ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.

by Admin | 10 May 2021 08:46 am05

Moja ya mambo muhimu kuyafahamu pia ni  kuhusu Roho Mtakatifu. Kwasababu Roho Mtakatifu ndio ukamilifu wa sauti ya Mungu kwetu..

Sasa kabla ya kwenda kuzitazama kazi kuu tatu za Roho Mtakatifu, hebu tuweke msingi kidogo wa kuufahamu utendaji kazi wa Mungu, katika ofisi zake tatu.

Wakati wa agano la kale, Mungu alizungumza na watu kutoka mbinguni, mwanzo wa agano hili jipya Mungu akazungumza na sisi ndani ya mwili wa Bwana Yesu.(Waebrania 1:2), na baadaye akazungumza na sisi kupitia Roho Mtakatifu. Ni sawa na kusema.. Mungu alizungumza nasi akiwa juu yetu(Kama Baba), kisha akazungumza nasi akiwa pamoja nasi katika mwili wa kibinadamu (Imanueli) na mwisho Mungu anazungumza ndani yetu kama(Roho Mtakatifu).

Katika hatua hizi tatu, hatua hiyo ya mwisho ndio hatua kamilifu kuliko nyingine zote, kwasababu Ni sauti ya Mungu iliyo karibu sana na sisi kuliko ilivyokuwa juu yetu (kama Baba), au ilivyokuwa pamoja nasi (kama mwana).

Ni sawa mtu azungumze na wewe kwa sauti kuu akiwa juu kabisa kwenye gorofa, kiasi kwamba humuoni ila unachoweza kusikia ni sauti yake tu na wewe upo chini ya hilo ghorofa, bila shaka kuna maneno ambayo unaweza usiyasikie vizuri kwasababu yupo mbali,  hivyo maneno mengine unaweza kuyaelewa kinyume na alivyosema.. Lakini huyo mtu atakapotoka huko aliko na kushuka chini ukamwona, akawa kama mita 5 kutoka mahali ulipo, akizungumza na wewe ni rahisi kumsikia vizuri kuliko alivyokuwa kule juu, ambapo ulikuwa unasikia sauti tu na sasa unamsikia na kumwona, lakini pia bila shaka wakati anazungumza kuna maneno unaweza usiyasikie vizuri, hata wewe unapozungumza na mtu aliye karibu na wewe ni lazima utapitia vipindi vichache vichache vya kuomba arudie alichosema…

Lakini hebu tafakari tena endapo huyo huyo mtu akikukaribia sana kiasi kwamba mdomo wake unafika katika sikio lako, bila shaka hapo utakuwa unamsikia vizuri zaidi kuliko alivyokuwa mita mbili mbele yako..hapo huwezi kumwambia arudie rudie yale anayoyasema.. Hivyo utamsikia vizuri kuliko kawaida, na utamwelewa, kwasababu amesogea karibu sana na wewe.

Na utendaji kazi wa Mungu ni hivyo hivyo, Roho Mtakatifu ni sauti ya Mungu iliyo karibu sana na sisi, haijaishia kusikika masikioni tu, bali inasikika hadi mioyoni mwetu. Ni sauti isiyo na chenga chenga. Sauti ya Bwana Yesu ilikuwa ni kamilifu, lakini ilikuwa na chenga chenga kwetu, hatukuweza kumwelewa vizuri kwasababu alikuwa anazungumza nje ya miili yetu. Ndio maana ilimpasa Bwana aondoke ili Yule Roho aje juu yetu.

Yohana 16:7 “ Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu”.

Umeona hapo? Bwana hana budi kuondoka ili Roho Mtakatifu aje…(Na kumbuka Roho Mtakatifu ndiye Yule Yule Bwana Yesu mwenyewe, isipokuwa anakuja katika roho (soma 2Wakorintho 3:17),

Sasa baada ya kuelewa hayo, twende kwa pamoja tukazitazame kazi kuu tatu za Roho Mtakatifu kwa ulimwengu.

1) Kazi ya kwanza ni kuuhakikisha ulimwengu kwa habari ya DHAMBI  2) Atauhakikisha kwa habari ya HAKI   3) Atauhakikisha kwa habari ya HUKUMU.

Hizi ndio kazi kuu tatu za Roho Mtakatifu kwa Ulimwengu, tutaziangalia moja baada ya nyingine.

1. Kwa habari ya dhambi:

Yohana 16:8 “Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.

9  Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi”

Kuhakikisha maana yake ni “kuweka sawa jambo”. Kitu ambacho hakikukaa vizuri sasa kimewekwa vizuri maana yake kitu hicho“kimehakikiwa”. Kadhalika Hapo Bwana Yesu anasema huyo Roho atakapokuja atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, maana yake hapo kwanza yeye alizungumza kuhusu dhambi lakini hakueleweka vizuri, lakini atakapokuja huyo Roho ataizungumzia vizuri dhambi kwa sauti ya ukaribu zaidi, na atafanya wengi kuelewa dhambi ni nini, kuliko jinsi wangemwelewa Bwana.

  Ndio maana Bwana Yesu anasema hapo… “Kwa habari ya dhambi, KWA SABABU HAWANIAMINI MIMI ”… maana yake yeye aliihubiri sana kuhusu dhambi, lakini watu hawakumwamini. Hivyo Roho Mtakatifu atakuja kuielezea vizuri na wengi wataamini. Na kumbuka dhambi ni “kutomwamini Mwana wa Mungu, kwamba yeye ndiye mkombozi wa ulimwengu. Hiyo ndiyo dhambi…hayo mengine kama uasherati, wizi, uchawi, uuaji n.k ni matokeo ya dhambi. Kwahiyo Bwana Yesu alihubiri sana kwamba “kila amwaminiye atapata uzima wa milele lakini Yule asiyemwamini atahukumiwa, maana yake atakuwa na dhambi”. Lakini pamoja na kuyasema hayo sana kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu, si wengi waliomwamini, ndio maana injili haikufika duniani kote, kipindi Bwana Yesu yupo duniani anahubiri. Ni wachache tu ndio waliokuwa wanaisikia sauti yake, wengine walikuwa hawamwelewi.

Lakini baada ya Roho Mtakatifu kushuka siku ile ya Pentekoste, Petro alivyosimama siku ile kuhubiri habari ya dhambi, biblia inasema watu zaidi ya elfu tatu waliokoka ndani ya siku moja.(Matendo 2:41). Na wakati miezi miwili tu nyuma, Bwana Yesu alizungumza maneno hayo hayo, tena mji ule ule Yerusalemu, lakini waliishia kumsulubisha, kwasababu hawakumwelewa.

Yohana 12:37  “Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini;

38  ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?”

Lakini miezi miwili tu baadaye kama tunavyosoma katika kitabu cha Matendo 2, Roho Mtakatifu alipozungumza kwa kinywa cha Petro, wale ambao hawakumwamini Bwana Yesu Yerusalemu, walianza kumwamini kwa kasi sana.

2. Kwa habari ya HAKI.

Yohana 16:10  “kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena”

Katika kipengele ambacho Bwana hakukigusia kabisa wakati yupo hapa duniani, ni kipengele cha HAKI. Na haki inayozungumziwa hapo, ni haki ile ipatikanayo kwa njia ya IMANI. Hii Bwana hakuigusia kabisa, na lengo la kutoielezea hii ni kwasababu ya ugumu wa mioyo ya watu, Ndio maana aliwaambia “yapo mambo ya kuwaambia lakini kwa wakati huo wasingeweza kustahimili,mpaka huyo Roho atakapokuja”

Yohana 16:12  “Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, LAKINI HAMWEZI KUYASTAHIMILI HIVI SASA.

13  Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake”.

Umeona jambo mojawapo ambalo wasingeweza kustahimili endapo wangeambiwa ni hilo la “HAKI”. Laiti Bwana angewafunulia siri Mitume kwamba, sisi watu wa mataifa nasi ni warithi wa ahadi za Mungu, kwamba kwa NEEMA tunahesabiwa HAKI kwa Kumwamini Yesu, kwamba na sisi ni warithi wa ahadi za Mungu, ni dhahiri kuwa wangerudi nyuma. Wangesema Bwana Yesu kachanganyikiwa. Yule aliyemwita Yule mwanamke wa kimataifa “Mbwa” halafu leo anamwita “mrithi”?.. Yule ambaye aliwatuma na kuwaambia “msifike miji ya mataifa kuhubiri (Mathayo 10:5)” ghafla anawaita tena mataifa ni warithi!!… Yule aliyesema “sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli (Mathayo 15:24)”. Leo hii yeye ndio atutume sisi huko kwao kuhubiri??.. Hakika amechanganyikiwa.

