ITAMBUE NAFASI YA WITO WAKO.

by Admin | 29 January 2021 08:46 pm01

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima, karibu tujifunze maneno ya uzima, Leo tutaangazia juu wito, na jinsi unavyoweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.

Tusome vifungu hivi,.

Mathayo 11:18 “Maana Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo.

19 Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake”.

Kama tunavyojua Yohana mbatizaji, aliitwa kwa namna ya kitofauti sana, aliishi maisha ya kuwa mbali na watu kwa muda mrefu jangwani, na kama tunavyojua huko jangwani hakuna vyakula vizuri, au mavazi mazuri, biblia inasema chakula chake kilikuwa ni nzige, na asali  basi!, hakujua juisi ya zabibu, wala supu ya makongoro, wala kuku, wala mayai, wala yogati, wala pizza, wala pilau, bali aliishi maisha ya kawaida kabisa, ya kula vyakula vya jangwani siku zote za maisha yake, na alikuwa na Amani katika maisha yale, wala hakuwa anaona kuna ugumu wowote au uzito wowote kuishi vile.

Vivyo hivyo na mavazi yake yalikuwa ya ngozi, magumu yasiyo na mvuto ..ndio maana Bwana aliwauliza wale watu..

Luka 7:24 “… Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo?

25 Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme”.

Unaona? Lakini maisha hayo ya kuishi majangwani na ya kula mapanzi hayakuwa kanuni kwamba kila mtu ayaishi, na sio kwamba ukiyaishi wewe ndio yatakufanya uwe wa rohoni zaidi ya wengine hapana.. Tunamwona Bwana Yesu yeye alipokuja, biblia inasema alikuwa anakula na kunywa..

Yeye hakuishi jangwani kama Yohana mbatizaji, bali aliishi katikati ya watu, na alikuwa anahudhuria karamu nyingi , na sherehe mbalimbali alizoalikwa na watu wa kawaida pamoja na watu wakubwa kama vile mafarisayo na waandishi, na watoza ushuru. Kwa ufupi hakujizuia kula chochote kizuri alichokaribishwa..mpaka ikafikia hatua watu wengine wakamwona huyu mbona kama ni mlafi, na mlevi? Unaona..

Lakini alikuwa anaufahamu wito wake, na kusudi lake aliloitiwa hapa duniani, Na sote tunajua hakuna mwanadamu aliyewahi kuishi maisha makamilifu yasiyokuwa na dhambi kama Bwana Yesu.

Hata na sisi pia, wito wa Mungu unatofautiana kati ya mtu na mtu.. Lipo jambo Mungu anaweza akawa ameliweka ndani yako, na unaona kabisa ukilifanya katika hali hiyo, ndio litakupa Amani kuliko kufanya katika mazingira kama ya mtu mwingine, ukishaona hivyo wewe fanya bila kuwaangalia watu.

Kuna watu wameitwa katika hali ya uhuru, na kuna watu vilevile wameitwa katika hali ya utumwa biblia inasema hivyo..Ikiwa uliitwa kutumika ukiwa chini ya mamlaka fulani usione vibaya kuwa hivyo, mtumikie Mungu kwenye nafasi yako, kwa uaminifu, na ukalitimiza kusudi la Mungu vema tu, kama alivyofanya  Nehemia, yeye alikuwa ni mnyweshaji wa mfalme, lakini kwasababu alijua nafasi yake na cheo chake alichopewa, alikuwa chachu kubwa ya kuikarabati upya Yerusalemu.

Lakini pia kama uliitwa katika hali ya uhuru, (sio chini ya mamlaka Fulani,) na unaona vema kutumika katika hali hiyo, basi mtumikie Mungu kwa bidii katika nafasi hiyo.

1Wakorintho 7:20 “Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa.

21 Je! Uliitwa u mtumwa? USIONE NI VIBAYA lakini kama ukiweza kuwa na uhuru, afadhali kuutumia.

22 Kwa maana yeye aliyeitwa katika Bwana hali ya utumwa, ni huru wa Bwana. Vivyo hivyo yeye naye aliyeitwa hali ya uhuru, ni mtumwa wa Kristo”.

Vivyo hivyo kuna walioitwa kuoa/kuolewa, na wengine kutokuoa, au kutokuolewa.. Ikiwa wewe huoni shida yoyote kuishi maisha ya kuwa na mke au mume, endelea na wito wako huo huo, mtumikie Mungu, sio lazima uishi kama yule au wale.. Lakini pia ikiwa umeitwa  katika kuoa, au kuoelewa, vilevile umtumikie Mungu kwa uaminifu katika nafasi hiyo.. usione ni vibaya.

1Wakorintho 7:27 “Je! Umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke.

28 Lakini, kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia; lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo.

Mathayo 19:11 “Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.

12 Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee”.

Hivyo wito unatofautiana kati yetu sisi kwa sisi, usijilaumu sana kwanini haupo kama yule, au kama Fulani, au kwanini haufanani na Yohana mbatizaji, Zaidi tumia muda wako kutafuta mapenzi ya Mungu Katika nafasi uliyopo kama alivyofanya Nehemia, kisha uujenge ufalme wa Mungu. Kuna wengine wamebarikiwa ujuzi, kuna wengine mali, kuna wengine ulezi, kuna wengine karama n.k. Hakuna kiungo cha Kristo kinachoweza kukosa kabisa nafasi yake katika kanisa, ikiwa kitamaanisha kweli kumtumikia Mungu.

Hivyo tuanze sasa kujua nafasi za wito wetu, na tuzitumie, kuujenga ufalme wa mbinguni.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KUNA MAJIRA MUNGU ATAIVURUGA MIPANGO YETU.

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

KWANINI MIMI?

UNYAKUO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/01/29/itambue-nafasi-ya-wito-wako/