESU AKALIA KWA SAUTI KUU.

KWANINI LEO HII KUNA KUNDI KUBWA LA WAKRISTO WALIORUDI NYUMA?

UNYAKUO.

NA ROHO NA BIBI-ARUSI WASEMA, NJOO!

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/23/je-ninyi-nanyi-mwataka-kuondoka/