TATIZO LA NDANI LINALOWASUMBUA VIJANA, WALIOOKOKA.

TATIZO LA NDANI LINALOWASUMBUA VIJANA, WALIOOKOKA.

Kuna tatizo sugu ambalo linalowasumbua watu wengi , hususani vijana pindi wanapookoka, Na pengine linakusumbua hata na wewe.

Vijana kadha wa kadha waliookoka, wamekuwa wakinipigia  simu, wengine wakinitumia meseji wakisema mtumishi, tangu nilipookoka, nimejitahidi kweli kuacha uasherati na kutazama picha chafu (za ngono) mitandaoni, Lakini naona kama ninamkosea Mungu kwasababu, zile taswira za yale niliyokuwa ninayafanya au ninayatazama, zinanijia mara kwa mara akilini mwangu, wakati mwingine hata wakati nikiwa naomba, au najifunza Neno.

Hivyo naona kama bado sijakamilika, Mungu hajanisamehe na kuniosha dhambi zangu, najisikia vibaya sana, imenipelekea kukosa nguvu ya kumtumikia Mungu.. Nifanye nini?

Kama na wewe umekuwa na tatizo kama hili nataka nikuambie, wewe sio wa kwanza,  Biblia inasema mtaifahamu kweli nayo hiyo kweli itawaweka huru.(Yohana 8:32)

Jambo ambalo wengi hatufahamu ni kuwa, Utakaso wa Mungu  umegawanyika katika sehemu mbili.

  1. Upo utakaso ambao utaupokea moja kwa moja siku ile unapookoka
  2. Upo utakaso ambao Unachukua muda kutimilika.

Tukianzana na huo wa kwanza, zipo hali ndani yako, ambazo Mungu anaziondoa, mara moja pindi tu unapookoka, kwamfano kiu ya kutenda yale maovu uliyokuwa unayatenda huko nyuma, kama vile wizi, matusi, uvaaji mbaya, pombe  n.k.

Lakini upo utakaso ambapo itakupasa upitishwe mahali Fulani kwanza kwa muda, ndipo uwe safi kabisa. Na ndio maana utaona katika agano la kale kuna unajisi ambapo ulikuwa ukishatakasika, ilikupasa usubirie mpaka ifike jioni ndio uwe safi, mwingine siku tatu, mwingine wiki mbili, inategemeana na unajisi wenyewe. Utajiuliza ni kwanini usiwe na saa hiyo hiyo?

Kwamfano embu soma vifungu hivi;

Walawi 11:25” na mtu awaye yote atakayechukua cho chote cha mizoga yao atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni”.

Walawi 15:27 “Na mtu ye yote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.

28 Lakini huyo mwanamke kwamba ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi”.

Sasa katika suala kama hilo, la picha chafu kuondoka ndani yako, hupaswi, kudhani kuwa Mungu hajakusamehe, Umeshasamehewa, dhambi zako, tangu siku ile ulipookoka na kuacha kufanya hayo mambo, lakini ule utakaso kamili haujakamilika ndani yako, hivyo itakuchukua muda kidogo, hivyo kwa jinsi unavyozidi kujitenga na hayo mambo, ndivyo Mungu anakusafisha mpaka utafika wakati hizo picha hazitakujia tena katika akili yako.

Utajiuliza ni kwanini Musa alipelekwa jangwani miaka 40, kabla ya kuitwa kwenda kuwaokoa wana wa Israeli. Ilikuwa ni kwa kusudi la kuondoa, kiburi na majivuno ndani yake  ambayo pengine yasingeweza kuondoka kwa siku moja au wiki moja. Vilevile wana wa Israeli walizungushwa jangwani kwa miaka 40, ilikuwa ni ili kuindoa miungu iliyokuwa mioyo mwao, wajifunze kumtegemea Yehova tu.

Hata gari lililo spidi haliwezi kuchuna breki na kusimamia hapo hapo tu, ni lazima litaendelea mbele kidogo, kwasababu lilikuwa katika mwendo kasi. Halikadhalika, ikiwa umeokoka leo, au hivi karibuni, hizo picha chafu ulizokuwa unazitazama, zilishaiharibu nafsi yako kwa muda mrefu sana, hivyo zinaweza kuchukua muda Fulani mpaka ziondoke kabisa. Ndio ujue dhambi sio jambo la kulichukuliwa kirahisi rahisi tu.

1Wathesalonike 4:3 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;

4 kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;

5 si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu”.

Lakini usihofu wewe endelea kukaa mbali na uchafu wote, na kidogo kidogo, Bwana atayasafisha mawazo yako, na kuna wakati utafika, hata hayo mawazo au hizo picha zitakuwa kama ni Habari za utotoni.

Dhambi  inagharama. Hivyo, usirudi nyuma, wala usifadhaike, songa mbele, zidisha ukaribu wako na Mungu, kaa tu mbali na vyanzo vyote vya uzinzi, tamthilia za kidunia acha, movie zote  zenye maudhui hayo acha, mazungumzo yenye uzinzi ndani yake, kampani za marafiki wahuni achana nazo, mitandao ya kijamii kama instagramu, ikiwa huna jambo la maana unafuata kule, ondoa, kwasababu vingi vilivyomo kule havikujengi,.. vyote hivyo jitenge navyo.. Kwasababu biblia inasema moto hufa kwa kukosa kuni.

Mithali 26:20a “Moto hufa kwa kukosa kuni;..”

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.

MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI.HATA UASHERATI NAO

KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE.

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments