TABIA ZA WATAKAOMKARIBIA SANA MUNGU SIKU ILE.

by Admin | 1 June 2021 08:46 pm06

Kwa mara ya kwanza Yohana alionyeshwa maono ya jinsi mbinguni kulivyo, na mfumo wake mzima wa utawala ulivyojiunda.

Tukisoma mambo yale tusidhani, Mungu alikuwa anamuonyesha Yohana sinema tu ya mbinguni jinsi kulivyo, Hapana zipo siri kubwa sana zinazotuhusu sisi, endapo tutazitambua.

Leo kwa ufupi tutazama ngazi hizo, na ni jinsi gani zilivyoficha siri za sisi kumkaribia Mungu..

Ukisoma kile kitabu cha Ufunuo, sura ya 4 yote, utaona Yohana alionyeshwa mbingu zikifunga. Na moja kwa moja macho yake yakakiona kile kiti cha Enzi cha Mungu kilichojaa utukufu mwingi.

Lakini kiti hichi hakikusimama peke yake, bali alionyeshwa pia viti 24 ambavyo vimekizunguka kile kiti cha enzi ambavyo vimekaliwa na wale wazee 24, na katikati ya vile viti 24 aliona pia wenye uhai 4 ambao wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi. Na nyuma ya wale wazee 24 kulikuwa maelfu kwa maelfu ya malaika mbinguni  wamemzunguka Mungu, wakimsifu na kumtukuza. Soma Ufunuo sura ya 4 yote.

Embu tusome baadhi ya vifungu kidogo; Tafadhali soma kwa utulivu,usiviruke.

Ufunuo 4:1 “Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo.

2 Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;

3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.

4 Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu.

5 Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.

6 Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma”.

Ufunuo 5:11 “Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu,

12 wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.

13 Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele.

14 Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.

Sasa ni vizuri ukajiuliza kwanini walivyozidi kumkaribia Mungu, walionekana na maumbile tofauti tofauti. Ikumbukwe kuwa hao wote wanaozungumziwa hapo ni malaika, hakuna mwanadamu hata mmoja. Jiulize ni kwanini wawe ni wazee, na si vijana, na vilevile kwanini wale wenye Uhai wanne wawe na maumbile kama yale na si vinginevyo.?

Hiyo ni kufunua kuwa rohoni, na sisi tukitaka kumkaribia sana Mungu, basi hatuna budi kupitia hatua kama za wale wanaoonekana wapo karibu sana na Mungu.

Kwamfano tukiwatazama wale wazee 24, wanafunua kuwa ili mtu aweze kumkaribia Mungu sana, ni lazima awe ni mzee rohoni, awe amekomaa siku za wokovu ndani yake. Awe kama Ibrahimu, awe kama Henoko aliyetembea na Mungu kwa miaka 300 bila kumwacha, awe kama Eliya aliyemtumikia Mungu mpaka uzee wake, awe kama Ayubu, Hana, na Simoni, Zekaria na Elizabeti. Ambao hao walitembea katika haki yote na Mungu wao bila kumwacha. Watu wa namna hiyo, wanapomaliza siku zao hapa duniani, na wametembea na Mungu tangu ujana wao, mpaka kufa kwao, basi ni wazee rohoni. Na hivyo watakapovuka kule ng’ambo watakuwa karibu sana na Mungu.

Kwasababu Mungu naye, anajitambulisha kama mzee wa siku (Danieli 7:9). Hivyo na wale watakaomkaribia ni lazima wawe wameshiba siku za wokovu, Lakini ikiwa wewe unataka kuwa mkristo tu wa kufa ili uende mbinguni, hutaki kutenda mapenzi ya Mungu angali ukiwa hapa duniani, hutaki kukua kiroho, ujue kuwa ukifa leo hii, kamwe hutakaa umkaribie Mungu kule mbinguni, utakuwa mtu baki tu, haijalishi umeikwepa hukumu

Kwa urefu wa somo hilo fungua link hii>>

https://wingulamashahidi.org/2021/02/22/tutamkaribia-mungu-kwa-idadi-ya-mvi-zetu-rohoni/

Sasa tupige hatua mbele kidogo, kumbuka hawa malaika 24 ambao walifanana sana na wanadamu wazee 24 ni kweli walikuwa karibu na sana na Mungu, lakini wapo waliokuwa karibu zaidi ya Mungu kuliko wao. Na hao si wengine zaidi ya wale wenye uhai 4.

