MZUNGUKO WAKO NI UPI?

by Admin | 26 January 2021 08:46 pm01

Ukichunguza utaona Mungu kaweka vitu vingi vya asili katika mzunguko wake. Na kulikuwa na sababu maalumu wa yeye kufanya hivyo..

Mhubiri 1:6 “Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.

7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; HUKO IENDAKO MITO, NDIKO IRUDIKO TENA”.

Hakushindwa kuufanya upepo upotelee tu huko hewani, au maji yapotelee tu ardhini, lakini ameamua kuyaweka katika mzunguko, kiasi kwamba hayo maji unayoyamwaga sasa hivi kwenye sinki, kuna wakati Fulani yatakurudia wewe wewe na utayatumia tena.

Hiyo ni kufunua kuwa kuna mambo mengi ya rohoni yapo kwenye mzunguko wake, na tusipoitambua mizunguko hiyo, yatatupita mengi kama sio kupata hasara nyingi sana.

Lolote unalolifanya sasa hivi, liwe ni jema au baya, moja kwa moja linaingizwa katika mzunguko huu wa rohoni usioonekana. Kama ni baya litaondoka lakini siku moja litakurudia tu.. haijalishi litachukua umbile gani.

Kama ni jema vilevile litakurudia tu, haijalishi litachukua umbile gani baadaye.. Hivyo ni vizuri ukajua wewe upo katika mzunguko upi, Na ndio maana Bwana Yesu alisisitiza sana maneno haya.

Mathayo 7:12 “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; …”.

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.

Ufunuo 13: 10 “Mtu akichukua mateka, atachukuliwa mateka. Mtu akiua kwa upanga, atauawa kwa upanga…”

Hizi ndio kanuni za asili ambazo mtu yeyote akizitumia hata kama sio mkristo, zitamletea majibu tu. Na ndio maana watu wengi wanashangaa kwanini mataifa yaliyoendelea yanazidi kutajirika, japokuwa hayamchi Mungu.

Ukiangalia utagundua kuwa  yanatoa misaada mingi  kila mwaka kwa mataifa maskini, na ndio maana yanazidishiwa.

Vilevile ukimpa Mungu, Ni kama vile umeingizwa kwenye mfumo wa mzunguko wa Baraka zake rohoni, pengine utaona kama umepoteza, lakini siku isiyokuwa na jina kitakurudia tu, kikiwa kimeshindiliwa na kusukwa sukwa, na kumwagika, kinaweza kisirudi kwa namna ile ile, lakini kitarudi kwa thamani ile ile tena mara dufu.

Mithali 11:25 “Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe”.

Lakini ukiwa mwovu, unaiba, unawarusha watu, unadhulumu haki za wengine,  mchoyo, mbinafsi, unawachonganisha wengine, unaua, moja kwa moja unaingia katika mzunguko huo wa laana za waovu, na mwisho wa siku malipo yake yatakurudia kichwani pako ukiwa hapa hapa duniani, tena kwa kusukwa-sukwa na kuzidishiwa na kumwagika.

Mithali 11:31 “Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi Zaidi”?

Kwa maneno hayo machache Mungu atufumbue macho yetu tuelewe tupo katika mzunguko upi. Ili tuishi maisha ya mafanikio hapa duniani.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HALI ZETU JINSI ZINAVYOWEZA KUATHIRI UTOAJI WETU.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Neno Bildi linamaanisha nini kwenye biblia(Matendo 27:28) ?

Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi?

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

JE UPENDO WAKO UMEPOA?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/01/26/mzunguko-wako-ni-upi/