NI LAZIMA KUISHIKILIA IMANI MPAKA MWISHO.

by Admin | 22 June 2021 08:46 pm06

Nabii Eliya alikuwa na Imani ya kutosha hata kushusha moto kutoka mbinguni, kuwaangamiza maadui zake, lakini masaa machache tu! baada  ya kushusha moto juu ya dhabihu ile, alimkimbia mwanamke mmoja mchawi aliyeitwa Yezebeli (alimkimbia kwa hofu kabisa), ili kujiokoa nafsi yake (1Wafalme 19). Ni sawa na fahali la ng’ombe na nguvu zake zote, halimwogopi fahali mwenzake, linapigana naye, lakini linamwogopa mbwa na kumkimbia kabisa..ndicho kilichomtokea Nabii Eliya. Alikuwa na Imani ya kuangushwa maadui zake walio magwiji, lakini aliizimisha kwa kumwogopa mwanamke mmoja tu!.

Pia tunaweza kujifunza kwa Petro, mtume wa Bwana Yesu..

Mathayo 14:24 “Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho.

25  Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.

26  Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.

27  Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.

28  Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.

29  Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu.

30  Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.

31  Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, EWE MWENYE IMANI HABA, MBONA ULIONA SHAKA?”

Hapo Mtume Petro, alikuwa na imani ya kuanzia lakini ya kumalizia hakuwa nayo, hatimaye akaanza kuzama kabla ya lengo lake kutimia.

Nasi pia tukumbuke Moto tuliokuwa nao wakati tunamwamini Yesu, ni lazima tuwe nao huo huo, tena na zaidi wakati wa mwisho wa maisha yetu..Hatupaswi hata kidogo kubaki na historia kichwani tu kwamba, miaka Fulani nilikuwa moto sana, miaka Fulani nilikuwa naweza kukesha kusali, miaka Fulani nilikuwa nashuhudia sana, miaka Fulani nilikuwa nasoma Neno sana.

Ukijiona juzi, au mwaka jana ulikuwa moto kuliko mwaka huu, tambua kuwa tayari umeshaanza kuzama…Imani yako imeshaanza kuwa haba!.. Unahitaji kumpigia yowe Bwana Yesu leo! Akusaidie.. Ukiona zile dhambi ambazo ulikuwa unaweza kuzishinda kirahisi mwaka jana lakini mwaka huu huwezi, leo ni wakati wa kupiga yowe, kabla ya hujamalizikia kuzama kabisa..Ukiona ulikuwa unaweza kusali masaa kadhaa lakini leo nusu saa tu ni shida!, unasinzia!, nguvu ya kulisoma Neno huna tena…hapo huna budi kupiga yowe kuomba msaada..kwasababu imani yako imeanza kupungua.

Ukiona ule ujasiri dhidi ya dhoruba zote za shetani, unaanza kupotea ndani yako, unahitaji kumlilia Bwana, ukiona hofu ya wachawi na madhara ya adui yamekuzingira, tofauti na hapo kwanza, ambapo ulikuwa na ujasiri wa kutohofu chochote, basi jua imani yako imeanza kutindika!.. huna budi kumpigia Bwana yowe! Kama ishara ya kutaka msaada..

Poteza kila kitu lakini usipoteze imani yako…kwasababu Imani ni ulinzi. Kamwe huwezi kumshinda adui shetani,  na dhoruba zake kama imani yako ipo chini.

Hivyo chunguza maisha yako leo!.. Je! Bado unayo imani ya kumalizia? Kama huna..leo hii kumbuka uliko toka, kumbuka uweza wa Mungu, mwanzo ulipomwamini, na mlilie Bwana, umwambie unahitaji Imani ya kwanza, na fanya hivyo kwa kumaanisha huku, ukirekebisha makosa yako yote ambayo yalikufanya urudi nyuma..Na Bwana atakusaidia kama alivyomsaidia Petro.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

AHADI YA ROHO ILIYOSALIA SASA KWA KIPINDI CHETU.

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

Je aliyezungumza na Musa kule jangwani ni Mungu mwenyewe au malaika wake?

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/06/22/ni-lazima-kuishikilia-imani-mpaka-mwisho/