KAMA VILE UMEME UTOKAVYO MASHARIKI UKAONEKANA HATA MAGHARIBI.

by Admin | 17 May 2021 08:46 pm05

Ni kipi kinakupa ujasiri wa kuishi ukristo ya juu juu tu ndugu ?

Bwana atusaidie tujue majira tunayoishi..

Ulishawahi kutafakari kwa makini kwanini Bwana alifananisha kuja kwake na umeme? Kama tunavyosoma katika kitabu cha  Mathayo 24:27-28

“Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

28 Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai”.

Umeme unaozungumziwa hapo sio huu wa transforma unaowaka majumbani, hapana, ni ule wa radi tunaouona sana sana wakati wa mvua, ule mwanga, unaomulika kwa ghafla sana bila hodi, ambapo kwa kawaida ukimulika mara moja usiku, mahali hapo panabadilika unaweza ukadhani ni mchana, kwa jinsi unavyoangaza sana ..

Ndivyo Bwana Yesu alivyoifananisha na siku ya kurudi kwake kuja kulichukua kanisa, Nuru yake itamulika ulimwenguni kote kwa muda mfupi sana, ambao hakuna mwanadamu yoyote anaweza kuutazamia, na Nuru hiyo itamulika, kwa wakati mmoja ulimwenguni kote, kama vile mwanga wa radi unavyoonekana mashariki mpaka magharibi kwa wakati mmoja.

Kipindi hicho, ambacho kipo karibuni kutokea, Yesu atafunua siri ambazo, zitatuandaa moja kwa moja kwa ajili ya kwenda katika unyakuo. Na siri zenyewe hazijaandikwa hata kwenye biblia, kwasababu hakukuwa na umuhimu wa kuandikwa kwasababu, si za wakati wote, bali za wakati maalumu. Ambao ndio huo wa kurudi kwake kulinyakua kanisa lake.

Utauliza maneno hayo tumeyajulia wapi.?

Kumbuka, sikuzote, mwanga wa radi unapowaka angani, kinachofuata huwa ni Ngurumo. Hivi vitu viwili huwa vinakwenda pamoja. Sasa wakati huo ambao Kristo atakapoangaza Nuru yake ulimwenguni kote kwa kipindi kifupi sana.. Kutaambata na NGURUMO za rohoni,. Ndio zile ngurumo SABA zinazozungumziwa katika kitabu cha Ufunuo sura ya 10.

Ngurumo hizo Yohana alizisikia zikitoa sauti zao, lakini alipotaka kuziandika kwa ajili yetu sisi, alisikia sauti ikimwambia asiziandike bali azitie muhuri..Tusome.

Ufunuo 10:3 “Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.

4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike”.

Umeona? Hizo ni jumbe, maalumu ambazo Kristo atazifunua kwa kanisa lake safi, kwa watu maalumu siku hizi za mwisho, wakati huo ambao MWANGA huo utamulika duniani kote. Hatujui ni nini Yesu kakiandaa kwa watu wake, lakini mpaka hakijafunuliwa sasa, ni kuonyesha kuwa ni mambo ya ndani sana ya siri, ambayo hayo ndio yatampa bibi-arusi wa Kristo Imani ya kwenda katika unyakuo.

Sasa mwanga  huo wa rohoni ukishamulika ulimwenguni kote, kama upo nje ya Kristo, basi ujue unyakuo utakupita tu, kwasababu hutaweza kuelewa hata Sauti ya hizo ngurumo saba zitakazonenwa ulimwenguni baada ya hapo.

Utauliza tena hilo tumelijuaje?

Ni kama tu kipindi kile cha Bwana Yesu sauti ilitoka juu mbinguni kuzungumza na makutano yaliyokuwa yanamfuata, lakini kwasababu NURU ilikuwa imeshawapita walichobakia kusikia tu ni ngurumo badala ya Sauti , ndivyo itakavyokuwa siku hiyo..

Yohana 12:28 “Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.

29 Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye.

30 Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu”.

Na ndio maana leo hii unaposisitizwa umtafute Kristo, maadamu muda mchache umebakia, wewe unachukulia mambo rahisi rahisi tu unadhani siku hiyo utaweza kuelewa kitu. Yesu alilijua hilo na ndio maana akatuambia, tujitahidi sasa kwa sababu upo wakati watu wengi watatamani waingie lakini wasiweze..wakati wenyewe ndio huo wakati wa NURU ya mwisho. Kwasababu itamulika kwa haraka sana kama vile radi, hatujui matukio hayo yatachukua muda gani pengine siku kadhaa tu, au wiki kadhaa tu, na kila kimekwisha.

Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.

25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako”;

Mimi sijui unasubiria nini, usiokoke, Wewe unadhani mambo yataendelea kuwa hivi milele? Hujui kuwa hii injili hadi sasa ingepaswa iwe imesharudi Israeli, maandalizi yao yapo tayari, usiku na mchana wanamlilia YEHOVA pale Yerusalemu kwenye ukuta ule wa maombolezo,  kuomba warudishiwe ufalme, lakini sisi tumekaa tu tukidhani, neema hii tutakuwa nayo milele.

Ni vizuri tukajua agenda ya Mungu kwetu ni ipi sisi watu wa mataifa, inashangaza kuona mkristo anachojua ni kutabiriwa tu, na injili za kupokea, na mafanikio ya mwilini basi hana habari na mambo ya ufalme wa mbinguni. Inahuzunisha sana.

Biblia inatuambia “utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.

Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu”, (Wafilipi 2:12-13)

Kumbuka: UMEME na NGURUMO vipo mbioni.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

SIKU ILE NA SAA ILE.

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

UFUNUO: Mlango wa 14

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/17/kama-vile-umeme-utokavyo-mashariki-ukaonekana-hata-magharibi/