JINSI WATU WANAVYOIUNDA SANAMU YA NDAMA MIOYONI MWAO.

by Admin | 25 November 2022 08:46 pm11

Mambo yaleyale waliyokuwa wanayafanya wana wa Israeli walipokuwa jangwani, yanafanywa sasa na wana wa Mungu. Ni vizuri tukafahamu asili ya ile ndani jinsi ilivyoundwa, ili tuelewe kwa undani, inavyoundwa sasa mioyoni mwa watu.

Maandiko yanatuonyesha, hawakuwa na rasilimali zozote za kuitengeneza, vilevile hawakuwa na urahisi wowote wa kuifanyia karamu yake, kwasababu pale palikuwa ni jangwani, hakuna namna wataweza kupika vyakula vizuri, pamoja na kupata pombe za kuifurahisha ibada yao.

Lakini cha ajabu ni kuwa, japokuwa changamoto hizo zilikuwepo, lakini vyote hivyo vilipatikana, na mambo yakaenda vizuri kabisa bila shida. Ndama akatengenezwa tena sio wa mawe bali wa dhahabu, vilevile Vinywaji vilipatikana(pombe zote) pamoja na vyakula vya kila namna? Na disco la miziki na vinanda juu vikawekwa.

Kutoka 32:2 “Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee.  3 Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni.  4 Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri.  5 Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Haruni akatangaza akasema, Kesho itakuwa sikukuu kwa Bwana.  6 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze”.

Utajiuliza vilipatikanaje?

Hii ni kuthibitisha kuwa nafsi ya mtu ikidhamiria kutafuta jambo Fulani, ni lazima itapata tu haijalishi mazingira iliyopo.

Ndicho walichokifanya hawa.. Walipohitaji dhahabu, wakakumbuka kuwa wake zao, wanazo kwenye masikio yao, wanazo kwenye shingo zao.. Hivyo wakazitumia hizo hizo na kuzikusanya, zikawa nyingi, mno, wakampa Haruni akaziyeyusha na matokeo yake ikatokea ndama kubwa iliyong’aa sana.

Biblia haijatuambia pombe na vyakula vizuri walivitolea wapi, lakini ni wazi kuwa, waliagiza watu, waende nje ya jangwa kununua vyakula hivyo na pombe, katika miji ya kandokando huwenda muasisi alikuwa ni Kora au mwingine.. Au pengine wakatoa baadhi ya hizo dhahabu wakanunua. Lakini kwa vyovyote vile, na kwa njia yoyote ile, shughuli ilikamilika.

karamu ilikuwepo, watu walikula, walikunywa walisaza..na zaidi sana Sanamu yenye utukufu ilitengenezwa. Akili hizo hawakuwahi hata sikumoja kuzielekeza kwa Mungu wao aliyewaokoa kwa gharama kubwa sana kutoka kwa watesi wao wamisri, hawakuwahi kufikiria kumfanyia Mungu karama ya shukrani kama hiyo wale na wanywe mbele ya Yehova kwa matendo makuu aliyowatendea..

Hata kufikiria kutengeneza kibanda kidogo tu cha udongo kwa ajili ya Mungu wao kukutana nao, kuliko Musa kupanda huko milimani, na kutoweka muda mrefu,hawakuwahi kufikiri hivyo, wanakuwa wepesi kuwaza kuunda miungu ya dhahabu ambayo haijawahi kuwasaidia kwa chochote..Unadhani Kwa namna hiyo wangeachaje kumtia Mungu wivu?

Mambo kama haya yanaendelea sasa miongoni mwa wakristo..

Tukisikia harusi Fulani inafungwa, tunakuwa wepesi kubuni kila namna ya kuifanya ipendeze, tunaweza kutoa hata michango ya milioni moja, na kutengeneza kamati nzuri za maandalizi, tunatoa mapendekezo haya au yale, mpaka inatokea na kuvutia, hata kama ilikuwa ni ya bajeti ndogo lakini itafanikiwa tu mwisho wa siku..Lakini kwa Mungu aliyetukomboa, aliyetufia msalabani, ambaye kila siku anatupigania usiku na mchana, anatupa pumzi yake bure, hatuna muda naye..Zaidi tunaitazama nyumba yake, au kazi yake, tunaona kabisa ipo katika hali ya unyonge, lakini tunapita tu,kama vipofu, tunasema Mungu mwenyewe atatenda..

Tukiangalia tulivyovichangia katika mambo yasiyo ya msingi ni vingi kuliko tulivyovipeleka kwa Mungu. Ndugu tukiwa watu wa namna hii hapo tuwe na uhakika kuwa tumeunda sanamu za ndama nyingi, na tunaziabudu bila kujua. Na zimemtia sana Mungu wetu wivu sana.

Kukitokea party, au birthday, au tafrija Fulani, ni wepesi sana kuutikia, lakini kwa Mungu ni mpaka tukumbushwe kumbushwe, tuvutwe vutwe.. Hii inasikitisha sana.

Embu hii Ndama ya dhabahu tuivunje.. Hii miungu tuiondoe ndani yetu, mioyo yetu itusute.. Tumpe Mungu kipaumbele cha kwanza, kwasababu yeye ndio anayestahili kuliko hao wengine. Tusiwaone wale ni wajinga sana kuliko sisi. Huwenda wale wanao unafuu mkubwa zaidi ya sisi ambao tumeshaona mifano lakini tunarudia mambo yaleyale.

Tumpende Mungu, tuuthamini na wokovu wake, tuithamini pia na kazi yake.

EFATHA.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Baali alikuwa nani?

Hema ya kukutania ni nini, na ilikuwaje?

Maashera na Maashtorethi ni nini?

Kusubu ni nini? Miungu ya kusubu ni ipi?

Ayala, Paa na Kulungu ni wanyama gani?

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/25/jinsi-watu-wanavyoiunda-sanamu-ya-ndama-mioyoni-mwao/