Hivyo Bwana aliliacha hilo hakuwaambia mitume, pamoja na mengine mengi ili yaje kufunuliwa na Roho Mtakatifu baada ya kuondoka kwake. Kwasababu kwa uchanga waliokuwa nao Mitume, wangeambiwa hizo siri, wangemwacha Bwana na kurudi nyuma (wasingeweza kustahimili)

Na siku ya kuifunua hiyo siri  ya HAKI YA MUNGU ilipofika, Roho Mtakatifu alimfunulia kwanza Mtume Petro, kipindi kile cha lile ono la Kornelio, na baada ya hapo alikuja kumfunulia tena Mtume Paulo hiyo siri..

Hebu soma hichi kisa taratibu..

Matendo 11:1  “Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu.

2  Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye,

3  wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.

4  Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema,

5  Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia.

6  Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani.

7  Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule.

8  Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu.

9  Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.

10  Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.

11  Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria.

12  Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule;

13  akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro,

14  atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.

15  Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo.

16  Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.

17  BASI IKIWA MWENYEZI MUNGU AMEWAPA WAO KARAMA ILE ILE ALIYOTUPA SISI TULIOMWAMINI BWANA YESU KRISTO, MIMI NI NANI NIWEZE KUMPINGA MUNGU?”

Umeona hapo? Kornelio ambaye ni mtu wa Mataifa anapokea Roho Mtakatifu  baada ya kuamini, tena Roho Yule Yule waliyepokea wakina Petro walio waisraeli,  bila shaka Petro alijua ni kwanini Bwana Yesu hakuwaambia hiyo siri wakati wapo duniani, alijua ingekuwa ni ngumu wao kumeza!… Maana unaona hapo juu tu kama tulivyosoma, mitume wengine walipopata habari ya kwamba Petro kaingia kwa watu wa mataifa, walishindana naye vikali..Mpaka Petro alipowaelezea kwa utaratibu..

Hiyo ndiyo siri ya Mungu ambayo ilisitirika tangu zamani, kwamba sisi watu wa MATAIFA, ni warithi wa ahadi za Mungu, kwamba tunahesabiwa HAKI YA KUURITHI UZIMA WA MILELE bure kwa njia ya IMANI YA KUMWAMINI YESU, Mitume hapo kabla walidhani wokovu ni kwaajili yao tu! (Wayahudi), lakini kumbe sivyo!.. hata watu wa mataifa pia..

Mtume Paulo naye aliielezea siri hii katika Wakolosai 1:26-27,  na katika Waefeso 3:6, unaweza kuisoma mistari hiyo binafsi.

Hiyo ndio maana Bwana Yesu akasema kwamba…. “kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena”…..Maana yake alipaswa aelezee hiyo Haki, lakini anaondoka anakwenda kwa Baba na wala hawatamwona tena, na wala hataielezea hiyo siri, lakini Roho atakuja kuliweka hilo sawa!..maana yake atalifunulia kanisa.

3. Kwa habari ya HUKUMU.

Yohana 16:11  “kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa”.

Hapo mkuu wa Ulimwengu anayezungumziwa ni  “shetani”. Na Bwana Yesu anasema…Mfalme wa ulimwengu amekwishahukumiwa.. Sasa hukumu inayozungumziwa hapo si ile ya ziwa la moto, (Hiyo ni kweli ilishapitishwa kitambo), lakini hukumu inayozungumziwa hapa si hiyo, bali ni hukumu ya kunywang’anywa mamlaka ya ulimwengu!!. Na kwamba mamlaka yote ya Duniani amekabidhiwa Yesu.

 Na mamlaka hayo shetani aliyapoteza wakati Bwana Yesu akiwa hapa duniani!. Kwajinsi alivyoutoa uhai wake kwaajili ya wengi, akakabidhiwa mamlaka yote ya mbinguni na duniani.

Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI”.

Sasa atakapokuja Roho Mtakatifu, ataliweka hilo sawa katika mioyo ya watu wengi, Watu wataelewa kwa undani ni kwa jinsi gani sasa hivi YESU NDIYE ANAYETAWALA MBINGUNI NA DUNIANI, NA HAKUNA MFALME MWINGINE KAMA YEYE. Mitume hawakumwelewa Bwana Yesu vizuri wakati wakiwa naye!!. Walikuja kumwelewa vizuri baada ya kuondoka kwake!. Kwamba alikuwa ni nani?.. Yule Yohana ambaye alikuwa anaegemea kifuani pa Yesu, ambaye alikuwa anamwona Bwana Yesu kama kaka yake tu! (Yohana 13:23)… Huyo huyo anakuja kumwona Bwana Yesu katika kisiwa cha Patmo kama miale ya moto, na anaanguka chini ya miguu yake kama mtu aliyekufa!! (Kasome Ufunuo 1). Roho Mtakatifu anamfunulia Yule Yule Yesu kama Mfalme wa wafalme, ambaye enzi na mamlaka yote ni zake.

Waefeso 1:20 “aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;

21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;

22  AKAVITIA VITU VYOTE CHINI YA MIGUU YAKE, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo

23  ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote”

Hivyo Roho Mtakatifu, atakapokuja atauonyesha ulimwengu kuwa YULE mkuu wa ulimwengu, shetani…hata kitu! Mbele za Bwana, kashashindwa…

Yohana 14:30 “ Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu”

Hana mamlaka yoyote juu ya wote waliomwamini Yesu..kashahukumiwa na kunyang’anywa mamlaka ya duniani na kuzimu. Wafu wote wanamilikiwa na Bwana Yesu (Warumi 14:9), maana yake ni kwamba mfano wa jambo lililotokea kwa Samweli, kuletwa juu na yule mchawi, kwasasa haliwezekani tena, kwasababu mkuu wa ulimwengu kashahukumiwa (kashanyang’anywa hayo mamlaka), anayewamiliki wafu wote kwasasa ni Mkuu wa Uzima, YESU!. Huyo pekee yake ndiye mwenye mamlaka ya kuileta roho ya mtu  juu na kuishusha chini, yeye peke yake ndiye mwenye mamlaka na uwezo wa kufufua au kuua!.

Kwahiyo kwa kazi hizo tatu ambazo Bwana Yesu alizozitaja, ndizo zinazokamilisha ushuhuda kamili wa Roho Mtakatifu kwa ulimwengu!!..

Na Roho huyo ndiye anayeshuhudia hata sasa…Na anashuhudia kwa vinywa vya watumishi wake waliojazwa na Roho Mtakatifu, Kwamba Kristo ni kweli!, na Watu wote kutoka mataifa yote na makabila yote anawapokea na kuwakubali na kuwahesabia Haki ya kupata uzima wa milele endapo watamjia, Kadhalika Bwana YESU ndiye mmiliki wa mbingu na nchi na shetani hana kitu mbele zake. Hivyo yeye ndio tumaini pekee la kulikimbilia na kulitegemea.

Je umezitii ushuhuda hizo za Roho Mtakatifu???.. kwa Kumpokea Yesu maishani mwako na kutubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha kabisa???, kumbuka yeye anapokea watu wote haijalishi ni kutoka Taifa gani, wala kabila gani.

 Kama bado hujamwamini, basi fahamu kuwa umeukataa ushuhuda wa Roho Mtakatifu maishani mwako.. Na hivyo utakuwa na HATIA kubwa, kwasababu Roho Mtakatifu amezungumza na wewe kwa sauti ya kueleweka kabisa, hivyo umeukataa ushuhuda ulio mkamilifu kabisa.

 Hivyo mpokee leo Yesu maishani mwako, Ukubali ushuhuda wa Roho Mtakatifu, ili ufanikiwe katika roho yako, biblia inasema yeye Roho Mtakatifu anatutamani kiasi cha kutuonea wivu, anatamani aingie ndani yako kuliko wewe unavyotamani aingie ndani yako, hivyo ulichobakisha tu ni kutii!.. kwa kutubu dhambi zako na kwenda kubatizwa ubatizo sahihi, kama bado hujabatizwa. Kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi (Yohana 3:23), na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38).

Na baada ya hapo, Neema ya kipekee ya Bwana itakuwa nawe daima.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/10/zifahamu-kazi-tatu-za-roho-mtakatifu-katika-ulimwengu/