KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.

by Admin | 30 July 2021 08:46 pm07

Daudi ni mfalme ambaye alikuwa amezungukwa na mashujaa hodari sana, na mashujaa hao aliowachagua walikuwa wamegawanyika katika makundi makuu matatu, Kundi la kwanza kabisa ambalo lilikuwa ndio la juu kabisa zaidi ya yote liliundwa na maaskari watatu, na lile pili yake liliunda na wawili, na lile la tatu liliundwa na mashujaa 37.

Sasa ukitaka kujua kwa urefu ushujaa wao, na mashujaa wenyewe walikuwa ni wakina nani fungua link hii usome zaidi…

Lakini leo tutaona kwa ufupi, ni nini kilimtokea  mmojawapo kati ya wale mashujaa watatu wa kwanza, Na ni ujumbe gani Kristo anataka tuupate kupitia ushujaa wake.

shujaa huyu aliitwa Eleazari, yeye kuna wakati walikutana na jeshi kubwa la wafilisti, wakati huo alikuwa peke yake tu, Israeli yote ilikuwa imeondoka, hata wale mashujaa wenzake hawakuwepo.. Lakini hakuogopa vita bali alinyanyuka na kuushikilia upanga wake mmoja.. akaanza kupigana na wafilisti yeye peke yake kama vile Samsoni, aliushikilia upanga wake kwa nguvu sana kiasi kwamba haikuwa rahisi kuuondoa mkononi mwake.

Lakini kwasababu maadui walikuwa wengi,kuna muda ulifika alilemewa sana, na ile nguvu ya kuendelea kuushikilia upanga ikamwishia, akataka kuuachilia ule upanga kwasababu alichoka sana, lakini biblia inatuambia upanga ule hakuwezi kutoka katika mkono wake, ikiwa na maana ulijiganda kama gundi katika mkono wake. Pale alipojaribu kurusha mkono, upanga haukuchomoka mkononi mwake, bali ulikwenda naye Hivyo akaendelea kupigana na wafilisti mpaka akawamaliza wote. Baadaye Israeli walipokuja kazi yao ikawa ni kuteka nyara tu huko nyuma, kwa kipigo cha jeshi la mtu mmoja.

2Samweli 23:9 “Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;

10 huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu”.

Hiyo ni kuonyesha jinsi gani, mtu anapotaka kung’ang’ana na kusudi la Mungu, kusudi nalo litang’ang’ana naye, ili kutimiza lile lengo.

Leo hii ukiling’ang’ania kusudi la Bwana kwa moyo wako wote na kwa bidii, lile kusudi nalo litang’ang’ana na wewe tu, hamna namna, kwasababu hiyo ni kanuni ya ki-Mungu, hata kama utafikia wakati umechoka, bado litaendelea kukung’ang’ania tu. Na ndio maana unaona ni kwanini watumishi wa Mungu wa kweli, hawachoki kumtumikia Mungu, japokuwa hawafanyi kazi ya mshahara, sio kwamba hawachoki, au hawapitii magumu, au hawapungukiwi nguvu..wanachoka, lakini wakati wanakaribia kuanguka, lile kusudi la Mungu linang’ang’ana nao, hivyo wanajikuta bado wanaendelea mbele na safari.

Isaya 40:29 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.

30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;

31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia”.

Hata sisi sote, tunapodhamiria kweli kwa mioyo yetu yote, kutembea na Mungu, kamwe Mungu hawezi kutuachia katikati tuaibishwe na shetani, tunakuwa mfano wa Eleazari, nguvu za Mungu zitaambatana na sisi kuhakikisha kuwa lile kusudi la Mungu linatimia kwa gharama zozote zile.

Lakini tukiwa watu vuguvugu, leo tupo na Mungu kesho shetani, hatujajikana nafsi zetu na kusema kuanzia leo mambo ya ulimwengu basi, tunakwenda na Kristo. Kamwe nguvu ya Mungu haiwezi kushikamana na sisi kama alivyokusudia, pale tunapoishiwa nguvu au tunapokumbana na majaribu. Na ndio hapo utaona mkristo anakuwa moto na Mungu siku za mwanzoni mwanzoni, tu ikifika baadaye, anapoa, mpaka anauacha wokovu kabisa..ukimuuliza ni kwanini atasema, hali ya maisha ilikuwa ngumu, mwingine nilipitiwa na ujana, mwingine nilikuwa katika mazingira yasiyo rafiki,..Sasa tatizo halipo kwa Mungu bali kwa huyu mtu.

Kwasababu Mungu akishaianzisha safari ndani ya maisha ya mtu  huwa haikatishi katikati, Kwasababu Mungu huwa hashindwi , anaelewa kabisa kuwa yapo majira mbalimbali tutapitia hapa duniani kama wakristo, hivyo anatuhakikishia nguvu ya ziada kutoka kwake,  lakini hiyo inakuja  endapo tu tutakuwa na nia ile ile ya kutembea naye.

Paulo alisema

Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”

Hivyo ishi maisha ya kumaanisha mbele zake, ishi ndani ya kusudi la Mungu, ili Mungu awe nawe nyakati za taabu. Swali ni Je umemaanisha kweli kumfuata Kristo? Kama bado basi leo ndio wakati wako wa kudhamiria kutoka katika moyo wako kutubu na kuacha dhambi zako zote, Fanya hivyo kisha baada ya hapo nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ikiwa hukubatizwa hapo kabla, Na Mungu mwenyewe atakupa Roho wake Mtakatifu, akutie nguvu hadi siku ukombozi wako.

Zingatia: Waliokombolewa na Mungu hawashindwi na ulimwengu.

Ikiwa utapenda upate huduma ya ubatizo sahihi, basi utawasiliana na sisi kwa namba hizi 0693036618, tukusaidie.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo .jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

LIPO LA KUJIFUNZA KWA WALE MASHUJAA 37 WA DAUDI.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/07/30/kuna-nguvu-ya-ziaida-katika-kulingangania-kusudi-la-mungu/