JE! SISI KAMA WAKRISTO NI DHAMBI KUSHEHEREKEA KRISMASI?.

JE! SISI KAMA WAKRISTO NI DHAMBI KUSHEHEREKEA KRISMASI?.

Tukisoma biblia hatuoni mahali popote ikitoa msisitizo juu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa au siku ya kufa kwa Bwana wetu YESU KRISTO. Kwamba ni jambo la lazima watu wote walifanye, au walizingatie kama sheria ya kidini, sasa swali linaweza kuulizwa kama ni hivyo basi hatupaswi kujiundia siku au kujiwekea utaratibu wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa au siku ya kufa kwa mwokozi wetu duniani, kwasababu maandiko yahatuagizi kufanya hivyo?.

Hilo swali ni rahisi kulijibu kama tutakaa na kufikiria juu ya maisha yetu ya kila siku. Embu jaribu kufikiria katika maisha yako tangu ulipozaliwa hadi sasa unavyoishi umeshawahi kualikwa katika sherehe za kuzaliwa za watu [Birthday] mara ngapi? Au umeshawahi kufanya sherehe ya kuzaliwa kwako mara ngapi?, au umeshawahi kusikia sherehe za kuzaliwa za watu wengine zikisheherekewa mara ngapi?. Ni wazi utafahamu kuwa aidha kama wewe hujawahi kufanya, au hujawahi kuthamini siku ya kuzaliwa kwako na hivyo huna mpango wa kujisumbua na mambo hayo fahamu kuwa hiyo haimzuii mwingine kutokuithamini siku yake ya kuzaliwa na kufanya sherehe kubwa na kuwaalika rafiki zake na ndugu zake baada ya kuona umuhimu wa kumshukuru Mungu kumwongezea mwaka mwingine wa kuishi duniani.

Vivyo hivyo tukirudi katika ukristo, hakuna sharti lolote lililotolewa na Mungu juu ya kusheherekea sikukuu yoyote ile, iwe ni ya pasaka, iwe ni ya pentekoste, iwe ni ya kuzaliwa kwa Bwana YESU, iwe ni ya kubatizwa , iwe ni ya kitu chochote kile hakuna sharti lolote tulilopewa. Lakini wapo wanaothamini mambo kama hayo katika maisha yao. Wapo wanaoona umuhimu wa kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa mfalme duniani miaka 2000 iliyopita, hivyo wanaona si vema wauache mwaka upite hivi hivi bila kutafuta au kuchunguza ni siku ipi inayoweza kukaribiana na siku Bwana aliyozaliwa ili waisheherekee. Kadhalika wapo wanaodhimisha siku ya kufa kwa Bwana, wanaona umuhimu wa kifo cha Yesu msalaba kilichowaletea wokovu na hivyo hawawezi kujizuia kufurahia na kushangalia kwa sherehe siku hiyo, wapo pia wanaodhimisha siku za kubatizwa kwao, siku ambayo walizaliwa mara ya pili. Wapo pia wanaodhimisha siku za Bwana kuwajibu maombi yako .N.k.

Lakini jambo linalowakwamisha wengi ni pale wanaposhindwa kutambua ni siku ipi hasa ambayo Bwana YESU aliyozaliwa na hiyo inawapelekea wafikiri wanaabudu miungu mingine hususani wanapoona tarehe 25 Disemba, anahusishwa na sikukuu ya kuzaliwa kwa miungu ya kipagani ya kirumi, ndipo wanapoona kuwa ni dhambi mbele za Mungu hata siku hiyo kumfanyia Mungu ibada.

Ni kweli tukichunguka katika maandiko tunaona kuwa Bwana Yesu hakuzaliwa tarehe 25 Disemba, kulingana na baadhi vifungu vinavyodokeza majira ya kuzaliwa kwake, kwamfano kama tukisoma kitabu cha Luka tunaona kuwa malaika Gabrieli alimtokea Zakaria kuhani (babaye Yohana mbatizaji) siku za zamu za ukuhani wa ABIYA.

Luka 1: 5 “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.

6 Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.

7 Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.

8 Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,

9 kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba”.

Kumbe katika siku za zamu za Abiya ambazo alikuwa anafanya kazi za kikuhani ndizo Zekaria alizotokewa na malaika Gabrieli. Na hivyo tukirudi katika agano la kale kuangalia zama ya Abiya ilikuwa ni ya ngapi na inadondokea mwezi gani ndipo tutakapopata majibu ya majira ya kipindi ambacho Zekaria alitokewa na Malaika Gabrieli. Na kama tunavyosoma katika 1Nyakati 24. Inasema:

1Nyakati 24: 7 “Kura ya kwanza ikamtokea Yehoiaribu, na ya pili Yedaya;

8 ya tatu Harimu, ya nne Seorimu;

9 ya tano Malkia, ya sita Miyamini;

10 YA SABA HAKOSI, YA NANE ABIA;

11 ya kenda Yeshua, ya kumi Shekania;

12 ya kumi na moja Eliashibu, ya kumi na mbili Yakimu;

13 ya kumi na tatu Hupa, ya kumi na nne Yeshebeabu;

14 ya kumi na tano Bilga, ya kumi na sita Imeri;

15 ya kumi na saba Heziri, ya kumi na nane Hapisesi;

16 ya kumi na kenda Pethahia, ya ishirini Ezekieli;

17 ya ishirini na moja Yakini, ya ishirini na mbili Gamuli;

18 ya ishirini na tatu Delaya, ya ishirini na nne Maazia”.

