Kwanini wakristo walipomuona Petro akigonga walisema “Ni malaika wake”?

by Admin | 10 September 2021 08:46 am09

SWALI: Kwanini wakristo wa kwanza waliposikia kuwa Petro kafunguliwa hawakuamini badala yake walitumia neno “Ni malaika wake”..kwanini wawaze vile au waseme vile?


JIBU: Tusome.

Matendo ya Mitume 12:11-17

[11]Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.

[12]Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba.

[13]Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza.

[14]Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango.

[15]Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. WAKANENA,  NI MALAIKA WAKE.

[16]Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.

[17]Naye akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza. Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali pengine.

Wayahudi tangu zamani hadi sasa wanaamini kuwa kila mtu anaye malaika mlinzi..Na malaika hawa wanaweza kuja katika maumbile tofauti tofauti..wanaweza kuja kwa sura ya mtu mwingine au kwa sura au sauti  ya yule mtu anayemlinda.

Vilevile tunaweza kulithibitisha hilo pia katika maneno ya Bwana aliyoyasema katika (Mathayo 18:10) Kwamba wapo malaika wanaosimama kwa ajili ya watu tangu wakiwa wadogo.

Sasa kulingana na hiyo habari ni kuwa Roda aliposikia sauti ya Petro, .hakuhangaika kuhakikisha kwamba yeye anayegonga ni Petro au la! bali aliamini moja kwa moja na kwenda kutoa taarifa ..Lakini alipowapelekea habari wale waliokuwa ndani haikuwa rahisi kwao kuamini moja kwa moja kama yule angeweza kuwa Petro. Kwasababu kutokana na mazingira Petro aliyofungiwa, ni ngumu kutoka kwani alikamatwa kwa amri ya mfalme, na vilevile alikuwa chini askari 16.

Hivyo jambo ambalo wangeweza kudhani ni kuwa malaika wake ndio amekuja kwa maumbile ya Petro au pengine kwa umbile lingine isipokuwa katumia sauti ya Petro labda kuwafariji au kuwapa taarifa juu ya kifo  chake.

Lakini  walipoona Petro anazidi kugonga mlango wakaenda kumfungulia, wakathibitisha kuwa kumbe alikuwa ni Petro na sio malaika wake.

Ni nini tunaweza kujifunza katika habari hiyo?

Ni karama ya Mungu kuwatuma malaika zake kutuhudumia.Lakini malaika hawa hawamuhudumii kila mtu tu ilimradi hapana bali ni watakatifu tu..ikiwa na maana kama wewe ni mwovu ujue kinachokulinda ni rehema za Mungu tu ili uendelee kuishi, lakini hakuna huduma yoyote unayoweza kupokea kutoka kwa malaika zake. Kinyume chake ni kuwa mapepo ndio walinzi wako.

Na ndio maana huwezi kuishi maisha ya raha au ya amani hata kama unazopesa zote ulimwenguni..ni kwasababu ufalme wa Mungu haupo wala hautembei pamoja na wewe. Ni heri ukatubu leo ukamkabidhi Yesu maisha yako. Naye atakuokoa na kuuleta ufalme wake wa mbinguni kutembea pamoja na wewe. Hapo ndipo utakapoona tofauti yako ya jana ambayo hukuokoka na leo ambayo umeokoka.

Na wokovu unakuja kwanza kwa kutubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha na pili ni kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo na kupokea Roho Mtakatifu.

Hivyo kama utapenda kumpokea Kristo leo basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi kwa msaada huo wa kiroho bure. Kumbuka saa ya wokovu ni sasa na wakati uliokubalika ni leo.

+255693036618/ +255789001312

Bwana akubariki

Mada Nyinginezo 

HUDUMU YA MALAIKA WATAKATIFU.

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

TUSIRUHUSU MAMBO YA KUSUBIRISHA, YAVURUGE MUDA WETU NA MUNGU.

Mafundisho

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/09/10/kwanini-wakristo-walipomuona-petro-walisema-ni-malaika-wake/