Je Elisha alimdanganya Ben-hadadi kuwa hatakufa kwa ugonjwa wake?

by Admin | 24 May 2021 08:46 am05

SWALI: Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu, samahani naomba kuuliza swali kwenye 2Wafalme 8:7-15. Kwanini Elisha alimwambia Hazaeli amwambie mfalme kuwa atapona na wakati Bwana alimuonyesha Elisha kuwa mfalme atakufa. Je! Ni kwanini Elisha alisema hivyo?. Je! Ni kweli alidanganya? Na ni kwanini alifanya hivyo?


JIBU: Tusome vifungu vyenyewe kwa faida ya wengine pia..

2Wafalme 8:7 “Kisha, Elisha akaenda Dameski; na Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, alikuwa hawezi; akaambiwa ya kwamba, Yule mtu wa Mungu amefika hapa.

7 Kisha, Elisha akaenda Dameski; na Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, alikuwa hawezi; akaambiwa ya kwamba, Yule mtu wa Mungu amefika hapa.

8 Mfalme akamwambia Hazaeli, Chukua zawadi mkononi mwako, ukaende ili kumlaki yule mtu wa Mungu, ukamwulize Bwana kwa kinywa chake, kusema, Je! Nitapona ugonjwa huu?

9 Basi Hazaeli akaenda kumlaki, akachukua zawadi mkononi mwake, za kila kitu chema kilichopatikana Dameski, kiasi cha mizigo ya ngamia arobaini, akaenda, akasimama mbele yake akasema, Mwana wako Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, amenituma kwako, kusema, Je nitapona ugonjwa huu?

10 Elisha akamwambia, Enenda, ukamwambie, BILA SHAKA UTAPONA; LAKINI BWANA AMENIONYESHA YA KWAMBA BILA SHAKA ATAKUFA.

11 Akamkazia macho hata akatahayari; na yule mtu wa Mungu akalia machozi.

12 Hazaeli akasema, Bwana wangu analilia nini? Akajibu, Kwa sababu nayajua mabaya utakayowatenda wana wa Israeli; utazichoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, utawaseta-seta watoto wao wachanga na wanawake wao wenye mimba utawapasua.

13 Hazaeli akasema, Lakini mimi mtumwa wako ni nani, mimi niliye mbwa tu, hata nifanye jambo hili kubwa? Elisha akajibu, Bwana amenionyesha ya kwamba wewe utakuwa mfalme juu ya Shamu.

14 Ndipo akamwacha Elisha, akarudi kwa bwana wake; naye akamwambia, Elisha alikuambiaje? Akajibu, Aliniambia ya kuwa bila shaka utapona.

15 Ikawa siku ya pili yake, akatwaa tandiko la kitanda, akalichovya katika maji, akalitandaza juu ya uso wake, hata akafa. Na Hazaeli akatawala badala yake”.

Ukingalia hapo, Elisha hakumdanganya Ben-hadadi kuhusiana na ugonjwa wake. Asingeweza kufanya vile kwani Ben-hadadi hakwenda kwa shari wala kwa dharau, bali alikwenda kwa unyenyekevu mwingi mpaka kuchukua uamuzi wa kubeba na sadaka zake kwa mtumishi wa Mungu. Kwahiyo Elisha kama mtumishi wa Mungu asingewezeka kufanya jambo kama hilo

Hivyo Elisha alipomwambia kuwa atapona, lakini bila shaka kuwa atakufa.. alikuwa anazungumza mambo mawili tofauti, jambo la kwanza ni kuwa kuhusiana na ugonjwa wake aliouulizia kuwa utamletea mauti,  Elisha alimwambia kuwa huo hautamletea mauti, bali atapona, lakini mauti yake itakuja kwasababu nyingine kabisa.

Na ndio maana utaona hapo baada ya siku mbili, biblia inasema alitwaa tandiko la kitanda, (blanketi). Kisha akalichovya kwenye maji, akalitandaza juu ya uso wake akafa. Kwa kawaida ukichukua hata shuka tu jepesi, akafunikwa uso, kisha maji yakamwagwa juu yake, huwezi pata pumzi, utakufa tu. Ndivyo ilivyokuwa kwa Ben-hadadi. Aliuawa kwa kifo kingine kabisa lakini sio cha ugonjwa wake.

Hatujui ni nini kilimpelekea mpaka akafanya vile, pengine labda alipokea taarifa mbaya kutoka kwa maadui zake za kuvamiwa, au alifanyiwa hila na watumishi wake, ikiwemo huyu Hazaeli, hatajui, lakini utaona kifo kilikuja kwa njia nyingine kabisa ya kujinyonga kwa kukosa pumzi na sio kwa ugonjwa.

Hivyo, jambo ambalo tunaweza kujifunza ni kuwa, Mungu anaweza kusema na wewe, juu ya habari ya uzima wako, au mafanikio yako, au amani yako. Lakini wakati huo huo anaweza kuzungumza juu ya kifo chako.

Kwamfano unaweza muuliza Mungu, Je! Nikifanya biashara fulani, nitafanikiwa na kupata faida? Akakujibu ndio utafanikiwa na kuwa tajiri sana mpaka kumiliki mashirika 20 . Lakini kwasababu ulimuuliza juu ya biashara yako tu, hukumuuliza juu ya hatma ya maisha yako ya milele. Unashangaa, baada ya mwezi mmoja unakufa.

Tunapaswa tuwe na hekima ya kutaka kujua pande zote, kama Daudi ambaye alimwomba Mungu, amjalie pia kujua hesabu ya miaka yake hapa duniani. Ili aishi maisha ya kumcha Mungu…

Zaburi 39:4 “Bwana, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu”.

Inasikitisha kuona kuwa watu wanathamini sana mambo ya mwilini, lakini ya rohoni wanayatupalia nyuma. Kana kwamba huko watakapokwenda yatafuatana nao.  Ukiwaeleza habari za mbinguni na kuzimu, wanakupuuzia, wao wanapoona Mungu anapozungumza nao juu ya mafanikio yao, ndio wanadhani wamefika. Kumbe hawajui, hapa duniani ni tuna pita tu.

Mtafute Mungu ndugu yangu.. Vya duniani vinapita!

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Kwanini wale dubu waliowauwa vijana wa Elisha walikuwa wa kike?

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Herode aliliwa na chango, Je, chango ni nini kibiblia?

SALA YA UPONYAJI/MAOMBI YA UPONYAJI.

Maswali na Majibu

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/05/24/je-elisha-alimdanganya-ben-hadadi-kuwa-hatakufa-kwa-ugonjwa-wake/