Kwahiyo hapo tunaona zamu ya Abiya ilikuwa ni ya NANE katika ufanyaji wa kazi za kikuhani. Na kazi hizo zilikuwa zinafanyia sabato mpaka sabato yaani wiki mpaka wiki, hivyo zama ya Abiya iliangukia wiki ya 8 katika utendaji kazi wa kikuhani. Na tunajua kuwa mwaka wa kiyahudi huwa unaanza mwanzoni mwa mwezi april, na hivyo ukihesabu hapo majuma mawili utaona zamu hiyo inadondokea katikati ya mwezi wa 6. Kwahiyo tunaona hapo Zekaria kumbe alitokewa majira ya mwezi wa 6 na muda mfupi baada ya hapo pengine mwezi wa 6 mwishoni au wa 7 mwanzoni mkewe Elizabethi alipata mimba, na biblia inatuambia pia miezi 6 baada ya kupata mimba kwake Elizabethi Malaika Gabrieli alimwendea Bikiria Mariamu na kumpasha habari za yeye kupata mimba ya Bwana Yesu (Luka 1:26).

Hivyo mpaka hapo tunaona ni mwezi wa 12 katikati au wa kwanza mwanzoni ndipo mimba ya Bwana YESU ilipotungishwa. Na tunajua kuwa baada ya miezi 9 mtoto huwa ndio anazaliwa, sasa ukipiga hesabu utaona kuwa uwezekano mkubwa wa kuzaliwa kwa Bwana wetu YESU KRISTO unaweza angukia katikati ya mwezi wa 9 au mwanzoni mwa mwezi wa 10, kwa kalenda yetu sisi. Na ndio maana utaona pia Bwana Yesu alianza kuhubiri akiwa na miaka 30 na akamaliza akiwa na miaka 33 na miezi 6, na siku aliposulibiwa ilikuwa ni Mwezi wa nne (April). Kwahiyo ukihesabu vizuri hapo utagundua alianza kuhubiri kati ya mwezi wa 9 hadi wa 10, ambao ndio mwezi aliozaliwa.

 

 

Zipo pia thibitisho nyingine zinaonyesha kuwa Kristo alizaliwa majira hayo lakini hatuwezi kuziandika zote hapa. Lakini je! wanaodhimisha siku hiyo tarehe 25 Disemba wanafanya makosa?. Jibu ni hapana kama tulivyotangulia kuona biblia haijatoa amri juu ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Yesu mahali popote, na hivyo yeyote anayefanya hivyo ikiwa ni kwa lengo lake binafsi kwamba anaona umuhimu wa kuunda siku yake inayoweza kukaribiana na siku ya kuzaliwa kwa Yesu ili amtukuze na kumfurahia Mungu, Iwe ni Aprili, iwe ni Agosti, iwe ni Septemba, Iwe ni Octoba, Iwe ni Disemba iwe ni siku yoyote ile hatendi dhambi maadamu kaiweka wakfu kwa Mungu wake, ili kumwabudu na kumshukuru.

Dhambi inakuja ni pale siku kama hiyo ambayo tayari umeshawakwa wakfu kuwa ibada kwa Mungu, halafu siku hiyo inageuzwa na kuwa siku ya kufanya sherehe za ulafi, ibada za sanamu,ulevi, pombe, anasa, uasherati n.k. hiyo ni sawa na kumkufuru Mungu moja kwa moja, na dhambi ya kumkufuru Mungu ni dhambi ya juu sana kuliko dhambi zote. Ni heri kama usingeichukulia kama ni sikukuu ya imani yako, kuliko kuiona hivyo halafu bado unainajisi. Hiyo ni sawa imeiweka nadhiri kwa Bwana halafu umeshindwa kuitoa.

Utakuta mtu ametoka kanisani siku hiyo, pengine hata kashiriki meza ya Bwana, na anajua kabisa siku kama hiyo inapaswa iwe takatifu, kama ni kusheherekea isheherekewa kwa upendo wa Kristo, isheherekewe kwa kuzingatia vigezo vya utakatifu na biblia, lakini badala yake mtu akitoka hapo na kwenda kunywa pombe, na kwenda kuzini, na kwenda kuzurura kwenye vikundi vya ngoma na disco, na kwenda kuabudu sanamu na kuzunguka kwa waganga, kuna hatari kubwa sana. Na Hivyo siku hiyo kwake inageuka kuwa ni laana badala ya Baraka.

Ndugu yangu upo sasa katika majira haya yanayoitwa ya sikukuu, embu kama umependa kuzifanya kuwa ni za Kristo, zifanye ziwe hivyo kweli kweli, uzilinde, na kuzifanya takatifu, vinginevyo itakuwa ni ibada ya kipagani kwako zaidi hata ya hao wapagani wenyewe. Ni maombi yangu wewe kama mkristo utapata akili katika hayo, kumbuka ni majira unayokwenda kuvuka mwaka, mambo mengi Mungu amekuepushia mabaya, tafakari miezi yote hiyo umevukishwa salama, hivyo usimalize mwaka wako vibaya kwa Bwana. Huu ni wakati wa kujinyenyezeka ili Mungu akupe rehema za Mwaka unaoanza.

Mungu akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Nikutakie sikukuu njema, na Heri ya Mwaka mpya katika jina la YESU KRISTO BWANA WETU.

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments