YEYE ALIYEUWASHA HUO MOTO LAZIMA ATALIPA.

by Admin | 7 April 2021 08:46 pm04

SWALI: Naomba kufahamu ufunuo wa mstari huu ni upi?

Kutoka 22:6 “Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa”.


JIBU: Kama vile biblia inavyotuambia katika kitabu cha Yakobo kuwa, moto ni kitu kidogo sana lakini kinawasha msitu mnene….Ndivyo ndimi zetu zilivyofananishwa na kitu kama hicho..

Yakobo 3:5 “…. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.

6 Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.

Hiyo ni kututahadharisha kuwa tunapaswa tuwe  makini sana  na vinywa vyetu, kwasababu madhara yatakayotokana navyo, Mungu atayadai yote mikononi mwetu, kwa mfano unapopanda mbegu za fitina katikati ya ndugu, (maneno ya uongo au ya chuki) ikapelekea mpaka wakatengana, au wakafikisha mahakamani, au wakapigana, au wakauana, ujue kuwa madhara hayo yote, Na hasara yote iliyotokea Mungu ataidai mikononi mwako.

Kumbuka moja ya mambo sita ambayo Mungu hapendezwi nayo ni pamoja na kupanda mbegu za fitina katikati ya ndugu.(Mithali 6:19).

Unapochonganisha ndoa za watu, ikapelekea mpaka wakaachana, pengine mpaka ndugu za pande zote mbili wakachukiana, watoto wakaishi bila pendo la wazazi wote, ujue kuwa wewe uliyehusika, utachukua makosa yao yote, Hutanusurika. Hata kama hukukusudia hiyo fitina ilete madhara makubwa kiasi kile.

Ukisababisha mpaka ndugu katika Bwana wakatenda dhambi kwa kujengeana chuki na  vinyongo kwasababu ya usengenyaji wako, na uzushi wako, ufahamu kuwa wewe uliyehusika, utayachukua makosa yao yote.

Yakobo 3:6 “Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum”.

Hivyo kabla hatujasema jambo fulani, au kabla hatujatoa taarifa za mtu kwa mwingine, tunapaswa tutafakari kwanza, na pia tuzithibitishe habari zenyewe, na  tujiulize je kuna umuhimu wowote wa sisi kuzisema? Au kutoa siri Fulani kwa wengine? Kama upo basi ni vizuri kufanya hivyo. Lakini kama hakuna, ni heri tukazilinda ndimi zetu. Kwasababu madhara yatakayotokana na maneno yetu baadaye Mungu atayadai yote mikononi mwetu.

Hiyo ndio maana ya huo mstari;

Kutoka 22:6 “Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa”.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.

KWARESMA IPO KIMAANDIKO?

TAFUTA KUWA NA AMANI NA WATU WOTE.

KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/04/07/yeye-aliyeuwasha-huo-moto-lazima-atalipa/