TUZIDI KUWA HODARI KATIKA BWANA.

by Admin | 26 December 2021 08:46 pm12

Shalom.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia..

Maandiko yanasema.

Waefeso 6:10 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake”.

Biblia inatufundisha kuwa mahodari katika Bwana na vile vile katika Uweza wa Nguvu zake.

Hapo kuna vitu viwili, 1). Kuwa Hodari katika Bwana. 2) Kuwa hodari katika uweza wa nguvu zake.

1) Kuwa hodari katika Bwana ni kupi?.

Kuwa Hodari katika Bwana ni katika kumtafuta yeye; yaani, kujituma katika kuutafuta uso wake.

Marko 12:30 “nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.

2) Kuwa hodari katika uweza wa nguvu zake.

Kuwa hodari katika uweza wa nguvu zake ni kuwa na uwezo wa kuzitumia zile silaha za roho ambazo tunazisoma katika mistari inayofuata.

Tusome,

Waefeso 6:10 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu”.

Biblia inatuasa tuwe hodari, tusiwe walegevu, kwasababu uweza wa Mungu unadhihirika katika uhodari wetu katika kuzitumia silaha hizo za roho.

Na silaha hizo ndio hizo zilizotajwa hapo ambazo ni Chepeo ya wokovu, Dirii ya Haki, Upanga wa Roho, Utayari miguuni, Kweli kiunoni na ngao ya Imani.

Askari ambaye si hodari ni yule ambaye anazo silaha lakini hana ujuzi au utaalamu wa kutosha wa kuzitumia.

Askari aliyeshika upanga halafu hana ujuzi wa kutosha namna ya kuutumia, adui akija atamdhuru pamoja na silaha yake.

Kadhalika na sisi tunapoushikilia upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu, na tukawa hatujui namna ya kulitumia inavyopaswa, adui yetu shetani anaweza kutudhuru kirahisi au kutupokonya upanga huo na kutudhuru nao.

Ndio maana utaona Bwana alipokuwa kule jangwani, shetani alipomjia kumjaribu kupitia Neno la Mungu, Bwana alikuwa ni hodari katika kulitumia Neno, hivyo alimjibu shetani kwa kumwambia “tena imeandikwa”.

Au kama Apolo alivyokuwa hodari katika maandiko.

Matendo 18:24 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko”.

Hivyo biblia inatuasa tuwe na ujuzi wa kulitumia kihalali Neno la Mungu.

2 Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli”.

Je wewe ni hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake?.

Je umejivika silaha za wokovu, na kuweza kusimama, na kuzipinga hila za shetani.

1 Wakorintho 16:13 “Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari”.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

JE! HAMPOTEI KWA SABABU HII?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2021/12/26/tuzidi-kuwa-hodari-katika-bwana/