Nini maana ya “chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu”?

by Admin | 29 October 2020 08:46 am10

SWALI: Biblia ina maana gani inaposema “chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu”?

Jibu: Tusome..

1Wakorintho 8:8 “Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu.

9  Lakini angalieni huu uwezo wenu usije ukawakwaza wale walio dhaifu”.

“Kuhudhurisha” maana yake ni “kutusogeza karibu na kitu”.. Hivyo biblia inaposema chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu, maana yake ni kwamba “chakula hakitusogezi sisi kuwa karibu na Mungu”.

Huwezi kula mboga nyingi au nyama, au aina fulani ya chakula kikamfanya Mungu awe karibu na wewe zaidi, au huwezi kula chakula fulani kikakufanya Mungu asikukaribia..Kitu pekee ambacho kitatufanya sisi tumkaribie Mungu au Mungu ajitenge na sisi ni dhambi!..basi hicho tu!, wala hakuna kingine..

Isaya 59:1 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;

2 lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusiki”

Kwahiyo tukila chakula chochote iwe nyama ya nguruwe, ya ng’ombe au chochote kile, hata tukila mboga, au aina yoyote ya chakula, hiyo haitusogezi wala kutuweka mbali na Mungu. Ndio maana ukiendelea kusoma mbele..Mtume Paulo anaendelea kusema maneno haya..“maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu.”

Sasa unaweza kuuliza, Vipi kuhusu pombe?, na majani ya bangi je? Ni sahihi kuyatumia kama mboga?. vipi kuhusu sumu? Tunywe sumu na kusema haituhudhurishi mbele za Mungu?.

Pombe yoyote ile ina kilevi, ambacho kwa jinsi mtu anavyozidi kuinywa,inambadilisha mtu huyo akili (inamtoa katika hali ya asili, na kumpeleka katika hali nyingine isiyo ya asili ya kiakili, ambapo matokeo ya hiyo hali ni kuzaliwa kwa mambo maovu..mfano wa mambo hayo  ni ugomvi, uasherati, mizaha, matusi, hasira, mafarakano, kutokujali na mambo mengine mengi ambayo ndiyo yanayomchukiza Mungu).

Kwahiyo pombe sio sawa kuinywa, vile vile na bangi sio sawa kuivuta wala kutumia majani yake kama mboga, kwasababu zina vilevi ambavyo vinamuharibu akili na kumfanya atoe mambo maovu moyoni, na kumfanya awe najisi kama Bwana Yesu alivyosema katika… Mathayo 15:19 “ Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; 20  hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi”

Kimiminika chenye kilevi kama Spirit, kinaweza kutumika kwa matumizi mengine ya nje kama ya kusafishia vidonda, au kuoshea vifaa lakini si kwa kuinywa, kwasababu hizo tulizojifunza hapo juu…lakini nyama ya nguruwe au ya ng’ombe haina kilevi chochote, ambacho mtu akitoka hapo, ataharibika akili na kuwa mtukanaji, au kuropoka, au kuwa na mizaha, au hasira, au itamfanya atafute kufanya uasherati wala uzinzi.

Waefeso 5:17  “Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.

18  Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho”

Ufisadi unaozungumziwa hapo sio ule wa “kuiba pesa” bali ni “tabia ya uasherati uliopindukia, ambyo imechanganyikana na mizaha, na kutokujali”

Kwahiyo chakula chochote kile ambacho hakitufanyi tutoe mambo machafu mioyoni mwetu,  hicho sio dhambi kukila, kwasababu hakituongezei chochote mbele za Mungu wala hakitupunguzii chochote kama biblia ilivyosema hapo.

Sasa swali la mwisho ambalo utauliza ni je! Kama chakula hakitusogezi mbele za Mungu, vipi kuhusu Meza ya Bwana?..je kile si chakula?, na mbona maandiko yanasema tunapoinywa damu yake tunatangaza mauti yake hata ajapo?.

Agizo la kushiriki meza ya Bwana ni agizo la kiibada, kadhalika na agizo la ubatizo..Hatuwezi kusema mkate ule ni chakula kitakatifu kwamba kila tunapokula hata tukiwa nyumbani au tukiwa kwenye sherehe ni kitu kitakatifu, hapana!… wapo wanaoitengeneza mikate ile kwa mfumo ule ule na kuitumia nyumbani mwao kama chakula cha siku zote, na isihesabike kama wameshiriki, kwasababu zile ni kama chapati tu! İsipokuwa zenyewe ni ngumu kidogo..Kwahiyo hata mtu asiyeamini anaweza kutengeneza nyumbani kwake akala kama chakula kingine tu, na isihesabike chochote kwake.

Umeona?..lakini Mkate ule unapotumika kwenye ibada ya meza ya Bwana (Pale waumini wanapokutana na kusema huu ni ishara ya mwili wa Kristo), tayari unabadilika maana, kulingana na tukio hilo, kadhalika maji yanapotumika katika ibada ya ubatizo, tayari yanabadilika maana kulingana na tukio hilo. Lakini baada ya tukio la ibada, yale maji ni kama maji mengine yoyote yanaweza kutumika kuogea au kunyeshea au yakamwagwa… Kadhalika mikate ile inayotumika katika meza ya Bwana au ngano ile baada ya ibada, inakuwa ni ngano kama ngano nyingine tu…haitusogezi mbele za Mungu.

Je umempokea Yesu?..au bado unatanga tanga na mambo ya duniani tu!..Biblia inasema katika Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.

Umeona?..usipotaka kumgeukia muumba wako leo..Ipo miaka inakuja huko mbeleni, ambayo nafasi unayoichezea leo, hutaipata tena..Miaka hiyo utakosa furaha na kutakuwa hakuna msaada..Hivyo kama hujampokea Yesu, nafasi ni sasa..Unachopaswa kufanya ni kutubu kwa kumaanisha kuziacha dhambi zako zote. Kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa Jina la Yesu, na kisha kupokea Roho Mtakatifu na kudumu katika Imani. Ukikubali kufanya hivyo Bwana atakupokea na kukutengeneza

Marana atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Je! Wana wenu huwatoa kwa nani? maana yake ni nini?

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?

JE! SISI KAMA WAKRISTO NI DHAMBI KUSHEHEREKEA KRISMASI?.

SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/29/nini-maana-ya-chakula-hakituhudhurishi-mbele-za-mungu/