JE! KUNA UCHAWI KATIKA KUTENDA WEMA?

JE! KUNA UCHAWI KATIKA KUTENDA WEMA?

Ni wajibu wa kila mkristo kutambua kuwa kuna vita vikubwa sana katika kuyafanya mapenzi ya Mungu, na mapenzi ya Mungu ni Neno la Mungu..Mtu anapolisoma Neno la Mungu na kulielewa na kulifanya au kulitenda kama lilivyoandikwa, hapo anakuwa anafanya mapenzi ya Mungu.

Leo tutakwenda kutazama kipengele kimoja cha Neno la Mungu ambacho huwa shetani anakiua kwa watu wengi. shetani huwa hapendi watu walishike Neno la Mungu, kwasababu Neno la Mungu ndio ufunguo wa mafanikio yote.

Kwamfano Neno la Mungu linasema tuwe watu wa kuomba (Wakosai 4:2, Wafilipi 4:6, Yakobo 5:16, Yuda 1:20) na pia kuomba/kusali ndio ngao pekee ya kujilinda na majaribu ya yule Adui Marko 14:38. Hivyo mtu anayeomba, kamwe shetani hawezi kumshinda kwa majaribu..Na njia mojawapo shetani anayoitumia kuangusha watu ni kwa njia ya majaribu.

Utauliza majaribu kwa namna gani?

Unapopanga kwenda kanisani halafu linatokea jambo la kukukwamisha, hilo tayari ni jaribu, unapopanga kwenda kutenda wema lakini kinatokea kitu cha kuvuruga huo mpango hilo tayari ni jaribu..Sasa majaribu kama hayo yanaweza kuepukika kama ukiwa mtu wa kuomba.

Ukiwa mtu wa kuomba utaona kila unalolipanga linakwenda kama ulivyolipanga…Ulipanga jumapili uende kanisani, unaona siku hiyo inafika hakuna vikwazo vyovyote vinavyojitokeza kuanzia asubuhi mpaka jioni, umepanga uende ukahubiri unaona ratiba zinakwenda kama ulivyopanga n.k.

Sasa turudi kwenye somo letu, lenye kichwa kinachosema je! Kuna uchawi katika kutenda mema?

Ndugu hakuna uchawi wowote katika kutenda wema/mema. Shetani amekuwa akiwatishia watu wengi kuwa ukifanya kitu fulani kwa mtu fulani unaweza kujikuta unalogwa!. Hivyo ni vitisho vya shetani kuwazuia watu wasibarikiwe. Kwasababu anajua funguo mojawapo ya kubarikiwa ni kuwa mtoaji..Bwana wetu Yesu alitufundisha hiyo siri ambayo tulikuwa hatuijui alisema..

Luka 6:38  “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.

Sasa shetani hataki tufanikiwe! Anachotaka tuendelee kuwa jinsi tulivyo..Na ili kuhakikisha hilo linafanikiwa anakimbilia kuligeuza hili neno la Bwana wetu Yesu, linalosema wapeni watu vitu nanyi mtapewa…yeye (shetani) analigeuza na kusema (usimpe mtu usiyemjua kitu usimpe nguo zako, atazipeleka kwa mganga na mwisho wa siku utajikuta wewe ndio unakuwa maskini, atakwambia usisaidie watu barabarani wengine ni wachawi, chuma ulete, utajikuta nyota yako inahamishwa).

Hayo ndiyo mahubiri ya shetani, ya kuwazuia watu wasibarikiwe. Na kwasababu inakuja na vitisho vikali, watu wengi inawaogopesha na hivyo inawafanya wasidhubutu kusaidia saidia hovyo!!. Nimewahi kuona filamu fulani inaonyesha mtu kapita barabarani akakutana na mtu anaomba msaada, na katika kuomba kwake akamsaidia kwa kumpa fedha, ghafla yale matatizo ya yule mtu yakahamia kwake huyo aliyetoa msaada.

