LANGO LIMEBADILIKA.

by Admin | 26 November 2020 08:46 pm11

Ezekieli 44:1 “Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa.

2 Bwana akaniambia, Lango hili litafungwa, halitafunguliwa, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana Bwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa”.

Shalom,

Kwa jinsi tunavyozidi kuishi hapa duniani ndivyo dunia inavyozidi badilika kwa kasi sana mbele ya macho yetu, na haibadiliki kuelekea pazuri, bali inabadilika kuelekea pabaya..Inabadilika kuelekea kwenye maovu mengi zaidi…Maovu ya jana ni heri kuliko ya leo…Na hiyo ndiyo inayopelekea wokovu kuwa mgumu kupatikana mioyoni mwa watu siku baada ya siku.

Ukitazama mistari hiyo, ambayo iliandikwa katika agano lake, na nabii Ezekieli inazungumzia juu ya unabii wa Masihi siku atakapokuja na kuingia hekaluni kupitia lango la mashariki, unabii huo upo mwilini na rohoni, lakini lengo leo sio kuzungumzia habari hizo .. Nachotaka uone ni huyo ujumbe uliopo hapo, kwamba, hilo lango lipo wazi lakini siku moja litafungwa, na likishafungwa kamwe halitakaa lifunguliwe tena daima.. Huo ndio ujumbe, Na wote tunajua kuwa lango hilo ni Neema ya wokovu.

Sasa   tukirudi kipindi cha agano jipya, tunaona  tena Yesu akilitaja lango hilo, lakini safari hii yeye halitaji tena kama “Lango”Kana kwamba ni kubwa sana.. bali analitaja kama mlango, na tena sio mlango tu, bali ni mlango mwembamba sana..tusome..

Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze

25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango,…..”.

Unaona? Sasa utajiuliza ni nini kimetokea mpaka sio lango tena bali ni mlango?

Ni kwasababu majira yanabadilika, Mlango wa mbinguni tangu zamani, Mungu aliukusudia uwe mpana ili watu wote waingie na ndivyo ulivyo, alikusudia uwe mwepesi kwa watu wote na mataifa yote kuuingia, ni LANGO pana sana. Hilo ndio lengo la Mungu hata sasa, Mungu hawezi kumminya mtu kwa makusudi kwamba akipate kile kitu kwa shida, sasa atufanyie hivyo ili iweje?.

Lakini kutokana na maovu na mambo mengi yaliyopo ulimwenguni sasa imepelekea mlango huu kuwa mwembamba sana, na hyo ni kutokana na kuzuka kwa milango mingine mingi sana ya upotevuni, na watu wamekuwa wakiiangalia kwa hiyo, na kusahau lile lango moja tu la Mungu.

Ndugu yangu, hizi ni nyakati mbaya sana tunazoishi, leo utaudharau wokovu wa Yesu Kristo, lakini alishatabiri kuwa kuna siku ataufunga mlango huu, na siku hiyo utakapofungwa ndipo watu watakapogundua kuwa walikuwa wanapuuzia kitu cha msingi sana, cha uzima wa roho zao.. Ndipo watakapoanza kubisha wafunguliwe, kumbe hawakujua  kuwa lango hilo likishafungwa mara moja, halitafunguliwa tena daima. Kitakachofuata baada ya hapo ni matujo makubwa sana ambayo hayajawahi kutokea duniani kote.

Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;

26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.

27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.

28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje.

29 Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.”

Hivyo wokovu sio wa kukwepwa, injili si ya kudharauliwa wala kupuuziwa kabisa, huu si wakati wa kumwangalia jirani, au ndugu, au mzazi, katika suala lako la wokovu, Ni wakati wa kumkimbilia Kristo na kumwangalia yeye tu, kwasababu muda uliobakia ni mchache, nani ajuaye lango hilo litafungwa leo usiku, au kesho asubuhi. Jiulize Unyakuo ukipita leo halafu ukabaki, na injili zote hizo ulizosikia, na mafundisho yote hayo uliyofundishwa na kujifunza, utaenda kujibu nini mbele ya kiti cha hukumu.

Usikubali kusongwa na jambo lolote, huu mlango umeshakuwa finyu sana.  Kuiingia sio mrahisi tena kama tunavyodhani, hivyo  ni wakati wa kufanya maamuzi magumu, wa kukubali kujitwika msalaba na kumfuata Yesu, na uwe tayari kwenda kubatizwa na  kupokea Mtakatifu.

Bwana akubariki sana.

Ikiwa bado hujabatizwa, na utapenda kupata huduma hiyo ya ubatizo, au kumpa Kristo maisha yako, basi wasiliana nasi inbox au kwa namba hizi +255789001312


Mada Nyinginezo:

Biblia inamaana gani kusema;aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi?

Mlango uitwao “Mzuri” Unaozungumziwa katika Matendo 3:2 ndio upi?

Naomba kujua watakaoenda mbinguni je! ni wengi au wachache?

NI NANI ANAYEUFUNGA MLANGO WA MAARIFA?.

YONA: Mlango 1

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/11/26/lango-limebadilika/