Biblia inaposema Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, Inamaana gani?

by Admin | 25 June 2023 08:46 pm06

SWALI: Biblia ilimaanisha nini iliposema Kaini ‘Akatoka mbele ya uso wa Bwana’. Kutoka kule kulimaanisha nini?


JIBU: Tunaona baada ya Kaini kumuua ndugu yake Habili kwa wivu, ambao ulizuka baada ya sadaka yake kukataliwa na ya ndugu yake kukubaliwa. Mungu alimsemesha, na kumweleza laana yake itakayompata baada ya pale. Lakini mwisho wa maneno yale, Tunaona Kaini anaonekana akitoka mbele ya uso wa Bwana. Maana yake ni nini?

Tusome.

Mwanzo 4:9 “Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? 

10 Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.  11 Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;  12 utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. 

13 Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.  14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. 

15 Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga.  16 Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni”

Alitokaje?

Kutoka mbele ya uso wa Bwana hapo, sio Kuahirisha mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea baina yake yeye na Mungu hapana. Bali ni kumwacha Mungu moja kwa moja. Yaani kwa ufupi mkataba wake na Mungu aliumalizia pale. Hakuna cha dhabihu tena wala sadaka, wala kumwomba Mungu, wala kujihusisha na tendo lolote la kiibada. Akaanza kujishughulisha na mambo ya kidunia tu, na sayansi, na utafiti na uvumbuzi, na akafanikiwa sana katika bidii yake hiyo, yeye na uzao wake wote, wakawa watu hodari duniani, lakini waovu sana (Soma Mwanzo 4:20-22). Na hawa ndio waliopelekea gharika kuletwa duniani.

Tofauti na uzao wa Adamu kwa Sethi, wao waliendelea kuwepo mbele ya uso wa Bwana, wakitaka fadhili na rehema kwa Mungu daima,wakiliitia jina lake.

Mwanzo 4:25 “Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.  26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana”.

Mpaka sasa makundi haya mawili yapo duniani. Lipo ambalo halina habari na Mungu,(Ambao ndio uzao wa Kaini rohoni) bali mambo ya kidunia tu, na limefanikiwa sana katika hayo, ni jepesi katika uvumbuzi na utafiti, lakini  Mungu kwao ni kama historia za mababu wa kale, ni kama vile mashariki na magharibi zilivyo mbali. Lakini sisi hatupaswi kufanana wa watu hao. Bali kama Watoto wa Adamu kwa Sethi. Furaha yetu ipo katika Bwana. Tegemeo letu ni yeye, na nguvu zetu ni yeye, haijalishi tutakosa vyote au tutapata vyote. Yeye ndiye atakayekuwa urithi wetu milele.

Je! Wewe upo kundi lipi?   Uthibitisho ni maisha yako ulipoyaelekeza.

Hizi ni nyakati za mwisho. Kristo anarudi. Tubu mgeukie Bwana, mtafute yeye.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Bustani ya Edeni ipo nchi gani?

FAHAMU MAISHA YA YESU KABLA YA HUDUMA.

Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?

Mtu wa kwanza kufa alikuwa nani?

JE! Kaini alimpatia mke wake wapi?

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/06/25/biblia-inaposema-kaini-akatoka-mbele-za-uso-wa-bwana-inamaana-gani/