by Admin | 2 July 2021 08:46 am07
Mhubiri mmoja maarufu huko India, siku moja alionyeshwa maono, anasema alipokuwa anakwenda katika ziara zake za kuhubiri katika kijiji kimoja, ilikuwa ni desturi yake kukutana na baadhi ya wenyewe wa maeneo hayo nyumbani kwao na kuzungumza nao, Sasa anasema alipokuwa anakaribia nyumbani kwa mwanamke mmoja aliyemfahamu, yule mwanamke alipomwona anaingia uwani mwake, akatoka jikoni moja kwa moja kwenda kukutana naye, na kabla hata hajamuamkia vizuri, muda huo huo alimwangukia magotini kwake, akaanza kulia. Wakati muhubiri huyu anafanya jitahada za kumwinua, amuulize shida yake, muda huo huo anasema alimwona Bwana Yesu amesimama pembeni yake, akimwangalia, kisha kitambo kidogo akamwona anamkaribia huyu mwanamke aliyekuwa Analia, akaenda kwenye shavu lake la kushoto, na kuweka mikono yake, na kukinga machozi yake, mpaka yalipojitengeneza kama kibwawa.
Na ghafla akamwona Bwana Yesu akipaa mbinguni, na yeye yupo naye, akafika sehemu nzuri sana, ambapo kwa mbele aliona kitu kama sanduku la agano limewekwa, kisha akamwona Bwana Yesu akiyamimina machozi ya yule mama juu ya sanduku lile la agano. Kisha akaanza kumwombea kwa Baba, kwa kuuugua sana na kwa machozi mengi.. Aliomba pale kwa kitambo, mpaka ikasikika sauti kama ya radi ikisema, AMESIKIWA. Anasema Hapo ndipo Bwana Yesu alipoacha kuomba. Akageuka akamwangalia huyu mhubiri, akamwambia mwambie binti yangu, maombi yake manne aliyokuwa anamwomba Mungu yamesikiwa.
Na dakika hiyo hiyo alijikuta amesimama karibu na yule mwanamke, kisha akamwinua na kumweleza alichoonyeshwa, yule mwanamke akaruka ruka kwa kuraha na kicheko kwa kujibiwa kule.
Kwanini, nimeandika ushuhuda huo, nikwasababu, biblia inasema machozi ya watakatifu yanathaminiwa sana na Mungu, jambo ambalo watakatifu wengi, pengine hawalijui, wanadhani kulia kwao ni bure, Si kweli, Mungu anayakusanya machozi yetu na kuyahifadhi katika chupa, biblia inasema hivyo;
Zaburi 56:8 “Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)
Umeona Machozi yetu kwa Bwana, yanatiwa katika chupa, kama vile divai nzuri inavyotunzwa katika viriba vipya. Na wakati huo huo bado yanaandikwa katika kitabu cha Mungu cha ukumbusho. Kaka/Dada Umekuwa ukilia kwasababu ya dhiki unazopitia kutokana na Imani yako, kumbuka kuwa Mungu anasikia, umekuwa ukilia kwasababu ya misiba iliyokukuta hivi karibuni Mungu anasikia, kwasababu ya magonjwa yasiyotibika, Mungu anasikia, Kwasababu ya injili Mungu anasikia na kuyatunza hayo machozi kama vile alivyoyatunza ya akina Paulo.
Matendo 20:19 “nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi;
20 ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba”,
Unapaswa ukumbuke kuwa huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo ya kutuombea haikuishia tu alipokuwa duniani, hapana, bali bado inaendelea hadi leo hii mbinguni, biblia inasema hivyo;
Waebrania 7:25 “Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee”.
Hivyo usiogope ni nini unapitia leo, wala usikate tamaa, kumbuka Yesu, faraja yetu yupo. zidi kumtumaini yeye na kumtegemea yeye, kwasababu daima yupo na wewe, kukusaidia, mkono wake hautakuacha kamwe.
Hakika sifa na heshima, na utukufu, ni kwa Bwana wetu YESU KRISTO milele na milele,
Amen.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/02/uyatie-machozi-yangu-katika-chupa-yako-ee-bwana/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.