TUTAMKARIBIA MUNGU KWA IDADI YA MVI ZETU ROHONI.

TUTAMKARIBIA MUNGU KWA IDADI YA MVI ZETU ROHONI.

Shalom, nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya uzima, biblia inatuambia..

Mithali 16:31 “KICHWA CHENYE MVI NI TAJI YA UTUKUFU, Kama kikionekana katika njia ya haki”.

Wengi wetu tunatafuta wokovu ili tu tuende mbinguni,  tunadhani wokovu ni kumkiri tu Yesu na kubatizwa, basi imeishia hapo, tunachosubiria tu ni  kufa na kwenda mbinguni.. Ndugu Mawazo kama hayo ndiyo yanatufanya kila siku tuwe watu wa kulegea legea watu wa kusubiri subiri,tukisema siku moja wataokoka, siku tunayokaribia kufa, siku ambayo tukishatimiza malengo yetu ndio tutakayomtumikia Mungu, hatujui kuwa kuchelewa kwetu kunatupotezea nafasi nyingi na kubwa sana mbinguni.

Ndugu yangu, maisha ya mwilini ni kivuli tosha cha maisha ya rohoni. Kama vile katika mwili kuna hatua, ya utoto, utu uzima na uzee, na kwamba ili mtu afikie ile ya mwisho ni lazima azipitie hizi za kwanza zote, vivyo hivyo na rohoni..

Kumbuka Uzee siku zote una kibali, una heshima,  na una utukufu,

Biblia inasema..

Walawi 19:32 “Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi Bwana”.

 Unaona na utukufu wake unadhihirishwa kwa zile mvi zinazotokea juu ya kichwa chake. Hali kadhalika rohoni, kwa jinsi mtu anavyokua kiroho, anavyodumu katika wokovu, anavyomtumikia sana Bwana, ndivyo mvi zake zinavyoongezeka kidogo kidogo, na kwa jinsi atakavyoendelea kung’ang’ana na Bwana atafikia  hatua kichwa chake chote kinajaa mvi, kinakuwa cheupe pe chote.

Ukishafikia hatua hiyo rohoni, ujue wewe ni mtu ambaye utakuwa karibu sana na Mungu utakapofika mbinguni.

Ukisoma kitabu cha Ufunuo, utawaona kuna wazee 24 mbinguni, Wale ni malaika wa Mungu, ambao wanafanana na wanadamu wazee, utajiuliza ni kwanini Mungu kawaweka pale kama wazee  na si vijana au watoto ili wakizunguke kiti chake cha enzi, tena wakiwa katika idadi yao hiyo ndogo ya 24?. Hiyo ni kuonyesha kuwa watu wa namna hiyo, ndio watakaokuwa karibu sana na Mungu hata wakati ule ukifika.

Ufunuo 4:3 “na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.

4 Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu”.

Na kama tunavyojua ili kumtambua mzee  utaona mvi nyeupe katika kichwa chake. Katika biblia tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo akiwa kama mzee wetu wa kwanza rohoni mwenye nywele hizo nyeupe..

Ufunuo 1:14 “Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto”;

Sasa kama tulivyosema, mpaka mtu afikie hatua ya uzee, ni sharti kwanza apitie utoto na ujana,..Vivyo hivyo rohoni ili tufikie ukomavu Mungu anaoutarajia kwetu hatuna budi kuukulia wokovu vya kutosha angali tukiwa hapa hapa duniani.

Inashangaza kuona mtu anayachukulia maisha yake ya rohoni, kirahisi rahisi tu, leo inapita bado yupo katika dhambi, kesho nayo hivyo hivyo, mwezi unapita, miaka inapita, anasikia tu injili anapuuzia, bado hajali maisha yake ya milele yatakuja kuwaje huko atakapokwenda, yeye anajitaabisha tu na haya maisha ya kitambo ya miaka 80, lakini yale ya mabilioni ya miaka hayaangalii. Anadhani kule ni kufa na kuingia tu, hajua kuwa zipo nafasi na vyeo, ambavyo si watu wote watapewa na Mungu.

Mwingine atasema ameokoka, lakini miaka nenda rudi, bado ni mchanga kiroho, hakui yupo pale pale, maisha yake hayana ushuhuda, ukimuuliza ni nini umefanya kwa Mungu wako, hana, yeye ni kusikiliza tu, basi, akidhani ndicho Mungu alichotuitia hapa duniani.

Tunapaswa tukifika kule tutambuliwe kwa mvi zetu rohoni, tumemtumikia Mungu wetu kweli kweli, sio tunatambuliwa kama vitoto vichanga tena.

Unapoyasikia maneno haya, usiyapuuzie, kumbuka unapaswa uwe ndani ya Kristo ukimtumikia kwa muda wa kutosha ukiwa hapa duniani, ili ujijengee daraja zuri kule unapokwenda, usidhani wokovu ni kuamini tu basi..wokovu ni maisha, kila siku unajenga maisha yako ya baadaye, kama vile unavyojijengea maisha yako ya mwilini.

Hivyo mimi na wewe kuanzia sasa, tutamani kuwa karibu na Mungu, kwasababu tukifa kule tutatambuliwa kwa idadi ya mvi zetu rohoni.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments