MATESO YA KUZIMU.

by Admin | 1 April 2021 08:46 am04

Je kuna uthibitisho wowote wa kimaandiko kwamba kutakuwa na mateso baada ya kifo kwa wale watakaokufa katika dhambi?.

Jibu ni ndio.. Tusome,

Luka 16:22 “Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.

23  Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, ALIPOKUWA KATIKA MATESO, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.

24  Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu NINATESWA KATIKA MOTO HUU.

25  Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe UNAUMIZWA.”

Watu wote ambao watamkataa Yesu katika maisha haya, watakapokufa wataenda kuzimu kwenye mateso, watu wote wanaoliharibu hekalu la Roho Mtakatifu (yaani miili yao) kwa kuvaa vimini, nguo za utupu,  zinazochora maungo yao, wanaopaka wanja, wanaopaka hina, wanaoweka kucha za bandia, na wigi ili wafanane na wanawake wa ulimwengu huu, biblia imesema, wote wataingia katika lile ziwa la moto.

Na biblia inazidi kusema kuwa kuzimu haishibi watu na wala haijai,.. ni kubwa kuliko hii dunia tunayoishi.

Mithali 27:20 “KUZIMU NA UHARIBIFU HAVISHIBI;….”.

Mithali 30:15 “……………Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi!

 16 KUZIMU; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!“.

Kuzimu haishibi!!..Inapokea tu watu kila siku kila saa… Ipo nafasi kubwa mno kuzimu na watu wanaingia huko kila siku. Biblia haidanganyi.

Watu wote wanaofanya uasherati, na wanaopenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu, ikiwemo kutazama filamu za kidunia, na tamthilia za kidunia, wote wataenda katika ziwa la moto kama hawatatubu na kuacha njia zao mbaya, hiyo ni kulingana na Neno la Mungu.

Wote wanaocheza kamari, ikiwemo kubeti, na michezo yote ya bahati nasibu. Wakifa katika hiyo hali wataenda kuzimu.

Watu wote wanaoishi na wanawake/wanaume ambao si wake zao/waume zao, na wote wanaotazama picha za utupu katika mitandao, na wanaojichua, na walawiti wote.. hao wakifa sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa la moto, hiyo ni kulinga na Neno la Mungu.

Na wote watakaoingia kuzimu, hakuna mlango wa kurudi tena au kutoka huko, wakiwa katika mateso huko kuzimu watatamani kutubu lakini itakuwa wameshachelewa, watalia lakini hakuna atakayesikia, mateso yao yatakuwa makali usiku na mchana, watakuwa tu katika hali ya majuto, wakijutia kiburi chao, uchafu wao waliokuwa wanaufanya kwa siri au kwa wazi, uasherati wao waliokuwa wanaufanya bila hofu, ulevi wao waliokuwa wanaufanya kila siku, anasa zao N.k

Kwa uchungu na mateso mengi wakiwa huko, watajigundua kuwa shetani alikuwa amewapofusha macho na hivyo watamchukia shetani kwa ukomo wa chuki, lakini watakuwa wameshachelewa, wangepaswa wafanye hivyo kabla hawajaingia huko.

Ndugu hakuna maombi yoyote yanayopanda kutoka kuzimu kwenda kwa Mungu, hakuna kilio chochote kinachotoka kuzimu na kwenda kwa Mungu, wala hakuna utukufu wowote wa Mungu unaotoka kuzimu, hivyo Mungu hasikii kilio cha watu wanaolia kuzimu, wala kelele zao hazimfikii,  wala sifa zao kwa Mungu, hakuna mtandao kati ya kuzimu na mbingu. Walioingia huko ndio wamesahaulika hivyo.

Isaya 38:18 “Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako.  19 Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu..”

Zaburi 6:5 “Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru?”

Shetani kanyanyua mahubiri, yanayosema kuwa kuna tumaini baada ya kifo, yaani wale watu waliokufa katika dhambi  na kuingia kuzimu, wanaweza kutolewa kutoka katika hayo mateso na kuingia peponi, kwasababu Mungu anasikia mateso yao na maumivu yao huko.. USIDANGANYIKE!!. Hakuna nafasi ya pili baada ya kifo, wala hakuna mageuzi wala mashauri kuzimu!!.. Wala hatuwezi kumwombea mtu aliyeshuka kuzimu, wala kumshauri Mungu juu ya hao waliopo kuzimu.

Mhubiri 9:10 “ Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, HUKO KUZIMU UENDAKO WEWE”.

Kaka/Dada unayesoma huu ujumbe, Iepuke kuzimu! Kwasababu kuzimu ipo kweli, sio nadharia, ni kitu halisi kabisa.  Na mtu akishuka huko hatatoka tena milele, na ndilo lengo kubwa la shetani, hataki kwenda mwenyewe kwenye moto wa milele, anataka kwenda na wengi.

Hivyo tusiruhusu hilo, aende peke yake na mapepo yake… Leo hii unapoisikia hii sauti nenda kachome hivyo vimini, na nguo zote za kikahaba, ikiwemo suruali, tupa hayo mawigi na mahereni unayovaa (mwili wako ni hekalu la Roho Mtakatifu).. usiangalie ni kundi kubwa kiasi gani linakiuka Neno la Mungu. Kuzimu utashuka peke yako, wala hutakuwa na jopo kubwa la watu, kama hutatubu. Wale funza wa kuzimu, ambao Bwana Yesu alisema hawafi watakutesa kule kuzimu usiku na mchana, na utalia wala sauti yako haitasikika popote, utakuwa peke yako, katikati ya giza nene, ukiungua tu, kwenye moto usiozimika.

Siku hiyo utasema heri ningesikia na kutubu, nisingekuwepo huku..lakini haitasaidia chochote.

Hivyo geuka leo na kutubu kwa vitendo, hiyo miziki unayoisikiliza ya kidunia  itakupeleka kuzimu, futa yote leo katika simu yako, na itoe katika nyumba yako, hizo filamu acha kuzitazama kuanzia muda huu, haijalishi zinapendwa na kusifiwa na wangapi. Kuanzia leo anza kumfuata Yesu kwa kumaanisha, na wala usiwe mshabiki wa Kristo, bali uwe mfuasi wake.

Kama umeamua kumfuata Yesu leo kwa kutubu, na kudhamiria kuacha vyote.. Bali uamuzi huo ni bora kuliko kitu kingine chochote ambacho ungeweza kukifanya, hivyo ili usirudi tena nyuma na uukulie wokovu, hakikisha unakishikilia kile ulicho nacho kwa bidii sana, kwa kusoma Neno la Mungu kwa bidii, na kutafuta kuzijua habari zake kwa bidii, mahali popote pale anapohubiriwa.

Na pia ili kuukamilisha wokovu wako, ni lazima ukabatizwe ubatizo sahihi kama bado hujabatizwa, Ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi (Yohana 3:23), na kwa jina la YESU KRISTO, ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kulingana na Matendo 2:38, Matendo 8:16, na Matendo 19:5, kwaajili ya ondoleo la dhambi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Ni kweli Waliolala Katika Kristo Wamepotea?(1Wakor 15:18)

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

Kuota upo nchi nyingine.

FUNGUO ZA UZIMA, MAUTI NA KUZIMU.

KUZIMU NI WAPI

Je! kuna maombi yoyote ya kumtoa mtu aliyekufa kwenye mateso ya kuzimu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/04/01/mateso-ya-kuzimu/