Je ni kweli Yuda hakuwa na dhambi kwa kumsaliti Bwana, kwasababu tayari ilikuwa imeshatabiriwa?

by Admin | 11 May 2021 08:46 am05

Ni muhimu kufahamu kuwa kila kitu kilichopo sasa au kitakachokuja tayari kilishatabiriwa. Watu wanaomtafuta Mungu walishatabiriwa na vile vile watu watakaomkataa Mungu tayari wameshatabiriwa.

Kadhalika upo unabii wa watakaokolewa siku za mwisho, na upo unabii wa watakaotupwa katika lile ziwa la moto.

Unabii wa watakaokolewa siku ya mwisho, ni kama huu ufuatao…

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;”

Na unabii wa watakaopotea siku za mwisho ni kama huu ufuatao…

Mathayo 7:22  “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23  Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Sasa nabii hizo nabii mbili ni lazima zitimie kama zilivyotabiriwa, maana yake watakuwepo watu watakaokolewa na watakaopotea,  hakuna namna yeyote jambo hilo litaepukika, wala kubadilishwa, hata tufunge na kuomba Nabii hizo mbili lazima zitimie.. watakuwepo watakaokwenda jehanamu!..na watakuwepo watakaoenda mbinguni.

Sasa kitu cha kipekee katika Nabii zote Mungu anazozitoa huwa HATAJAGI MAJINA, Kwamba Fulani na Fulani ndio wataokolewa, na Fulani na Fulani ndio watakaopotea. Hapana! Kamwe hatoi majina, ikiwa na maana kuwa nafasi ya kwenda mbinguni ipo kwa kila mtu, vile vile nafasi ya kwenda motoni ipo kwa kila mtu. Hivyo nijukumu la kila mtu kuhakikisha anapambana kuwepo miongoni mwa watakaokolewa, na si miongoni mwa wanaopotea. Na kama akishinda maana yake atakuwa katika lile kundi la waliotabiriwa uzima  wa milele. Lakini akishindwa atakuwa miongoni mwa waliotabiriwa kuingia kwenye adhabu ya milele.

Hivyo hata utabiri wa Yuda kumsaliti Bwana Yesu haukumtaja jina kwamba atatokea Mtu Fulani anayeitwa Yuda, huyo atamsaliti Bwana. Hapana! Hakuna utabiri wowote unaosema hivyo.. bali ulitaja tu tabia.

Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake”

Maana yake ni kwamba miongoni mwa wale mitume 12, kila mmoja alikuwa anayo nafasi ya kumsaliti Bwana na kutimiza unabii huo!, na vile vile kila mmoja alikuwa na nafasi ya kutomsaliti Bwana. Sasa inapotokea mmoja anayeendekeza hiyo tabia ya kutokujali, zaidi ya wengine wote, pamoja na kwamba anaonywa na anaujua ukweli, lakini hataki kubadilika na kuufuata ukweli, basi huyo ndio anachukua nafasi ya kutimiza huo unabii.  Na miongoni mwa wanafunzi wa Bwana wote, ni Yuda pekee ndiye aliyekuwa anaonyesha tabia za kutokujali, alikuwa ni mtu wa kupenda fedha, hata alikuwa anafikia hatua ya kuiba katika mfuko wa Bwana. Ingawa Bwana alishawambia mapema kwamba mmoja wao atamsaliti, lakini Yuda kwa kulijua hilo wala hakujali, wakati wengine walitilia maanani, na kujizuia kwa hali zote ili wasimsaliti Bwana, lakini Yuda hakujali, na mwishowe..akawa yeye ndiye aliyetimiza huo unabii… “Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake”

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba, Yuda alikuwa na hatia kuisaliti damu ya Bwana Yesu, na alifanya dhambi.

Lakini ya Yuda yamepita, Na unabii wake kashautimiza, tumebaki sisi, tunaoishi sasa…je na sisi unabii wetu ni upi?

Tusome 2Timotheo 3….

2Timotheo 3:1 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

2  Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

3  wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

WASALITI, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;

5  wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao”.

Hapo Mstari wa 4 hapo unasema, watatokea watu WASALITI, na sio wasaliti tu!, bali pia watakuwa wakaidi, wenye kujivuna, wakali, wasiopenda mema n.k.. Yuda alikuwa ni MSALITI tu!, lakini hakuwa na hizo tabia nyingine. Lakini hawa wa siku za mwisho wametabiriwa kuwa na usaliti pamoja na tabia nyingine mbaya nyingi juu yake.

Jiulizae kama wewe ni miongoni mwa hao?.. kama una tabia moja wapo ya hizo au baadhi ya hizo, basi fahamu kuwa unautimiza huo unabii bila ya wewe kujua, hivyo huna sababu ya kumshangaa, wala kumlaumu Yuda kwa kumsaliti Bwana, kwasababu wewe ni zaidi ya Yuda.

Bwana atusaidie, tusiwe miongoni mwa watakaotimiza unabii wa watu waovu wa siku za mwisho, bali tutimize unabii wa watu wema watakaotokea siku za mwisho,ambao wataurithi uzima wa milele.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “Siku moja nyuani mwa Bwana ni bora kuliko siku elfu”?

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Tofauti kati ya ufunuo, unabii na maono ni ipi?

Sikukuu ya kutabaruku ni ipi?

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/11/je-ni-kweli-yuda-hakuwa-na-dhambi-kwa-kumsaliti-bwana-kwasababu-tayari-ilikuwa-imeshatabiriwa/