Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe..Ni neema Bwana katujalia kuliona jua tena siku ya leo, karibu tuyatafakari maandiko Pamoja..
Kama tunavyojua tunaishi katika siku za mwisho, na kila dakika inayosogea mbele ndivyo tunavyozidi kuusogelea ule mwisho…Hivyo leo tu tayari tumeshapunguza siku nyingine moja, kati ya zile chache zilizobakia mbele yetu, kuufikia ule mwisho.
Lakini Pamoja na hayo biblia inatuonya kuwa mojawapo ya dalili za kurudi kwa pili kwa Kristo ni kuongezeka kwa MAASI NA MAARIFA. Leo hatutazungumzia sana juu ya kuongezeka kwa maarifa, kama utapenda kufahamu juu ya hilo basi utatutumia ujumbe inbox tukutumie somo lake. Lakini leo tutaangalia juu ya kuongezeka kwa MAASI,(Mathayo 24:12) ambapo tutajifunza kitu cha muhimu sana. Na pia nakushauri kabla ya kusoma somo hili, tenga muda pitia somo fupi lililotangulia kabla ya hili lenye kichwa kinachosema “Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi? Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo?” kwasababu linamahusiano mkubwa sana na hichi tutakachokwenda kujifunza leo.
Ukiyatafakari Maisha ya leo unaweza kusema, ni afadhali na jana na juzi kuliko leo kwa jinsi maasi yanavyozidi kuongezeka…Upendo wa wengi unapoa, mauaji yanaongezeka, chuki zinaongezeka, visasi, ubinafsi, wizi, uasherati na kila aina ya uchafu, unazidi kuongezeka…
Hiyo yote ni ishara ya kurudi kwa pili kwa Kristo, Lakini swali la kujiuliza ni je!.. kwanini ishara ya mabaya ndio iwe dalili ya kurudi kwa Yesu, na si Ishara ya mazuri, yaani kwanini Bwana Yesu asingesema kabla ya kurudi kwake Mema yataongezeka sana?.
Jibu ni kwamba…wakati wa Kristo kurudi, (yaani kipindi kifupi kabla ya kutokea mawinguni) Kiwango cha utakatifu cha watakatifu kitakuwa kipo juu sana.. Na ishara mojawapo ya kuwa kiwango cha utakatifu kimekuwa kikubwa ni kiwango cha maovu kuwa kikubwa.
Ndugu unapoona dhambi zimezidi mipaka, jua kuwa sehemu Fulani mema yamezidi sana… Inaweza isiwe ni watu wengi wanatenda hayo mema, lakini hata kama ni mmoja tu! Basi atakuwa anatenda mema kwa kiwango kikubwa..
Wengi hawalioni hili wakifikiri kwamba kwasababu dhambi ni nyingi katika kipindi hichi basi hakuna kabisa watu wanaompendeza Mungu. Usilisahau hilo siku zote (Maovu kuwa juu ni ishara ya utakatifu pia kuwa juu). Ukiona kuna maasi makubwa sana katika mji fulani jua upande mwingine katika mji huo huo kuna wakamilifu au mkamilifu wa kiwango kikubwa sana.
Wakati Mungu amechukizwa na maasi ya Sodoma na Gomora, wakati huo huo Mungu alikuwa amependezwa sana na mtu mmoja aliyeitwa Ibrahimu, ambaye tunamwita sasa Baba wa Imani, Hivyo Ishara ya maasi kuongezeka Gomora ni ishara ya wema kuongezeka kwa mtu Fulani wa Mungu mahali fulani. Ukiona dunia inazidi kuoza sasa, jua ni ishara kuwa kuna watakatifu mahali Fulani wanazidi kujitakasa sana.
Ukiona sasa hivi kuna wanawake wengi wanaotembea nusu uchi barabarani, na hata wanaingia makanisani wakiwa hivyo… usifikiri ni wote wapo hivyo…Hiyo ni ishara ya kuiogopa sana, kwasababu ni ishara kuwa kuna mwanamke/wanawake mahali Fulani wanaojiheshimu na kujisitiri sana, na kumheshimu Mungu kwa viwango vya kimbinguni..
Unapoona kuna wimbi la manabii wa uongo..ni jambo la kuogopa wala sio la kucheka na kudharau, kwasababu hiyo ni ishara kwamba kuna kuna watumishi wa Mungu wa kweli. Biblia inasema katika siku za mwisho magugu na ngano vyote vitakomaa.. hivyo ukiona shambani magugu yamekomaa jua na ngano pia zimekomaa…Ndio maana mavuno yanakuja.
Hata Maisha ya kawaida yanatufundisha..Ijapokuwa miaka hii watu wanaonekana duniani kuwa dhaifu, na magonjwa kuongezeka na uwezo kupungua…lakini ukifuatilia rekodi, utagundua kuwa bado zinavunjwa kila mwaka.
Mtu mwenye mbio kuliko wote anaishi miaka yetu hii hii ambayo watu wanakula vibaya, watu wana magonjwa sana n.k. kumbe katikati ya kizazi ambacho watu ni wadhaifu watakuwepo watu ambao ni Hodari kuliko wote katika historia?.
Na katika Imani ni hivyo hivyo…Katikati ya maovu ya dunia yaliyokithiri, Bwana anao watu wake walio waaminifu, wakati wa mfalme Ahabu ambapo Yezebeli mke wake aliifanya Israeli kuwa nchi ya kichawi kiasi kwamba manabii wote waliouliwa, lakini mahali Fulani alikuwepo Eliya Mtishbi, na kama hiyo haitoshi walikuwepo pia manabii wengine 7000 ambao hakupigia goti baali katika mji, Bwana aliojisazia.. Hivyo ndugu huu sio wakati wa kusema aaah! dunia imeharibika yote, hivyo na mimi lazima niwe mwovu…au aaah siku hizi hakuna watakatifu hivyo hakuna haja ya mimi pia kujitakasa..n.k Usikubali kuusikiliza huo ni uongo wa shetani ambao upo kama KILEVI, shetani anawalevya watu wote wa ulimwengu, wafikiri kwamba hali inafanana kila mahali na kwa kila mtu.
Likumbuke hili neno.. Mhubiri 7:10 “Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi? Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo”.?
Bwana atusaidie tufumbuke macho..na tuzidi kujitakasa. Maadamu wakati siku ile inakaribia.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MKUMBUKE MKE WA LUTU.
DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.
MAONO YA NABII AMOSI.
Wanaowachukua wanawake wajinga mateka ni akina nani?
YONA: Mlango wa 4
UFUNUO: Mlango wa 3 part 3
Rudi Nyumbani:
Print this post
Amen watumishi wa Mungu
Mungu atusaidie