Wenye Uhai 4 walisimama moja kwa moja mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, mbele ya wale wazee 24, Ndio makerubi wa Mungu. Hawa walikuwa na nyuso 4 kila mmoja. Uso wa kwanza upande wa kulia ulikuwa ni wa simba, upande wa kushoto ulikuwa ni wa ndama, upande wa nyuma ulikuwa ni wa Tai, na upande wa  mbele ulikuwa ni kama wa binadamu. Ndivyo Ezekieli alivyoonyesha kwa uwazi wote viumbe hai hao  jinsi walivyo (Ezekieli 1:1-26)

Japokuwa Yohana alionyeshwa upande mmoja mmoja wa kila kiumbe hai huyo kwasababu kulikuwa na sababu ya yeye kuonyeshwa vile, Lakini wote hao walikuwa na sura 4 kila mmoja wao (Soma Ufunuo 4).

Sasa kama tulivyotangulia kusema, haikuwa sinema tu, kwamba Mungu anataka kutuonyesha viumbe hao jinsi walivyo wa ajabu hapana. Bali alikuwa anatuonyesha kuwa na sisi tukitaka kumkaribia zaidi yeye. Ni lazima tuwe kama wao Rohoni, kwamba ni lazima uwe na sura hizo nne, ili ukidhi vigezo vya kuwa karibu sana na Mungu. hivyo tu.

Na leo kwa ufupi tutatazama kila uso wa hao makerubi, unawakilisha nini kwa leo. Tukianzana na ule..

USO WA SIMBA:

Kama tunavyojua simba ni mnyama jasiri asiye na woga,

Mithali 30:29 “Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri.

30 Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote;”

Kuonyesha kuwa kama mkristo, ni lazima uvae sura ya ujasiri kwa ajili ya imani yako na injili, kama Yesu Kristo alivyokuwa, na ndio maana anaitwa Simba wa Yuda (Ufunuo 5:6). Yeye hakuogopa mwanadamu yoyote, ilipofika suala la wokovu hata Herode alipotaka kumkamata, aliwaambiwa wale watu akisema “mwambieni Yule MBWEHA”!.. kuonyesha kuwa yeye hababaishwi na mwanadamu yoyote kuhubiri injili.

Vilevile na sisi ni lazima tuwe kama simba tukiwa hapa duniani kwasababu shetani naye hatufuati kama kondoo, bali kama Simba, biblia inasema hivyo katika 1Petro 5:8, Unategemea vipi na sisi tumwendee kwa upole katika kuuharibu ufalme wake?

USO WA NDAMA:

Upande wa kushoto wa vile viumbe walikuwa na uso wa ndama. Kama tunavyojua ndama ni wanyama wa kafara, wa kuchinjwa, wa kuchukua  dhambi za watu n.k. Hivyo hiyo ni kuonyesha kuwa unapokuwa mkristo ni lazima uso wa ndama/mwana kondoo, uwe nao pia. Yaani ukubali kuteseka kila siku kwa ajili ya manufaa ya wengine, na si yako tu peke yako. Ukubali hata kujinyima kwa ajili ya injili,

Paulo alisema..”Ninakufa kila siku”.. 1Wakor 15:31. Hata Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili yetu, ili sisi tupate ondoleo la dhambi. Vivyo hivyo na sisi kama wakristo, tunapaswa tuwe na uso huu wa ndama ndani yetu. Tuwe tayari kufa kila siku kwa ajili ya injili ya Kristo. Kujitoa ikiwemo na mali zetu  na nguvu zetu kwa ajili ya injili., kama alivyofanya Kristo na mitume wake.

