BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

by Admin | 15 July 2021 08:46 am07

Huruma ni nguzo muhimu sana ambayo tunapaswa tuwe nayo sisi tuliompokea Kristo maishani mwetu.

Ni kwanini tuwe na huruma? Ni kwasababu Baba yetu naye ni mtu mwenye huruma.

Luka 6:36 “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma”.

Lakini wengi wetu bado hatujafahamu vema huruma hasaa ni nini. Kuna tofauti kati ya huruma na Rehema(wafilipi 2:1). Rehema ni neno pana linalomaanisha kusamehe au kusaidia hata kama mtu huyo hastahili kupewa fadhili hizo, lakini huruma ni kitendo cha kuonyesha kusamehe/kusaidia/kujali kwa mtu ambaye anaonekana anahitaji msaada huo hata kama hatosema,au kuonyesha.

Kwa mfano mwanajeshi vitani anapomkamata adui yake (ambaye ni mwanajeshi kama yeye). Na ikatokea adui huyo akajisalimisha kwa magoti akiomba asiuliwe,..Na yule mwanajeshi akamsaheme, kwa kuomba kule, basi hapo kaonyesha kitendo cha huruma.

Lakini ikitokea, Yule adui amekamatwa lakini bado analeta ubishi, bado ni mkaidi, anataka kuleta madhara, na wakati huo huo  Yule mwanajeshi bado akayahifadhi tu maisha yake..Hiyo sio huruma bali ni rehema.

Mfano mwingine wa rehema  ni pale raisi anapowaachilia wafungwa, sio kwamba wale watu walimwomba watoke, au wamejirekebisha kwa tabia zao mbaya, au ni wema sana hapana bali ni pengine raisi anatimiza tu wajibu wake wa kisheria kama raisi, wa kusamehe wafungwa kila muhula kwake.

Mfano mwingine wa huruma ni pale Baba anapomtimizia mtoto wake mahitaji yake ya chakula au mavazi,huwezi kusema anaonyesha kitendo cha rehema, hapana, bali huruma, kwasababu anajua sikuzote mtoto ni dhaifu, hana uwezo wa kujiamulia mambo yake mwenyewe.

Hivyo rehemu na huruma vyote vinahitajika sana kwetu. Lakini leo tutajikita sana katika upande wa huruma, na tayari tumeshapata  msingi wa maana halisi ya huruma, kwamba huwa unaenda moja kwa moja kwenye kundi la watu wanaoonyesha kuhitaji msaada fulani.  Basi biblia inatufundisha sisi kama wakristo, tuonyeshe huruma zetu, kwa makundi kama hayo; kwasababu Baba yetu wa mbinguni naye anaonyesha huruma zake kwetu sisi tunapomlilia, usiku na mchana.

Kibiblia ni makundi gani tunapaswa tuyaonyeshee huruma zetu?

1) HURUMA KWA WENYE MAGONJWA.

Utaona katika maandiko Bwana Yesu aliwaponya wagonjwa wengi sana kwasababu aliwahurumia, hakuwaacha tu waende zao,bali alijitahidi kuchukuliana nao, na kuwaponya.

Marko 1:40 “Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.

41 NAYE AKAMHURUMIA, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.

42 Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.

Unaona? nasi vivyo hivyo, tunapoona wengine wanataseka na magonjwa, wanaumwa, hatupaswi kuwaacha hivi hivi, tuwe nao karibu tuwaombee, tujiweke na sisi katika nafasi zao, Jiulize je! Kama na wewe ungekuwa unaumwa kansa, au kisukari, au ukimwi kama Yule, halafu unaona  watu hawakujali hata kukuombea, utajisikiaje?.

Tazama tena kisa hiki kingine..

Luka 7:12 “Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.

13 Bwana alipomwona ALIMWONEA HURUMA, akamwambia, Usilie.

14 Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka”.

2) HURUMA KWA WENYE UHITAJI.

Kuna wakati jirani yako atakuwa amepungukiwa na kitu fulani aidha  mboga kidogo,  au sabuni, au pesa kidogo za matumizi, na pengine hilo lipo ndani ya uwezo wako, hupaswi kumuacha tu hivi hivi, bali uonyeshe huruma zako, kwasababu hivyo ndivyo Mungu anataka..

1Yohana 3:17 “Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia HURUMA ZAKE, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?

18 Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli”.

3) HURUMA KWA WALIOKUMBWA NA MATATIZO:

Kuna muda ambao, mtu fulani atahitaji msaada wa haraka kutoka kwako, labda mgonjwa wake kazidiwa anaomba msaada wako,wa kumfikisha hospitali, na wewe pekee ndio upo hapo wa kuweza kumsaidia, wakati kama huo, usijione kuwa upo buzy sana, au unawahi ibadani, zingatia kumsaidia kwanza, kwasababu biblia inatufundisha hivyo kwa ule mfano wa msamaria mwema;

Luka 10:30 “Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.

31 Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.

32 Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.

33 Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona ALIMHURUMIA,

34 akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza”.

4) HURUMA KWA WAKRISTO WALIORUDI NYUMA:

Hapa ni mahali pengine ambapo tunapaswa kupazingatia sana. Kuna wakati ndugu mwenzako katika imani anaweza kurudi nyuma, pengine akauacha wokovu kabisa, lakini akawa anatamani kurudi tena kwa Mungu, wewe kama mkristo, ni lazima uonyeshe huruma zako kwa mtu kama huyo kumsaidia, tutalisoma hilo katika ule mfano wa mwana mpotevu, utaona baada ya kuasi nyumbani na maisha kuwa magumu huko alipokwenda alizingatia kurudi nyumbani. Na aliporudi alimwambia baba yake maneno haya;  Lakini utasoma babaye hakumfukuza bali alimuhurumia.

Luka 15:19 “sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.

20 Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, AKAMWONEA HURUMA, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.

21 Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.

22 Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;

23 mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi;

24 kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia”.

Vivyo hivyo na sisi tuwahurumie wale ambao wanarudi kwa moyo wa dhati kwa Mungu.

5) HURUMA KATIKATI YA WAAMINIO.

Vilevile sisi kama waaminio, tuliokoka, kanisa la Kristo, ni lazima tujue kuwa kila kiungo kinamuhitaji mwenzake, unapoona kiungo kimoja kimeumia, au kimefadhaika huna budi kukitibu, unapoona kimepungukiwa huna budi kukijali, kinapokukosea huna budi kikisamehe. Ndivyo Bwana anavyotaka.

Waefeso 4:32 “tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi”.

Bwana atusaidie tuyazingatie hayo, ili na sisi tufanane na Baba yetu wa mbinguni, ambaye anatuhurumia kila wakati.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UPENDO WA MUNGU.

JE! NI WAPI UTAPOKEA HISIA ZA KWELI ZA KI-MUNGU?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

SI KWA UWEZA WALA KWA NGUVU BALI KWA ROHO YANGU, ASEMA BWANA.

Kwa jina lake Ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa.

Je! Mfalme Abiya na Mfalme Asa walikuwa ni ndugu?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/15/basi-iweni-na-huruma-kama-baba-yenu-alivyo-na-huruma/