NI NANI ATAKAYEUCHUKUA MSALABA WA YESU?

by Admin | 7 August 2021 08:46 pm08

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo, Ni siku nyingine tena tumepewa neema ya kuiona, hivyo nasi hatuna budi kutumia nafasi hiyo kujifunza maneno yake maadamu tumepewa nafasi hiyo.

Tukiwa hapa duniani ni lazima tujue kuwa upo ufalme ambao Bwana Yesu alienda kutuandalia huko mbinguni. Lakini kwa bahati mbaya ufalme huo hautakuwa wa watu wote, watakaopewa neema ya kuingia huko. Wengine watakuwa waalikwa tu, lakini hawatakuwa wafalme na makuhani, bali ni Bibi-arusi tu wa Kristo peke yake, na ndugu za mfalme ndio watakaokuwa na ufalme huko mbeleni. Soma (Mathayo 22:1-13)

Na hao Yesu alisema watakuwa ni watu   “waliodumu naye katika Majaribu yake”

Luka 22:28 “Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu.

29 Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi”.

Umeona, wale waliodumu naye katika majaribu yake tangu, kuzaliwa kwake, mpaka anaanza hudumu, na hadi kufa kwake. Na hao si wengine zaidi ya akina Mariamu, ma mitume na wengine baadhi waliomfuata Yesu kila mahali alipokwenda kama vile Mathiya. Na sisi tuliotokea kipindi hichi ambao tutashiriki kama wao hapa duniani kwasasa.

Sasa leo tutamwangalia mtu  mwingine mmoja, ambaye naye alishikiriki, kwa sehemu katika majaribu ya Yesu, na kwa kupitia yeye, tutajifunza na sisi tufanye nini ili, tuwe na nafasi katika ufalme huo mkuu sana. Na mtu mwenyewe si mwingine zaidi ya Simoni Mkirene.

Utakumbuka wakati ambao Bwana Yesu anakaribia kwenda kusulibiwa, baada ya kupigwa sana, kutemewa mate, kupigwa makofi, kuvikwa taji la miiba n.k., hali yake haikuwa nzuri kabisa. Biblia inasema aliharibiwa kuliko mtu yeyote duniani, hakuwa tena kama mwanadamu ukimtazama, kwa mapigo aliyoyapata (Isaya 52:14).

Lakini wale askari bado waliona hiyo haitoshi, wakamtwika msalaba wake, ili aubebe mpaka Goligotha, lakini alipojitahidi kuubeba mwendo kadhaa, hakuweza kutembea kabisa, mwendo wake ulikuwa ni mdogo sana, hakuwa na nguvu ya kuunyanyua msalaba kwasababu aliumizwa sana, Pengine wakawa wanampiga kwa mijeledi  kama punda, walau waone kama ataongeza mwendo, lakini hakukuwa na mwitikio wowote katika hilo, ni jinsi gani Bwana alivyochoka..

Hatimaye wakaona, atawacheleweshea tu muda, hivyo ikawabidi watafute njia mbadala. Hapo ndipo wakaangalia kulia na kushoto miongoni mwa watu waliokuwa pale, lakini hawakuona hata mmoja aliyeweza kuunyanyua msalaba ule. Tengeneza picha biblia inasema, kulikuwa na mkutano mkubwa sana wa watu waliokuwa wanamfuata Yesu kwa nyuma hiyo siku, lakini askari hawakuona hata mmoja miongoni mwao mwenye uwezo wa kuubeba msalaba wa Yesu. Wengi wao walikuwa ni watakazamaji tu, wengine walalamikaji, wengine wahurumiaji tu, hakuna hata mmoja aliyeweza kusogeza hata shingo yake, kuimsaidia Yesu.

Lakini kwa bahati nzuri kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa anatokea SHAMBA, ambaye hakuwa hata na habari za kusulibiwa kwa Yesu, lakini askari wakamwona huyo ndiye anayefaa, wakamkamata kwa lazima, wakamshurutisha aunyanyue ule msalaba mzito mabegani mwake mpaka Goligotha.

Luka 23:26 “Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.

27 Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea”.

Sasa jiulize ni kwanini awe ni huyu mtu aliyetoka SHAMBA na si wale wengine? Ni kwasababu askari walimwona ni mtu wa KAZI, aliyezoelea utumishi, mtu wa kupiga majembe, mtu wa kukata mashoka huko misituni, hivyo wakimkatama huyo amsaidie ili  safari ile ndefu ya msalaba mzito isiishe katikati bali itawafikisha Goligotha walipokusudia. Na kweli ikawa hivyo.

Jiulize tena kwa upande wa pili, Bwana Yesu alijisikiaje moyoni mwake kwa mtu kama huyu. Akiona katwikwa mzigo ule uzito asiostahili kuubeba, ni wazi kuwa moyo wake ulimhurumia, kwa kila jasho alilokuwa analitoa nyuma yake, wakipandisha kilima kile kirefu hadi Kalvari. Unategemea vipi mtu kama huyu asiwe sehemu ya Ufalme aliokwenda kuwaandalia watakatifu wake mbinguni. Ikiwa tu Yule mwizi pale msalabani hakufanya chochote chema, wala hakumsaidia Yesu kwa lolote lakini alipoomba tu aliambiwa usiku ya leo utakuwa pamoja nami peponi, Si zaidi kwa mtu kama huyu ambaye alikuwa sehemu ya majaribu ya Yesu Kristo duniani?

Marko 15:21 “Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.

22 Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa”.

Ni nini tunajifunza?

Bwana hawezi kutupa sehemu ya msalaba wake, ikiwa sisi si watu wa SHAMBA. Si watu wa kuzoelea  kazi ya Mungu, Kwasababu ataona kama tutaishia njiani, tukautupa msalaba wake tukakimbia, tusilitimize kusudi lake, kwasababu ni watu laini laini.

Kuwa mtu wa shamba ni pamoja na kuwa mtu wa kulitendea kazi Neno la Mungu, na sio kuwa msikiaji tu au msomaji tu. Kama wale makutano ambao walikuwa wanafuata tu kwa nyuma, lakini wasifanye chochote kwa ajili ya Kristo.

Kuwa mtu wa shamba ni pamoja na kujitoa kwa ajili ya Kazi ya Kristo, kwa vile vidogo ulivyojaliwa, kwa karama Mungu aliyoiweka ndani yako.

Kuwa mtu wa shamba ni pamoja na kujizoesha kuishi maisha ya Utauwa(1Timotheo 4:7-8). Yaani kuwa mwombaji, mfungaji, na mshuhudiaji wa habari njema.

Hapo ndipo Bwana ataona sababu ya kukupa wewe neema ya kuubeba msalaba wake. Na faida yake ni kuwa utakuwa sehemu ya ufalme huko mbinguni alipokwenda kutuandalia. Kwasababu ufalme huo ni kwa wale tu walioshiriki taabu yake wakiwa hapa duniani.

Hivyo sisi sote kuanzia sasa, tuwe wakakamavu rohoni, tuwe hodari kama Simoni, sio walegevu walegevu, wasikiaji tu lakini sio watekelezaji wa kile tunachokisikia, vitu vidogo vidogo tu vinatutoa katika mstari wa wokovu,  bali kila siku tutafute ni nini mapenzi ya Mungu.

Bwana akubariki sana, na nikutakie mafanikio mengi katika safari yako ya wokovu hapa duniani.

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HALI ZETU JINSI ZINAVYOWEZA KUATHIRI UTOAJI WETU.

nini maana ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba?

AINA TATU ZA WAKRISTO.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/07/ni-nani-atakayeuchukua-msalaba-wa-yesu/