JE CHANJO YA KORONA NI ALAMA YA MNYAMA?

by Admin | 11 August 2021 08:46 am08

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu, libarikiwe, karibu katika kujifunza maandiko.

Leo tutajifunza swali la msingi na la muhimu, linalozunguka katika vichwa vya watu wengi, walio wakristo na wasio wa kristo, na swali lenyewe ndio hili> Je chanjo ya Korona/corona ndio chapa ya mnyama yenyewe au ni kitu kingine?

Ili kupata jibu la swali hili vizuri, ni vyema kwanza kujua maana ya chapa na lengo la chapa!. Chapa maana yake ni lebo, au utambulisho. Kitu kilichotiwa chapa maana yake kimewekwa utambulisho wa hicho kitu, kwamfano bidhaa Fulani inayouzwa katika duka, ni lazima iwe na chapa au lebo, lengo la hiyo lebo/chapa ni kuitambulisha ile bidhaa Mmiliki wake pamoja na asili yake na vile vile ni nembo ya hati miliki ya wenye bidhaa.

Na kawaida chapa, au nembo ya bidhaa inawekwa mwishoni kabisa mwa bidhaa ile inapokamilika kutengenezwa, na huwa haiwekwagi mwanzoni mwa bidhaa ile inapotengenezwa.

Kadhalika, biblia imetabiri, kipindi kifupi sana kabla ya dunia kuisha, Shetani atawatia alama/nembo watu wake. Ili kwamba ithibitike kuwa wao ni milki yake ya halali, na hatua ya kutiwa chapa ni hatua ya mwisho kabisa ya uthibitisho wa mtu kwa shetani. Maana yake ni kwamba mpaka mtu aipokee chapa, tayari alikuwa katika kuandaliwa na shetani muda mrefu, hivyo sio jambo la kufumba na kufumbua tu.

Maana yake ni kwamba wote watakaoipokea chapa, ni sawa na mtu aliyemaliza kuiandika barua, anamalizia na sahihi tu pale chini!, ile sahihi ndio chapa!, lakini habari yenyewe sio ile sahihi bali ni ule ujumbe!.. kadhalika chapa!, ni sahihi tu ya uhalali wa mtu kwa shetani. Msingi huu utatusaidia kujua kuwa chapa ya mnyama sio jambo la kwanza kumtambulisha mtu kuwa ni milki ya shetani, bali ni jambo la mwisho!. Kwasababu kama ingekuwa ni jambo la kwanza, wapo watu waliokufa na hali hawana hiyo chapa ya mnyama na bado walikuwa ni milki ya shetani, na siku ya mwisho wataingia katika ziwa la moto!.  Hivyo jambo la kuogopa sasa sio hiyo chapa inayokuja ambayo ni 666, bali ni kujiupusha na shetani muda huu na kazi zake zote, kwa kumpokea Bwana Yesu, na kubatizwa katika ubatizo sahihi na kuishi maisha matakatifu.

Kwa kufanya hivyo utakuwa umejitoa kabisa kwenye mkondo wa watu wa Yule mwovu, na wanaotengenezwa kuwa wake, na mwisho kutiwa chapa yake.

Sasa tukirudi kwenye swali letu, linalouliza, Je! Chanjo ya Corona ni alama ya mnyama au ni kitu kingine?. Jibu ni kwamba chanjo ya corona sio chapa ya mnyama!.. Isipokuwa inatangaza ujio wa chapa ya mnyama.

Katika maandiko tunasoma kulikuwepo na matukio ambayo yalikuwa yanatangulia kutokea, ambayo yalikuwa yanatangaza ujio wa tukio Fulani kubwa mbeleni. Kwamfano utaona janga mafuriko ya gharika ya Nuhu, ambayo yalitokea duniani kutokana na maasi ya wanadamu, na janga lile likafuta idadi kubwa karibia yote ya watu duniani… Kwa janga lile kubwa ijapokuwa liliangamiza na kubakisha watu nane tu!.. Lakini bado mwisho wa dunia ulikuwa haujafika!.

Lakini tukio lile lilikuwa linatangaza au kuhubiri jinsi mwisho wa dunia utakavyokuwa… Kwamba siku moja kabla mwisho wa dunia kufika, siku hizo zitafanana sana na siku za Nuhu,.. maasi yataongezeka, na vile vile dunia itaharibiwa yote kwa moto (2Petro 3:6), kama ilivyoharibiwa kwa maji kipindi cha Nuhu.

Mathayo 24:37  “Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

38  Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,

39  wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu”

Vile vile hii chanjo ya korona sio chapa ya mnyama, bali inatangaza habari za chapa ya mnyama ambayo ipo mbioni kuja.. Kama vile gharika ya Nuhu inavyotangaza au kuhubiri gharika ya moto inatakayokuja mwisho wa dunia.

Kwahiyo tunaweza kuisema hii mithali na sisi “kama ilivyokuwa siku za chanjo ya Korona”.. “ndivyo itakavyokuwa siku za chapa ya mnyama”.. Kama ilivyokuwa siku za chanjo ya Korona, watu walikuwa hawawezi kusafiri sehemu baadhi, au kufanya shughuli Fulani bila kuwa na hiyo chanjo, ndivyo itakavyokuwa siku za ile chapa ya mnyama zitakapotimia.. katika siku hizo watu hawataweza kununua wala kuuza, wala kufanya biashara yoyote bila kuwa na chapa hiyo ya mnyama katika vipaji vya nyuso zao na katika mikono yao ya kuume.

Kwahiyo Chanjo ya Korona, wala ugonjwa wa korona sio chapa ya mnyama.

Sasa unaweza kuuliza ni kwanini isiwe chapa ya mnyama?. Maandiko yametupa majibu yote jinsi chapa ya mnyama itakavyokuwa na itakavyotenda kazi. Hivyo tukitumia maandiko tunaweza kupata majibu yote na kutusaidia kutoyumbishwa na upepo wowote wa elimu unaokuja mbele yetu sawa sawa na Waefeso 4: 14…

Waefeso 4: 14 “ ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu” (www wingulamashahidi org)

Sasa mambo  yafuatayo ndiyo yatakayoitambulisha Chapa ya Mnyama.

  1. Chapa ya mnyama itaanza kufanya kazi baada ya kanisa kunyakuliwa na si kabla:

Hili ni jambo la kwanza ambalo kila mkristo anapaswa alifahamu. Chapa ya mnyama haiwezi kufanya kazi kabla ya kanisa la Kristo kunyakuliwa. Baada ya watakatifu kuondolewa duniani kwa tendo maarufu lijulikanalo kama unyako, ndipo chapa ya mnyama itakapoanza kutenda kazi..

Na sasa (wakati huu tunaoishi) kanisa bado halijanyakuliwa, watakatifu bado wapo duniani. Na maandiko yanasema kanisa la Kristo ndilo linaloizuia ile siku isifike, kwasababu ndilo lenye Roho Mtakatifu.. Hivyo siku litakapoondolewa ndipo yule mpinga-kristo atanyanyuka na kuihimiza chapa yake..

2Wathesalonike 2:5  “Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6  Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7  Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. 8  Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake”

  1. Chapa ya mnyama itaanza kutenda kazi baada ya Mpinga-Kristo kunyanyuka:

Hili ni jambo la  pili ambalo kila mkristo anapaswa alifahamu….

Huyu mpinga-Kristo biblia inamtaja kama ASI, au MWANA WA UHARIBIFU.

Maandiko yanasema hivyo katika kitabu cha…

2Wathesalonike 2:3  “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; AKAFUNULIWA YULE MTU WA KUASI, MWANA WA UHARIBIFU;

4  yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.

5  Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6  Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake”.

Na mpaka sasa ofisi atakayotokea Mpinga-kristo imeshajulikana (ni ofisi ya kipapa, kulingana na maandiko), lakini kwamba ni papa yupi, bado haijajulikana.. Na wakati chapa ya mnyama inazinduliwa duniani kote, biblia inasema mpinga kristo atakuwa ameshapata nguvu duniani kote, na kupewa nguvu na mataifa yote, na ndiye atakayeiratibu na kuihimiza, na vile vile atakuwa ameshajiweka tayari kutaka kuabudiwa kama Mungu. Jambo ambalo mpaka sasa halijatimia…ingawa lipo mbioni sana kutimia baada ya unyakuo wa kanisa kupita.

  1. Dhiki kuu itakuwa ni miaka mitatu na nusu.

Hili ni jambo la tatu na la muhimu pia kila mkristo kufahamu. Dhiki kuu ya mpinga Kristo itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu, yaani miezi 42 (Ufunuo 13:5). Na tendo la watu kulazimishwa kuipokea chapa, litakuwa ni tendo la haraka sana na lenye kuchukua muda mfupi, ili kuiruhusu ile dhiki kwa miaka mitatu na nusu. Maana yake ni kwamba wakati chapa inazinduliwa, kitakuwa ni kitendo cha muda mfupi na cha shinikizo kubwa sana..haitachukua miaka au mwezi, kukamilisha zoezi hilo.. kama sasa inavyofanyika katika chanjo.

Sasa hebu jiulize, tangu huu ugonjwa wa Korona umetokea ni miaka mingapi imepita?.. Na tangu chanjo ziache kutolewa ni muda gani umepita?, na mpaka zoezi hili limalizike kwa watu wote, maana yake kila mtu awe amechagua kupokea au kutokupokea itachukua muda gani?, huoni  ni jambo ambalo litachukua muda mrefu sana, pengine hata linaweza kuchukua miaka zaidi ya miaka miwili au mitatu mbeleni au hata zaidi ya hapo?..Sasa endapo likichukua miaka miwili mbeleni muda wa dhiki kuu utapatikana wapi?, muda wa vile vitasa saba vya ufunuo 16 utapatikana wapi?.

Umeona?.. kwahiyo hii chanjo sio chapa ya mnyama?.. chapa ya mnyama itakapoanza kufanya kazi itakuwa ni kipindi kifupi sana, kila mtu duniani ambaye hakwenda kwenye unyakuo atakuwa ameshachagua aidha kuipokea au kutoipokea, pengine zoezi hilo litaendeshwa chini ya mwezi mmoja tu!.. ili kuruhusu muda wa dhiki kuu ya miaka mitatu na nusu kwa wale ambao wataikataa. (tembelea www wingulamashahidi org)

  1. Chapa itasimamia sana Masuala ya kiimani:

Hili ni jambo la Nne na la mwisho ambalo kila mkristo anapaswa alifahamu. Chapa haitaletwa duniani kutokana na matatizo ya kiafya wala kiuchumi. Hapana!… Sababu kubwa ya chapa ya mnyama italetwa kutokana na masuala ya kiimani.. Yaani kile watu wanachokiamini na kukiabudu!… (Hicho ndicho kiini cha ile chapa).

Maana yake ni kwamba kipindi kifupi sana kabla ya chapa hiyo kuzinduliwa, shetani atanyanyua majanga na matatizo mengi ambayo yatakuwa yanasababishwa na imani za watu, vikundi kama vya kigaidi kama ISIS, BOKOHARAM, ANTI-BALAKA, ALQAEDA, ALSHABAAB n.k vitanyanyuka kwa kasi na kuleta shida kubwa sana duniani kote..vile vile manabii wengi wa uongo wataleta shida kubwa sana duniani kwa kufanya vitu vya ajabu na vyenye kutishia amani ya dunia.

Kutokana na hilo basi, dunia itatafuta mtu mmoja na taasisi moja maarufu ambayo inaweza kutoa mashauri na hata kutatua hayo matatizo, ndipo hapo atatafutwa mtu wa kidini mwenye ushawishi mkubwa kuliko wote, na mwenye nguvu kiusemi. Na huyo dunia nzima itamwamini na kumpa nguvu. Kiongozi huyo wa juu sana wa kidini, ndipo atakuja na wazo la namna ya kushughulikia kutatua matatizo hayo ya kiimani, ndipo atatoa wazo la kila mtu kusajiliwa katika Kanisa, au msikiti, au taasisi yoyote ambayo ipo chini ya mfumo wake huo. (www wingulamashahidi org)

 Na yeyote ambaye atakosa au kuukataa huo utambulisho basi hataweza kuuza wala kununua wala kufanya shughuli yoyote, na zaidi ya yote ndiye atakayeonekana anachafua amani ya dunia. Na hivyo atakamatwa kwa kipindi kifupi sana na kupelekwa katika magereza maalumu, ambapo huko atapitia dhiki ambayo biblia inasema haijawahi kuwepo wala haitakuwepo baada ya hapo, kwa muda  wa miaka mitatu na nusu na ndipo atakufa… Wakati wengine waliosalia ambao wameipokea chapa ya mnyama, wakingoja kuingia katika mapigo ya vitasa saba (tunayoyasoma katika Ufunuo 16). Kumbuka haya yote yatatokea baada ya kanisa kunyakuliwa juu mbinguni.

Huu ni mhutasari tu wa Chapa ya Mnyama jinsi utakavyokuwa, kwa maelezo marefu juu ya chapa hii ya mnyama, unaweza kuwasiliana nasi inbox kwa namba hizi 0693036618/0789001312. (www wingulamashahidi org)

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba chanjo ya korona si chapa ya mnyama, lakini inatangaza ujio wa chapa ya mnyama. Na ugonjwa wa Korona haujatengenezwa na wanadamu, bali ni Tauni kutoka kwa Mungu (sawasawa na Luka 21:11), ambapo ugonjwa huu ni dalili mojawapo kubwa sana ya kurudi kwa Kristo.

Dalili zote za kurudi kwa Yesu zimeshatimia… unyakuo upo karibu sana, je! Umempokea Yesu?..kwa kutubu dhambi zako zote na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu?, kama bado kumbuka kuwa unyakuo utakapopita, utaachwa, na hutaachwa kwasababu unachapa ya mnyama, hapana utaachwa kwasababu tayari wewe ni wa Yule mwovu hata bila chapa!,.. Chapa itakuwa ni muhuri tu wa kuhitimisha kwamba wewe ni milki ya shetani.. Hivyo si wakati wa kuifikiri chapa na kuiogopa!, kitu cha kuogopa sasa ni dhambi..Hicho ndio cha kuogopa na kukikimbia, na kwa nguvu zetu hatuwezi kuikwepa wala kuishinda dhambi bali kwa kumpokea na kumwamini Yesu.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

CHAPA YA MNYAMA

Kwanini Bwana aliwalenga mbwa na nguruwe tu katika Mathayo 7:6?

Je! Ni dhambi kumpiga au kumuua mnyama bila sababu yoyote?

UFUNUO: Mlango wa 18

YONA: Mlango 1

Jiepushe na tamaa ya Mali/kupenda fedha.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/08/11/je-chanjo-ya-korona-ni-alama-ya-mnyama/