Hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.

by Admin | 25 August 2022 08:46 pm08

SWALI: Inakuwaje tunaambiwa mambo mengine tunajaliwa? Na si kwa jitihada zetu, kujaliwa ni nini kibiblia?


JIBU: Kujaliwa maana yake ni kuwezeshwa kufanya jambo ambalo wewe kwa nguvu zako kamwe huwezi kulitenda.

Haya ni mambo ambayo biblia inatuambia mtu anajaliwa kuyafanya.

1) Kupokea wokovu:

Bwana Yesu alisema..

Yohana 6:65 “Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu”.

Alisema maneno hayo, baada ya kuona wengi wa wanafunzi wake wanarudi nyuma kwa maneno yake magumu aliyokuwa anayesema, ya kuinywa damu yake na kuula mwili wake,. Hapo ndipo akasema maneno hayo. Ikiwa na maana kuwa hata sasa ukimwona mtu ameokoka kwelikweli kwa kumaanisha kumfuata Yesu na gharama zake, usidhani ni kwa nguvu zake, ameweza hivyo, hilo jambo halipo, hakuna mwanadamu mwenye asili ya dhambi anayeweza kujiamulia tu kwa akili zake kuamini mambo ya rohoni, asiyoyaona.

Alivutwa kwanza, na Mungu, kisha akapewa uwezo huo wa kukubaliana na vigezo vyake.

Yohana 6:44 “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho”.

2) Kujua siri za ufalme wa mbinguni:

Si kila mtu atapewa kuzielewa siri za ufalme wa mbinguni. Yesu anasema hivyo katika..

Mathayo 13:10 “Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?

11 Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa”.

Hiyo ni baada ya kuwapa mifano kadha wa kadha  ihusuyo ufalme wa mbinguni, bila kuwapa ufunuo wake, isipokuwa wanafunzi wake tu waliomfuata kumuuliza..ndipo akawaambia maneno hayo.

Ndugu kusoma biblia ni moja na kupokea ufunuo wa Mungu wa kweli ni jambo lingine, wapo watu wana elimu kubwa za theolojia, wanajua historia yote ya maandiko, wameirudia biblia mara 1000, kifungu baada ya kifungu, kama ilivyokuwa kwa mafarisayo na masadukayo, lakini wakashindwa kuelewa Neno dogo la ubatizo wa maji, kwamba ni lazima uwe wa kuzamishwa na kwa jina la Yesu. Au kufahamu kuwa sanamu hazipaswi kuhusianishwa ibada yoyote ya Mungu.

Hivyo ukiona wewe umepewa uelewa wa Neno la Mungu, mshukuru sana, wala usijisifu ukadhani ni kwa utashi wako, au uelewa wako mwepesi umeweza kujua hilo, Hapana bali umejaliwa  na Mungu..

3) Kuhudumu.

Kazi yoyote ya utumishi kwa Mungu, iwe ni ya madhabahuni au nje ya madhabahuni, ambayo unaifanya kwake, ujue kuwa, ni kwa nguvu ulizojaliwa na Mungu, wala si zako;

1Petro 4:11 “Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina”.

Si wote, wamepewa nguvu hizo, hivyo tumika kwa uaminifu.

4) Kutooa/kutokuolewa kwa ajili ya Bwana.

Wapo watu ambao Bwana Yesu amewapa uwezo wa kuyatawala mapenzi yao. Hivyo wanaweza kukaa bila kuoa/kuolewa na wasione shida yoyote. Sasa watu wa namna hii, sio kwa nguvu zao bali Bwana Yesu anasema ni kujaliwa.

Mathayo 19:10 “Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa.

11 Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa”.

Hivyo, kwa kuhitimisha ni kuwa uonapo tendo lolote, la ki- Mungu lililogumu kufanyika kwa binadamu wa kawaida, ujue kuwa limetokea kwa kujaliwa na Mungu, na sio kwa nguvu za  mtu yule.

Tukiyafahamu haya, basi tutajifunza kuitii sauti ya Mungu, na kumwomba sana, na kuwa wanyenyekevu ili asitupite, kama hatutajaliwa na Mungu, haijalishi tutahubiriwa injili mara ngapi, tutaona miujiza mingi kiasi gani, tutatokewa na Yesu mara ngapi, kamwe hatuwezi kubadilika, Farao aliona miujiza mkubwa sana kutoka kwa Musa, lakini Mungu hakumpa moyo wa kutubu.

Yuda alikuwa ni mtume ambaye hakutokewa na Yesu,(linaweza likawa ni jambo dogo) bali aliishi na Yesu kabisaa kwa miaka mitatu na nusu, lakini bado ndani yake kulikuwa hakuna badiliko la dhati, na ndio maana akaja kumsaliti baadaye.

Yohana 17:12 “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie”.

Hivyo uisikiapo sauti ya Mungu inaugua ndani yako, usiipuzie hata kidogo, chukua hatua haraka badilika. Kubali kutubu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, Upokee kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwasababu hiyo sauti haitadumu milele ndani yako. Upo wakati itanyamaza kimya. Hivyo maanisha kumtii Mungu.

Bwana atasaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya ugonjwa wa kufisha? (Yeremia 17:9)

USIMPE NGUVU SHETANI.

Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?

Wala msimwite mtu baba duniani;..Hapo Bwana wetu Yesu anamaanisha nini kusema hivyo?

Kwanini Bwana Yesu alivikwa taji ya miiba?

Kiyama ni nini?

Je! Siku ya unyakuo watoto wachanga watanyakuliwa?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/25/amejaliwa-na-baba-yangu/