Ndugu usidanganyike na injili hiyo ya kuzimu!..(kumbuka kulishika Neno la Mungu ni vita!)..lazima upambane hiyo vita na uishinde..na huishindi kwa maneno tu! Bali kwa kulijua Neno la Mungu vizuri, vinginevyo ni rahisi kwenda na maji..kwasababu shetani anavitisho vya kutosha kuhakikisha hulitendi neno la Mungu. Kila jambo kwako atakuundia picha ya kulogwa tu.

Hivyo ni uongo kwamba ukifanya wema utalogwa, au utafungua mlango kwa shetani kuyadhuru maisha yako…Huo ni uongo

Sasa unaweza kuuliza hata kama “yule fulani namjua ni mchawi, au anaamini ushirikina, au ni mganga wa kienyeji” akija kuniomba fedha au chochote kile nimpe??..je hatanidhuru?..Jibu ni ndio mpe..hutapatikana na madhara yoyote badala yake ndio utabarikiwa…hata kama ni mchawi kaja kukuomba na umeona ni kweli anahitaji msaada mpe usifikiri mara mbili mbili…kwasababu hakuna uchawi katika kutenda mema!..

Mithali 25:21 “Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; 22 Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu”..

Utasema hilo ni agano la kale, vipi katika agano jipya? Kasome Warumi 12:20.

Sasa hapo anasema “Adui yako” na si rafiki yako, maana yake ni kwamba “yule mtu ambaye unaona anaweza kukuletea madhara”.. Huyo ndiye msaidie kwa kumpa chakula au chochote kile, kwasababu hakuna chochote kitakachokupata wewe cha kukuletea madhara unapomsaidia, badala yake hicho ulichompa ndio kitakuwa chachu ya kumponya yeye, na Mungu atakubariki wewe kwa kufanya hivyo.

Ndugu kuna vita kali katika kulishika Neno, tena si ndogo…Hilo Neno la Bwana Yesu kulisoma ni rahisi, lakini ukilileta katika maisha halisi linavita vingi, limejaa vitisho vya shetani ndani yake, limewafanya hata watu wakiona mtu kalala barabarani, kaishiwa nguvu wampite tu! Bila kutoa msaada wowote..wakihofia kwamba endapo wakimsaidia ndio nyota zao zitakwenda hivyo..kumbe kwa kumpita yule ndio wanazipita baraka zao hivyo hivyo.(kasome Luka 10:32-36).

Na  kuna mahubiri siku hizi yanayofundisha kinyume cha hilo Neno zuri la Bwana wetu Yesu Kristo, “neno lililojaa upendo wa ajabu”…lakini wanahubiri na kulitukuza neno la Adui shetani lililojaa chuki na vitisho!. Tangu lini Mungu aliye na upendo akamkataza mwanadamu wake kuwa na upendo?. 

Unataka kupata fursa? Unataka kupata vitu? Unataka kubarikiwa?..Njia ni hiyo (wapeni watu vitu nanyi mtapewa), na sio tu fedha, au chakula.. bali hata faraja..wafariji wanaohitaji kufarijiwa nawe pia siku ya kupata mashaka na masononeko, Bwana atamtuma mtu wa kukufariji, watie moyo wanaohitaji kutiwa moyo ili itakapofika siku ambayo utakuwa umekaribia kukata tamaa, uwe na deni kwa Mungu wako la wewe kufarijiwa pia n.k n.K.

Mathayo 5:42  “Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo. 

43  Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; 

44  lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, 

45  ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 

46  Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? 

47  Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? 

48  Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”

Bwana akubariki, na Bwana atubariki wote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JIEPUSHE NA UNAJISI.

NA ROHO NA BIBI-ARUSI WASEMA, NJOO!

KWA VILE ALIVYOKUWA MTU WA HAKI.

UPONYAJI WA ASILI

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments