KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

by Admin | 2 September 2021 08:46 am09

Jina la Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.. Maandiko yanasema..

Ezekieli 14:13 “Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuipelekea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama;

14 WAJAPOKUWA WATU HAWA WATATU, NUHU, NA DANIELI, NA AYUBU, kuwamo ndani yake, WANGEJIOKOA NAFSI ZAO WENYEWE TU KWA HAKI YAO, asema Bwana MUNGU”.

Hapo maandiko yamewataja watu watatu tu! Nuhu, Danieli pamoja na Ayubu. Unaweza kujiuliza ina maana ni hao tu ndio waliokuwa na haki kuliko manabii wengine wote na watakatifu wengine wote walioandikwa kwenye biblia (Agano la kale)?. Jibu ni la!..

Watakatifu wote wa kwenye biblia walikuwa na haki mbele za Mungu, na walimpendeza Mungu katika nafasi zao.. Lakini kulikuwa na jambo la kipekee katika hawa watu watatu, lililowafanya mpaka Bwana Mungu awataje hapa.. tutaenda kulitazama jambo hilo, ambapo litatusaidia na sisi kuenenda vyema katika ukristo wetu.

Sasa ili tuweze kuweka msingi wa kuelewa tabia waliyokuwa nayo hawa watu watatu, hebu tusome tena, maandiko mistari inayofuata ya mbele kidogo..

Ezekieli 14:19 “Au nikipeleka tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama;

20 wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, HAWATAOKOA WANA WALA BINTI; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao”.

Nataka tuone huo mstari wa 20, unaosema.. “Hawataokoa wana wala binti”. Maana yake ni kwamba watu hawa walikuwa wana tabia ya KUWAOKOA WATU NA GHADHABU YA MUNGU,  yaani Mungu alipotaka kuwaadhibu watu wote, hawa walisimama kuwaombea watu wao, au familia zao au wana wao, kitu kilichomfanya Mungu aghairi hasira yake kwa wale waliowaombea.

Kwa mfano utaona Nuhu, Mungu alipotaka kuigharikisha dunia, maandiko yanasema alionekana Nuhu peke yake ndiye mwenye haki,  wengine wote ikiwemo familia yake walikuwa miongoni mwa watu waliostahili adhabu ya gharika…. Lakini Nuhu alimwomba kwa ajili ya familia yake, na Mungu akamwambia atengeneze safina, sasa lengo la kutengeneza ile safina sio kujiokoa yeye peke yake bali yeye na nyumba yake, maandiko yanasema hivyo..

Waebrania 11:7 “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, ALIUNDA SAFINA, APATE KUOKOA NYUMBA YAKE. Na hivyo akauhukumu makosa ulimwengu, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani”.

Hapo biblia inasema aliunda safina “APATE KUIOKOA NYUMBA YAKE”.. maana yake apate kuwaokoa wana wake na mke wake!.. Hivyo kitendo cha watoto wake kupata neema ya kuokoka ilikuwa ni kwasababu ya Nuhu Baba yao.

Vile vile tunamwona mtu kama Ayubu. Huyu naye alikuwa ni mtu wa kipekee sana, kwani kabla ya mambo yote alikuwa akiwaombea rehema watoto wake kwa Mungu kila siku.

Ayubu 1:4 “Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao.

5 Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, YUMKINI KWAMBA HAWA WANANGU WAMEFANYA DHAMBI, NA KUMKUFURU MUNGU MIOYONI MWAO. NDIVYO ALIVYOFANYA AYUBU SIKUZOTE”.

Umeona tabia ya Ayubu?.. alikuwa ni mtu wa kuiombea nyumba yake rehema.. Inapokuja hatari hakutaka aokoke peke yake..alitaka kuokoka na familia yake..

Na mtu wa mwisho tunayeweza kumtazama ni Nabii Danieli, huyu maandiko hayajasema kama alioa au hakuoa!.. Lakini tabia ile ile ya kuwajali watu wa jamii yake, hata kuwaombea kwa Mungu, ndiyo iliyokuwa ndani yake..mpaka Mungu akaghairi mabaya juu ya watu wake Israeli kutokana na maombi ya Danieli. Na maandiko yanamtaja Danieli kama mtu aliyependwa sana na Mungu!..

Danieli 9:20 “Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, NA DHAMBI YA WATU WANGU ISRAELI, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu;

21 naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni.

22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danielii, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.

23 Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe UNAPENDWA SANA; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya.

24 Muda wa majuma sabini UMEAMRIWA JUU YA WATU WAKO, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu”.

Kama ukisoma sala hiyo kuanzia juu kidogo (mstari wa kwanza), utaona jinsi Danieli alivyokuwa akiomba dua kwaajili ya watu wake(Yaani waisraeli wenzake walio katika hali ya utumwa huko Babeli). Na alipomaliza kuomba kwaajili yake na Watu wake, hapo katika mstari wa 24, maandiko yanasema Malaika Gabrieli alimjia na kumpa maneno ya faraja juu ya WATU WAKE ANAOWAOMBEA , ili kukomesha makosa, kuishiliza dhambi na kufanya upatatisho n.k

Ni jambo gani tunajifunza kwa watu hawa watatu?

Jambo kuu tunaloweza kujifunza kutoka kwa hawa watatu ni ile hali ya kujali wengine!… Wanaona itawafaidia nini wao kupata raha na kuokoka, na ilihali familia zao zinapotea?, ndugu zao wanapotea?..!.. wakaona hawana budi kutafuta njia yoyote ya watu wao kuwaokoa ndugu zao, haijalishi wanaonekana bado ni waovu mbele za Mungu!.. Ndio maana unaona Nuhu alijenga safina na akapona na wanawe watatu!, kadhalika Ayubu alikuwa anawaombea wanawe kila siku kwa kuwatolea dhabihu, kwasababu alihisi pengine wanawe wanaweza kuwa wamemuudhi Bwana mahali fulani katika maisha yao, hivyo aliuchukua mzigo wao.

Na wa mwisho ni Danieli, aliona hana sababu ya yeye kujifurahisha kwenye nyumba ya kifalme na ilihali watu wake wapo katika hali ya kukataliwa na Mungu, hivyo akachukua jukumu la kufunga na kuomba kwaajili ya watu wake.

Ndugu tabia ya kujali uzima wa wengine, inaweza kudharaulika leo lakini ni jambo la heshima kubwa sana mbele za Mungu, Mungu ameweka kumbumbu la hawa watatu zaidi ya manabii wengine wote kutokana na tabia yao hiyo, kwa tabia hiyo ndio iliyomfanya Bwana awatukuze watu hawa watatu zaidi ya wengine wote.

Inawezekana leo umempokea Yesu, lakini ndani ya moyo wako, huna mzigo wa wengine kuwa kama wewe!.. Ni jambo baya sana…Inawezekana umeokoka, lakini moyoni mwako huna mzigo na Baba yako au mama yako ambaye bado hajaokoka kama wewe, Au huna mzigo na rafiki yako au ndugu yako ambaye bado yupo katika ulimwengu, au unaserebuka mtu fulani anapokufa bila kuokoka!

Fahamu kuwa tuna wajibu wa kuokoka sisi na vile vile kuwafikishia wengine wokovu.. kama sisi tulivyoupokea..ni lazima tuwe sababu ya wokovu kwa watu wengine..Ndivyo tutakavyompendeza Bwana na kukaa katika kumbukumbu lake daima.

Bwana atujalie tuweze kuyatenda mapenzi yake.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

KWANINI MIMI?

Neno “Via” linamaanisha nini katika biblia?

Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/09/02/kwanini-ni-nuhu-ayubu-na-danieli/