USO WA TAI:

Wenye uhai 4 walikuwa na uso wa Tai kwa nyuma. Tai ni ndege anayeiona mbali sana, Jicho lake linaweza kuona chakula kutokea mbali sana, mahali ambapo wewe huwezi hata kumuona juu. Na sio tu chakula, bali pia maadui.

Na ndio maana Bwana Yesu alisema katika siku za mwisho, ni Tai tu ndio watakaoweza kuona chakula cha kweli cha roho kilipo. Wengine wote watakuwa kama kuku, wakisikia Kristo yupo huku wanakimbilia, yupo kule wanakimbilia, manabii wa uongo na imani potofu zikiwachanganya, wanabahatisha kwasababu macho yao hayawezi kuona mbali.

Luka 17:37 “Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai”.

USO WA MWANADAMU:

Wenye uhai 4 hawa walikuwa pia na nyuso wa binadamu kwa mbele.

Kumbuka mwanadamu, ndiye aliyejuu ya zaidi ya wanyama wote ambao Mungu alishawahi kuwaumba. Mwanadamu anao ujuzi, hekima, utashi, fikra, elimu, ujuzi, maarifa. Kwa kutumia tu utashi aliopewa na Mungu anaweza kubuni na kuvumbua mambo makubwa sana, ambayo yanaweza kumletea matokeo chanya au matokeo hasi. Inategemea na dhima yake ni nini.

Hivyo, Na sisi pia ni lazima tutumie utashi wetu tuliopewa na Mungu, kumpendeza Mungu. Sio kila mahali, tutatumia maombi tu peke yake hapana. Wakati ule Mungu anampa Musa maagizo ya kutengeneza vitu vya hemani, alimwambia akamtafute mtu aliyeitwa Bazaleli, ambaye Mungu atampa  ujuzi na utashi wa uchongaji wa vitu hivyo.

Kutoka 31:1 “Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

2 Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda;

3 nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,

4 ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba”,

Tujiulize je! Sisi tulishawahi kumbunia nini Mungu?  Watu wa ulimwengu wanatushinda, wao kila siku wanambunia mungu wao shetani, mambo mapya kila siku, mengi ya kuwavutia wao, wanamtungia kila aina ya nyimbo za miundo tofauti tofauti, lakini sisi kama wakristo, ujuzi wetu tuliopewa na Mungu tumeuweka kapuni, tukimwimbia Mungu badala tufikirie ni jinsi gani nyimbo zetu zitakuwa zimejaa Roho, sisi tunawaiga wale wa kidunia staili zao.

Bwana atusaidie sana.

Hivyo Bwana atusaidie sana. Nyuso zote hizo 4 tuwe nazo. Yaani tuwe jasiri kama Simba, tuwe wa kujitoa kama ndama, tuwe na jicho la kuona mbali chakula chetu kilipo kama Tai, na pia tuwe na hekima na ujuzi kama mwanadamu.

Tukiweza hayo, basi tujue kuwa tutakuwa karibu sana Mungu, kuliko tunavyodhani, kwasababu shetani anakuwa hana upenyo wa kutuingilia. Kwasababu kila upande kuna uso tunamwona.

Mwisho, kabisa, upako wa wenye uhai hawa wanne ulitembea pia katika nyakati saba za kanisa. Hivyo kama utapenda kufahamu kwa urefu juu ya nyakati hizo na jinsi mihuri ile ilivyofunguliwa basi fungua link hii utakutana na mfufulilizo wa maelezo hayo.

https://wingulamashahidi.org/2018/07/19/mihuri-saba/

Bwana akubariki sana.

Je! Umeokoka ndugu? Je! Una habari kuwa tunaishi katika kipindi ambacho tutashuhudia tukio la kurudi kwa pili kwa Kristo duniani?  Unalifahamu hilo? Kwasababu hakuna dalili hata moja Kristo aliyoizungumzia haijatimia. Ni heri ukayasalimisha maisha yako leo kwake, ili siku ile isikukute pabaya.

Tubu kwa kumaanisha kabisa, kisha kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo upate ondoleo la dhambi zako.

Jina la Bwana libarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

UFUNUO: Mlango wa 4

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/01/tabia-za-watakaomkaribia-sana-mungu-siku-ile/