Maji ya Farakano ni nini katika biblia?

by Admin | 31 January 2022 08:46 pm01

Kama jina lake lilivyo “Maji ya Farakano”…maana yake ni maji yanayoondoa mafarakano.

Mtu yeyote katika Israeli ambaye alikuwa amejitia unajisi kwa kugusa maiti ya mtu, alikuwa amejifarakanisha na Mungu, hivyo hana budi kujitakasa, ili akubalike mbele za Mungu.

Na kitu pekee kilichokuwa kinaweza kumtakasa ni maji hayo maalumu, yaliyojulikana kama MAJI YA FARAKANO.

Maji hayo yalikuwa yanatengenezwa kwa majivu ya Ng’ombe mwekundu, ambaye hajazaa bado, wala hajatiwa nira, wala hajakamuliwa maziwa.

Ng’ombe huyu alikuwa ni maalumu kwa ajili ya upatanisho Wa dhambi za wana wa Israeli.

Baada ya kuchinjwa na kuteketezwa, majivu yake yalihifadhiwa na kuchanganywa na maji safi, sasa maji hayo ya majivu ya huyo ng’ombe ndio yaliyoitwa maji ya Farakano.

Endapo mtu yeyote atagusa maiti basi atajitakasa kwa kunyunyiziwa maji hayo ya farakano na atakuwa safi. Na mtu yeyote asiyejitakaswa na maji hayo sheria ilikuwa ni kuuawa.

Hesabu 19:1 “BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2 Hii ndiyo amri ya sheria BWANA aliyoagiza, akisema, Waambie wana wa Israeli wakuletee ng’ombe mke mwekundu asiye na kipaku, mkamilifu, ambaye hajatiwa nira bado;

3 nanyi mtamleta kwa Eleazari kuhani, naye atakwenda naye nje ya kambi, na mtu mmoja atamchinja mbele yake;

4 kisha Eleazari kuhani atatwaa katika damu yake kwa kidole chake, na kuinyunyiza damu yake kuelekea upande wa mbele wa hema ya kukutania mara saba;

5 kisha mtu mmoja atamchoma moto huyo ng’ombe mbele yake; ngozi yake, na nyama yake, na damu yake, pamoja na mavi yake pia atachoma moto;

6 kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng’ombe.

7 Ndipo kuhani atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, kisha baadaye ataingia kambini, naye kuhani atakuwa najisi hata jioni.

8 Na huyo aliyemchoma moto ng’ombe atazifua nguo zake majini, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

9 Kisha mtu mmoja aliye safi atayazoa majivu ya huyo ng’ombe, na kuyaweka yawe akiba katika mahali safi nje ya kambi, nayo yatatunzwa kwa ajili ya mkutano wa wana wa israeli, kuwa ndiyo maji ya farakano; ni sadaka ya dhambi.

10 Na yeye ayazoaye majivu ya huyo ng’ombe atazifua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; na jambo hili litakuwa amri ya milele, kwa wana wa Israeli, na wa mgeni akaaye kati yao.

11 Mtu agusaye maiti ye yote atakuwa najisi muda wa siku saba;

12 naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi.

13 Mtu awaye yote agusaye maiti wa mtu aliyekufa, asijitakase, yuatia unajisi maskani ya BWANA; na mtu huyo atakatiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ukali juu yake bado”.

Lakini katika agano jipya hatuna sheria hiyo, kwamba tukigusa maiti tunakuwa najisi mpaka tunyinyuziwe maji hayo.

Unajisi katika agano jipya sio kushika maiti, wala si kula bila kunawa, si kukaa bila kuoga, wala si kuingia kanisani bila kutawadha..ni vizuri kufanya hayo kwa lengo la usafi tu!, Lakini haitusogezi karibu na Mungu n.k.

Bali unajisi hasa ambao unatuweka mbali na Mungu ni kutoa maneno machafu mdomoni mwetu, na kuwaza mabaya moyoni mwetu.

Marko 7:15,18-23 “Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu…..

18 Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi;

19 kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote.

20 Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.

21 Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati,

22 wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.

23 Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi”

Mambo haya ndio yanayotufarakanisha sisi na Mungu na kutufanya kuwa najisi mbele zake.

Na unajisi huo hautakaswi kwa Maji ya Farakano, bali kwa Neno la Mungu.

Waefeso 5:25 “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;

26 ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;

27 apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa”.

Na neno la Mungu, ambalo ndio maji yatutakasayo linasema..

Matendo ya Mitume 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Hilo ndilo Neno la Mungu litusafishalo na kutuondolea UNAJISI WOTE!. Na ndio maji yetu ya Farakano katika agano jipya.

Je umetubu na kubatizwa kwa jina lake Yesu Kristo?..Je umepokea Roho Mtakatifu?..Kama bado unangoja nini?.

Hizi ni siku za mwisho na Bwana yu karibu kurudi, na walio najisi wote hawataurithi uzima wa milele.

Maran atha!.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?

Nini maana ya usimfunge ng’ombe kinywa apurapo nafaka!.(Kumbukumbu 25:4)

JIEPUSHE NA UNAJISI.

TATIZO LA NDANI LINALOWASUMBUA VIJANA, WALIOOKOKA.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/01/31/maji-ya-farakano-ni-nini-katika-biblia/