HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

by Admin | 4 November 2020 08:46 pm11

Shalom!. Karibu tuyatafakari pamoja maandiko.

Elimu yoyote ile ya kidunia ni hekima..hekima sio tu kujua Nahau, na misemo na methali. Mtu anayekwenda kusoma elimu fulani labda ya uchumi au udaktari, anaingiza hekima ndani yake ya namna ya kumtibu mtu au namna ya kufanya biashara. Kadhalika na Elimu nyingine zote mtu anazokwenda kuzisomea, anakuwa anajiongezea hekima katika nyanja hiyo anayokwenda kuisomea.

Sasa fomula ya kujiongezea maarifa katika mambo ya kidunia, haina tofauti sana na ile ya kujiongezea hekima katika mambo ya kiMungu. Tunapomwomba Mungu atupe hekima na maarifa katika kumjua yeye, haitakuja tu kwa kumwomba na kisha kukaa kusubiri, hapana!..Bali inakuja kwa kumwomba kwanza, na kisha kwenda kuitafuta.. Unapokwenda kuitafuta kwasababu ulishamwomba Mungu, anachokifanya yeye ni kuifanikisha njia yako katika kwenda kuitafuta…anakupa uwezo wa kuelewa kiwepesi zaidi kuliko kama ungekuwa hujamwomba.

Ni fomula ile ile tu ya mwanafunzi anayemwomba Mungu amfanikishe katika masomo yake, hawezi kuomba Mungu ampe uwezo wa kuelewa na kufanya vizuri katika mitihani na huku ameacha kusoma kabisa, hapo hatapata chochote, lakini kama amemwomba Mungu kwa Imani, na kwenda kusoma ndipo akili yake inaongezewa uwezo mara dufu zaidi ya kuelewa tofauti na yule mwanafunzi ambaye hajamwomba Mungu kabisa.

Na pia katika kuitafuta Hekima ya kiMungu ni hivyo hivyo, Tunapomwomba Mungu atupe hekima ya kiMungu sawasawa na Yakobo 1:5, hatupaswi kusubiri tu!..Ni wakati wa kuiweka imani katika matendo baada ya hapo..kwa kwenda kuanza kulisoma Neno lake kwa bidii na kumtafuta yeye kwa bidii zote, na kwa nguvu zote.

Mathayo 22:37  “Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza”

Ukianza kuweka bidii katika kumjua Mungu, kwa moyo wako wote kiasi kwamba moyo wako wote upo kwake, na unatumia akili zako zote ulizopewa na Mungu katika kumtafuta yeye, na kuifanya kazi yake, na pia unatumia nguvu zako zote Mungu alizokujali za kimwili na kiroho..Hekima ya kiMungu itazidi kuingia ndani yako, na utakuwa unazidi kumjua Mungu na kuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua mambo kwa kadri siku zinavyozidi kwenda.. Bwana ataisafisha njia yako na utakuwa na hekima nyingi.

Utauliza vipi na Sulemani, na yeye aliipata hekima kwa njia hiyo hiyo?

Jibu ni ndio!..Sulemani baada ya kumwomba Mungu hekima, hakukaa tu na ghafla akaanza kujikuta anaelewa mambo…La! hakufanya hivyo, kinyume chake baada ya kumwomba Mungu hekima, alianza kutafuta huko na huko kwa kusoma mambo mengi ya kiMungu na kimaisha, ndipo hekima ikaingia ndani yake, Mungu akamsaidia kupata alichokiomba…Maandiko yanasema hivyo katika mstari ufuatao..

Mhubiri 12: 9 “Walakini, kwa sababu huyo Mhubiri alikuwa na hekima, aliendelea kuwafundisha watu maarifa, naam, akatafakari, akatafuta-tafuta, akatunga mithali nyingi.

10 Huyo Mhubiri akatafuta-tafuta ili apate kuona maneno yapendezayo, na yale yaliyoandikwa kwa unyofu, yaani, maneno ya kweli”.

Huyo ni Sulemani, ambaye baada ya kuomba hekima, akajikita katika kwenda kuitafuta huko na huko, akajikita katika kutafakari sana..na alipopata uelewa wa mambo ndipo akazitunga mithali..Na alikuwa akitafuta kuelewa mambo KWA KUSOMA VİTABU VİNGİ, na kufanya utafiti mwingi, na alikuwa mpaka anachoka mwili kwaajili ya kusoma tu. Mpaka akasema “Kusoma sana kwa uchosha mwili”..

Mhubiri 12: 12 “….. hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; NA KUSOMA SANA HUUCHOSHA MWİLİ”

Je! Wewe ulishawahi kuzitafuta habari za Mungu kwa bidii namna hiyo mpaka Mwili ukachoka?..na uchovu anaouzungumzia hapo na Sulemani sio uchovu wa usingizi (maana kuna mtu atasoma Neno dakika 10 na kusikia usingizi, na mwisho akasema amechoka..Hapo! hujachoka! Bali umekuwa mvivu). Uchovu unaozungumziwa hapo na Sulemani ni kama ule mwanafunzi anaochoka wakati karibia na anapohitimu, baada ya kusoma miaka mingi. Pale ambapo kichwa chake kimejaa maarifa ya kutosha ya kuweza kukabiliana na mtihani wowote unaokuja mbele yake, lakini mwili wake umekuwa dhaifu kwa kuihangaikia hiyo elimu, alipokuwa akijitesa na kujizuia kwa mambo mengi ilimradi tu aipate hiyo elimu.

Bwana atusaidie nasi tuwe kama Sulemani, na tumpende Bwana Mungu wetu kwa mioyo yetu yote, kwa akili zetu zote, na kwa nguvu zetu zote, ili tuweze kuipata hekima ya kiMungu ndani yetu…

Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako”.

Kama hujaokoka, Kristo yupo mlangoni, hizi ni siku za mwisho, na wokovu ndio mwanzo wa hekima..Hivyo mpokee Kristo leo kwa kumwamini na kutubu dhambi zako zote, na kubatizwa. Naye atakukubali, kama alivyosema katika Neno lake.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kuume, maana yake nini?

WALIO NA HEKIMA NDIO WATAKAOELEWA.

MAASI KUONGEZEKA NI ISHARA YA NINI?.

Nini maana ya “katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni”.

MAMBO 5 AMBAYO KILA MKRISTO ANAPASWA KUFAHAMU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/04/hekima-ya-kimungu-inaingiaje-mioyoni-mwetu/