KWANINI LEO HII KUNA KUNDI KUBWA LA WAKRISTO WALIORUDI NYUMA?

KWANINI LEO HII KUNA KUNDI KUBWA LA WAKRISTO WALIORUDI NYUMA?

Shalom. Karibu tujifunze Neno la Mungu, maadamu ule mwisho unakaribia..

Kila siku tunapaswa tukumbuke kuwa wokovu ni tunu ya thamani ambayo tunapaswa tuishikilie kwa gharama zozote, wokovu kuupata ni rahisi sana, lakini kuushikilia mpaka mwisho si kitu kirahisi, kwasababu kuna ufalme mwingine (wa giza) hapa duniani ambao upo mahususi kwa kazi hiyo moja tu ya kuhakikisha watu wanaupoteza wokovu hata kama walikuwa wameshaupata.

Na ndio hapa wahubiri tunapaswa tusisitize kwa watu, Kwasababu ndivyo walivyofanya hata na mitume (baba zetu wa imani), ukiangalia utaona mafundisho yao yote yalikuwa ni ya kutilia msisitizo  suala la kuishindiania imani, wakatuambia TUISHINDANIE imani ambayo tumekabidhiwa sisi watakatifu mara moja tu.

Yuda 1:3 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu”.

Sio kwamba walikuwa hawaoni fursa za kibiashara zilizokuwa zimewazunguka mitaani mwao, walikuwa wanaziona, pengine hata zaidi ya sisi, lakini hawakuona sababu ya kutuandikia kwenye hichi kitabu kinachoitwa biblia, kwasababu walijua  vita hasaa vipo wapi, mapambano hasa ya mwanadamu duniani yapo wapi..

Tukumbuke kuwa tukibadilishwa maisha yetu, na kufanywa kuwa viumbe vipya, mambo hayatabakia kuwa vilevile kama yalivyokuwa mwanzoni.. Shetani ni lazima aamke na kuanza kuuwinda wokovu wako kwa gharama zozote zile.. atakuchukia kwa ukomo wa chuzi pale tu atakapokuona unaanza kupiga hatua katika wokovu wako, na sio katika mafanikio ya biashara yako, shida yake kubwa ni Imani yako.

Na katika kipindi ambacho unapaswa ujiandae kukutana naye uso kwa uso basi ni wakati ambapo umeanza maisha mapya ya wokovu.

Lakini kama usipoliweka hilo akilini, ukaambiwa ukiokoka basi, wewe ni wa mbinguni moja kwa moja, njoo sasa tukufundishe mambo mengine ya kidunia..Nataka nikuambie maisha yako ya rohoni yapo hatarini sana kugeuka.(Ndio maana kuna kundi kubwa la wakristo waliorudi nyuma leo hii).

Kwasababu shetani ni lazima atahakikisha analeta mambo mawili kwako, la kwanza ni DHIKI, na la pili ni UDHIA.

Mathayo 13:20 “Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha;

21 lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa”.

Dhiki, ni mateso unayoyapata kutokana na kile ulichokiamini; Na udhia ni maudhi utakayoyapata kutoka kwa watu, kwa kile unachokiamini, huu ndio wakati ambapo pengine hata ndugu/familia hawatakuelewa au watakutenga, ni wakati ambapo pengine utajikuta unapingwa na viongozi wako wa dini, au wanakupiga na kukufunga kisa tu umemfuata Yesu, au umekuwa na msimamo Fulani wa Neno la Mungu, ni wakati ambapo mambo yako yanaweza yasiende sawa, utapitia kuvunjwa moyo mara kadhaa, lakini Mungu atakuwa pamoja na wewe,  kumbuka yote hayo yanasababishwa na shetani, ili tu kukutikisha urudi ulipotoka. Yanatokea kwa ruhusa maalumu kutoka kwa Mungu.

Lakini ni ya muda tu, hayawezi kudumu milele, Mungu hawezi kuruhusu yadumu milele. Kuna kipindi kitafika yataisha. Lakini ni wachache sana wanaoweza kuvumilia hata hicho kipindi kiishe..

Na hapa ndipo watu wengi wanaporudi nyuma. Na kuuacha wokovu. Kwasababu hawakujiandaa kwa huo wakati.

Kumbuka kuwa tutaufikia mwisho mzuri wa imani, kwa kuishindania kwa gharama zozote na  kwa kuvumilia..hilo tu.

Luka 8:15 “Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia”.

Bwana atusaidie tuweze kuyashinda hayo yote.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je kupiga miayo ni ishara ya mapepo?

MUNGU HANA MBARAKA MMOJA TU!..MWAMINI.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Daawa ni nini kama tunavyosoma katika biblia?

FUNGUO ZA UZIMA, MAUTI NA KUZIMU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments