Walakini ataokolewa kwa uzazi wake.

by Admin | 8 February 2022 08:46 pm02

SWALI: Biblia inaposema mwanamke ataokolewa kwa uzazi wake, inamaanisha nini?

1Timotheo 2:14 “Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.

15 Walakini ataokolewa kwa uzazi wake, kama wakidumu katika imani na upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi”.


JIBU: Tofauti na inavyotafsiriwa na watu wengi, kwamba andiko hilo linamaanisha kuwa mwanamke yeyote ambaye atakuwa na watoto wa kulea, basi mwisho wa siku ataokolewa kwa kutimiza tu kusudi hilo.  Mtazamo ambao sio sahihi na unakinzana na maandiko, Kwasababu kama kila mwanamke angekuwa anaokolewa kwa namna hiyo, hata wanawake wachawi nao wangeokolewa kwasababu na wao pia wanao watoto wa kulea.

Lakini biblia ilimaanisha nini kuandika hivyo? 

Mtume Paulo aliandika maneno hayo, kuonyesha jinsi gani huduma ya mwanamke ambaye ana watoto jinsi ilivyo na nguvu hata kusababishia wokovu kwake mwenyewe IKIWA atawalea watoto wake katika misingi ya imani, upendo na utakaso, pamoja na moyo wa kiasi kama ilivyoainishwa hapo..Na sio kwa kuzaa tu basi.

Kwasababu atakuwa ameifanya huduma ya kuokoa kizazi kingine.. Tengeneza picha kama wanawake wote ulimwenguni wangekuwa wanatimiza wajibu wao huu wa kuwalea watoto wao katika misingi ya imani, leo hii, kusingekuwa na haja ya kuhubiri injili kwasababu watoto wote wangekuwa tayari wanamjua Mungu. Lakini injili imekuwa ngumu kwa kizazi cha sasa kwasababu jambo la kwanza mzazi analolithamini kwa mtoto wake ni elimu tu, Mungu ni ziada, mtoto akifaulu darasani ndio furaha yake kubwa, wakati hajui hata mstari mmoja wa biblia. Hajui hata pambio moja la kumsifu Mungu. Mzazi haoni aibu hata mtoto wake anakuwa hadi mtu mzima hajui biblia ina vitabu vingapi.

Kwahiyo hapo mtume Paulo alikuwa anaonyesha nguvu iliyopo katika mwanamke kulea watoto wake vema, ambayo mwisho wa siku itampelekea hata na wokovu wake mwenyewe. Kwamfano Mungu akiona mtoto Yule ambaye alilelewa katika misingi kama Samweli, amekuwa sababu ya wokovu kwa Israeli, unategemea vipi Mungu amwache mama aliyemlea?. Ni sawa tu na yule anayewavuta watu kwa Kristo, ambao biblia inasema kitendo hicho kina nguvu ya kuokoa roho ya mhubiri na kufunika wingi wa dhambi zake.

1Petro 5:20 “jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi”.

Kwahiyo ikiwa wewe ni mwanamke na Mungu kakujalia watoto ujue jukumu lako la kwanza, la injili ni kwa watoto wako, hakikisha hao wanakuwa katika misingi ya kumcha Mungu, wafundishe, na pale wanapokosea Mungu kakupa ruhusu ya kuwaadhibu, lengo ni kuwaweka katika mstari wa kumcha Bwana, na sio kuwatesa. Ukifanya hivyo matokeo yake utakuja kuyaona baada ya haya maisha hapa duniani.

Tito 2:4 “ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;

5 na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MWANAMKE ULIYEKOMAA KI-UMRI, ITAMBUE HUDUMA YAKO.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

Raheli aliwalilia vipi watoto wake?

MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/02/08/walakini-ataokolewa-kwa-uzazi-wake/