Kwanini hatuirithi neema kama tunavyoirithi dhambi?

by Admin | 20 December 2021 08:46 pm12

Kristo atukuzwe! Kama dhambi ilikuja kupitia mtu mmoja (Adamu), na kila aliyezaliwa ameirithi, kwanini Neema iliyoletwa na Bwana Yesu hatujairithi, yaani wote wanaozaliwa wasiwe na dhambi?


Jibu: Ni kweli maandiko yanasema katika Warumi 5:12-21, Kwamba kwa kupitia mtu mmoja Adamu dhambi iliingia, na hivyo na sisi uzao wake wote tukaingia katika hali ya kukosa (yaani tukazaliwa huku tumerithi dhambi)..

Lakini swali ni je kwanini haipo hivyo kwa Bwana, kama yeye anafananishwa na Adamu wa pili, kwanini na sisi tusizaliwe hali tumeirithi hiyo neema bila kupitia hatua nyingine hizo za wokovu?.

Jibu ni kwamba, hatujairithi Neema kwa namna ya kimwili kwasababu Bwana Yesu hajatuzaa katika mwili kama Adamu alivyotuzaa sisi katika mwili.

Endapo Bwana angetuzaa upya watu wote katika mwili, kama vile Adamu alivyotuzaa kupitia Hawa, basi na sisi tungeirithi hiyo neema kwa njia ya mwili na kungekuwa hakuna haja ya kupitia hizo hatua za wokovu.

Lakini kwasababu Bwana hakuwa na mke, na wala hajazaa kwa namna ya mwili, kwasababu kama angekuja kwa njia hiyo ya kuzaa katika mwili basi wangezaliwa wanadamu wengine ambao ni uzao wa Bwana ulio mkamilifu kama Bwana, na hivyo sisi wengine ambao ni uzao wa Adamu ambao tumekwishazaliwa tayari tungekuwa bado tupo kwenye dhambi..na hapo kungekuwa hakuna wokovu.

Lakini ashukuriwe Mungu, Kristo hakuja kuleta uzao mwingine duniani bali kuukomboa ule ambao tayari upo, (yaani sisi tulio uzao wa Adamu).

Hivyo ni lazima Bwana aje na mpango mwingine wa kutuzaa katika roho na si katika mwili, ili tuwe uzao wake katika roho, na tuzirithi ahadi zake hizo katika roho..Ndio maana Bwana Yesu alisema hatuna budi kuzaliwa mara ya pili katika Roho.

Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.

Umeona hapo?

Na tunazaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho, yaani kwa Ubatizo wa maji na Kwa Ubatizo wa Roho Mtakatifu.

Maana yake ni kwamba mtu aliyebatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu (Matendo 2:38, Yohana 3:23), na akapokea Roho Mtakatifu anakuwa tayari amezaliwa mara ya pili, na hivyo ni mzao wa Bwana Yesu katika Roho. (Na tayari kapata ukombozi wa roho yake).

Ukombozi wa miili yetu utakuja siku ile ya unyakuo itakapofika (Waefeso 4:30), wakati parapanda itakapolia tutakapovikwa miili mipya ya utukufu isiyo na kasoro.

Swali ni je!. Mimi na wewe tumezaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho, kumbuka Bwana anasema mtu asiyezaliwa mara ya pili hawezi kuurithi uzima wa milele.

Maran atha!.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Noeli ni nini, na je! Neno hili linapatikana katika biblia?

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

JE! USIPOTIMIZA NADHIRI ZAKO ZOTE KWA BWANA. HAWEZI KUKUSAMEHE?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/12/20/kwanini-hatuirithi-neema-kama-tunavyoirithi-dhambi/