Nini maana ya Kuzumbua na kujitoja?

by Admin | 20 July 2021 08:46 pm07

Nini maana ya kuzumbua na kujitoja? Katika biblia.(Walawi 6:3, Kumbukumbu 14:1, )

Jibu: Neno kuzumbua tunalisoma katika kitabu cha Mambo ya Walawi 6:3, na tafsiri ya neno hilo ni “kukipata kitu”, pengine ambacho kilikuwa kimepotea, au kimehamishwa mahali pake..

Walawi 6:1“ Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

2 Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya Bwana, akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la kunyang’anya, au kumwonea mwenziwe;

3 AU KUZUMBUA kitu kilichopotea na kutenda la uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo

4 ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang’anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea ALICHOKIZUMBUA yeye,”

Na hakuna mahali pengine katika biblia neno hili limeonekana tena.

Vile vile neno “kujitoja” tunalisoma katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 14:1, ambalo maana yake ni “kujikata”.. Mtu anayejikata kwa wembe au kisu katika mwili wake maana yake amejitoja kwa kitu hicho.

Kumbukumbu la Torati 14:1 “Ninyi mmekuwa wana wa Bwana, Mungu wenu; MSIJITOJE miili yenu, wala msifanye upaa katikati ya macho yenu kwa ajili ya aliyekufa”

Hakuna mahali pengine popote neno hili limeonekana katika biblia.

Katika maneno hayo mawili tunajifunza kuwa Mungu hapendezwi na dhuluma, maana yake kama ndugu yako kapoteza kitu na wewe ukakipata! (maana yake ukakizumbua), unapaswa umrudishie mwenyewe kitu hicho, hupaswi kubaki nacho wewe na kukificha kana kwamba ni chako na kumdanganya Yule aliyekipoteza.. jambo hilo halimpendezi Mungu kabisa.

Vile vile, biblia haijaturuhusu sisi kuitoja miili yetu, maana yake kuikata kata, kipagani… kama mfano wa wale manabii wa baali kipindi cha Nabii Eliya, walivyojikata..

1Wafalme 18: 28 “Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika”.

Hata leo, watu wanajikata katika matambiko yao ya kimila, na hata katika kuchanjwa chale, na wengine katika kujichora alama(tattoo). Namna zote hizi za kujikata ni machukizo mbele za Mungu, Kwasababu miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, maana yake Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu, hivyo hatupaswi hata siku moja kufikiri kuiharibu nyumba yake hii.. kwasababu tukiiharibu na yeye amesema atatuharibu sisi. (1Wakoritho 3:17)

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

CHUKIZO LA UHARIBIFU

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

PALE UNAPOKUWA NA SABABU ZA KUMLAUMU MTU, UFANYE NINI?

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

Kwa jina lake Ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/20/nini-maana-ya-kuzumbua-na-kujitoja/